Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano nchini DRC yanaathiri raia :UNHCR

Charline (kushoto) mwenye umri wa miaka 11 amekimbia mapigano huko Bunagana jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC na kukimbilia eneo la Rutshuru yeye na familia yake. (Maktaba)
©UNICEF/Jean-Claude Wenga
Charline (kushoto) mwenye umri wa miaka 11 amekimbia mapigano huko Bunagana jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC na kukimbilia eneo la Rutshuru yeye na familia yake. (Maktaba)

Mapigano nchini DRC yanaathiri raia :UNHCR

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limeendelea kutoa wito wa sitisho la mashambulizi dhidi ya raia jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako matukio hayo yameendelea kusababisha vifo miongoni mwa raia. 

UNHCR imetolea mfano tukio la tarehe 12 mwezi huu wa Julai huko Rwangoma mjini Beni lililosababisha vifo vya watu 6 na Zaidi ya 1,000 kukimbia ili kusaka usalama.

Kupitia taarifa iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi hii leo msemaji wa UNHCR Boris Cheshirkov amesema mashambulio hayo yanafanywa na vikundi vya kiraia vilivyojihami na ni pamoja na huko jimboni Ituri, mashambulio ambayo yanalenga raia. 

Kando mwa hayo yanayofanywa na vikundi vilivyojihami, UNHCR imetaja pia mapigano kati ya jeshi la serikali ya DRC na kikundi cha waasi cha M23 huko Goma jimboni Kivu Kaskazini ambayo pia yanatishia hali ya usalama ukanda wa Maziwa Makuu.