Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CSW ni jawabu la usawa na maendeleo endelevu duniani- Guterres

Ufunguzi wa mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani 11 Machi 2024 New York, Marekani.
UN /Manuel Elias
Ufunguzi wa mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani 11 Machi 2024 New York, Marekani.

CSW ni jawabu la usawa na maendeleo endelevu duniani- Guterres

Wanawake

Jukwaa la Kamisheni ya Wanawake duniani, CSW, ni kichocheo cha mabadiliko tunayohitaji, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres hii leo wakati wa ufunguzi wa mkutano 68 wa Kamisheni hiyo, CSW68 jijini New York, Marekani mkutano utakaofanyika kwa wiki mbili.

Guterres amesema katika zama hizi ngumu na migawanyiko mikubwa, hebu na tutokomeza umaskini katika nyanja zote kwa kuwekeza kwa wanawake na wasichana, na kushinikiza ili amani na utu kwa wanawake vipatikane pembe zote za dunia.

Katibu Mkuu ametanabaisha kuwa dunia inapitia nyakati ‘zenye mawimbi’ makubwa na kwamba wanawake na wasichana ndio wameathiriwa zaidi.

Kwenye maeneo ya mizozo na vita duniani kote, wanawake na wasichana wanadhurika zaidi na vita vilivyoanzishwa na kuendelezwa na wanaume.

“Maelezo yako dhahiri na wazi: Wanawake wanaongoza kupatikana amani. Bajeti na sera zinapaswa kufuatia –zikiwa na malengo makubwa kwa ajili ya ushiriki wa wanawake na uwekezaji wa adharura kwenye harakati za wanawake za ujenzi wa amani,” amesema Katibu Mkuu.

Ameongeza kuwa wanawake na wasichana wengi wanakabiliwa na vita dhidi ya haki zao za msingi iwe majumbani mwao na hata kwenye jamii zao. Maenedeleo yaliyopatikana kwa mapambano makali sasa yanarudishwa nyuma.

“Hatuwezi kukubali dunia ambamo bibi watahofia kuhusu mustakabli wa wajukuu zao wa kike watafurahia haki chache kuliko walizofurahi wao. Lazima tupaze sauti tena kwa wazi. Isitokee sisi tukiwa tunatazama,” amesema Guterres.

Tweet URL

Akili Mnemba imetawaliwa na wanaume, tuchukue hatua

Kuhusu teknolojia, hasa matumizi ya Akili Mnemba au AI, Katibu Mkuu amesema katika zama za sasa ni wanaume ndio wanatawala teknolojia hiyo kama viongozi na katika ngazi ya kiufundi.

“Matumizi hayo ya teknolojia ya AI yanaweza kutumiwa na wanaume kuongoza mipango kuanzia mipango miji hadi upatikanaji wa mikopo bila kusahau tiba. Hii itakuwa na hatari kwa wanaume, wavulana, wanawake na wasichana.

“Ni wakati kwa serikali, mashirika ya kiraia na wataalamu wote wa teknolojia duniani kote kuunganisha juhudi zao ili kuziba pengo la kidijitali kati ya wanawake na wanaume na kuhakikisha wanawake wana fursa ya kuamua kuhusu masuala ya teknolojia za kidijitali,” amesema Katibu Mkuu.

Wanawake ndio taswira ya umaskini

Amegusia pia umaskini duniani akisema una taswira ya mwanamke. Nategemea msaada wa serikali katika marekebisho ya mfumo wa fedha duniani wakati wa mkutano wa zama zijazo utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu ili mfumo wa fedha duniani uendane na uchumi wa sasa duniani na ukidhi mahitaji ya nchi zinazoendelea na hatimaye ziweze kuwekeza kwa wanawake na wasichana.

Na serikali kwa upande wao zina wajibu wa kuwekeza kwenye kutokomeza umaskini na kufikia maendeleo jumuishi na endelevu kwa wote.

Amesisitiza kuwa kuchagiza usawa wa kijinsia kwa kutokomeza umaskini kunahitaji ushiriki kamilifu wa wanawake na uongozi wao kwenye taasiis za fedha.

Guterres ametoa takwimu akisema zaidi ya mawaziri wa fedha 8 kati ya 10 ni wanaume. Zaidi ya magavana 9 kati ya 10 wa Benki Kuu ni wanaume.

Tusaidie vijana wanawake badala ya kuwakandamiza- Stacey

Stacey Mdala, mwanasayansi wa takwimu kutoka Malawi, ni Mwakilishi wa Vijana ambaye naye alipata fursa ya kuhutubia ufunguzi wa CSW68 .

Ametumia hotuba yake kusihi kuwa “kila mmoja wetu kuchukua juhudi za makusudi kutusaidia sisi vijana kuendelea kulinda utofauti wetu, kutulinda dhidi ya aina zote za ubaguzi na unyanyasaji kwa sababu tunataka kusikika.”

Mdala pia amesihi viongozi kuwekeza kwa wanawake na wasichana kwenye uhandisi, sayansi na hisabati au STEM.

“Tunataka usawa katika upangaji na uelekezaji wa rasilimali. Na tunataka usawa katika fursa hizo zote. Wezesha wanawake vijana na wasichana. Hebu na tuwe washirika wao na si wapinzani. Hebu na tuwasaidie badala ya kuwakandamizi,” alitamatisha hotuba yake.

Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW68  kwenye makao makuu ya UN jijini New York, Marekani.
UN /Manuel Elias
Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW68 kwenye makao makuu ya UN jijini New York, Marekani.

Sitisho la mapigano Gaza: Bahous

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women ambalo ndio limeandaa mkutano huu, Sima Bahous ametaka sitisho la mapigano Gaza haraka iwezekanavyo.

“Natoa wito pia wa ufikishaji haraka na kwa usalama kwa misaada ya kiutu eneo lote la Gaza, kuachiliwa kwa mateka wote na kukomeshwa kwa ukaliaji na kurejea kwa mwelekeo wa kusaka amani ambao una haki na jumuishi kwa ajili ya sauti za wanawake,” amesema Mkuu huyo wa UN Women.

Amesema hilo ndilo tumaini pekee kwa mustakabali unahitajika.

Ni kwa vipi wanawake wanaweza kuondolewa kwenye lindi la umaskini

Bahous pia amesema “zaidi ya wanawake na wasichana milioni 100 wanaweza kuondolewa kwenye lindi la umaskini iwapo serikali zitapatia kipaumbele elimu, huduma za afya, ujira wa haki na wa usawa na kupanua wigo wa hifadhi ya jamii.

“Kuziba pengo la jinsi na ajira kunaweza kuongeza pato la ndani la taifa kwa asilimia 20 kwenye maeneo yote duniani,” amesema Bi. Bahous.

Amesema faida ya uwekezaji kwenye usawa wa jinsi ni dhahiri na wazi na ni Ushindi kwa jamii nzima na pia kiuchumi.

Maudhui yanayopatiwa kipaumbele kwenye mkutano huo wa CSW68 ni Chagiza mafanikio ya usawa wa jinsia na wezesha wanawake wote na wasichana kwa kutatua suala la umaskini na imarisha taasisi na ufadhili kwa misingi ya kijinsia.