Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama limepitisha azimio la kutaka kusitishwa uhasama Sudan wakati wa Ramadhani

Baraza la Usalama lakutana kujadili hali ya Sudan na Sudan Kusini
UN Photo/Manuel Elías
Baraza la Usalama lakutana kujadili hali ya Sudan na Sudan Kusini

Baraza la Usalama limepitisha azimio la kutaka kusitishwa uhasama Sudan wakati wa Ramadhani

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio la kutaka kusitishwa kwa uhasama nchini Sudan wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Azimio hilo lililowasilishwa leo na Uingereza, likitaka kusitishwa mara moja kwa mapigano nchini Sudan katika mwezi wa Ramadhani na pande zote katika mzozo huo kutafuta suluhu endelevu kupitia mazungumzo limeungwa mkono na wanachama 14  kati ya wjumla ya wajumbe 15 wa Baraza hilo na mjumbe mmoja ambaye ni  Urusi imejizuia kutoshiriki katika kura hiyo kwenye Baraza la Usalama.

Akizungumza baada ya upigaji kura naibu mwakilishi wa kudumu wa Uingereza Kwenye Umoja wa Mataifa James Kariuki amesema “ Tunawahimiza Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF kuchukua hatua kutekeleza kwa wito huu wa umoja wa Mataifa wa amani na kunyamazisha mtutu wa bunduki. Pia tuzazihimiza pande zinazozozana kujenga imani na kutafuta suluhu endelevu kwa mzozo huo kupitia mazungumzo.”

Naye Naibu mwakilishi wa kudumu wa Urusi Kwenye Umoja wa Mataifa mwanachama ambaye alijizuia kupiga kura hiyo amesema “Urusi ilijizuia wakati wa kupiga kura kuhusu azimio hilo lililowasilishwa na Uingereza la kusitisha uhasama nchini Sudan. Tuliamua kuruhusu azimio hili lipite kwa sababu ni suala la maisha ya watu wa Sudan ambao wanateseka kote nchini kutokana na matokeo ya mzozo unaoendelea. Kukomesha ghasia nchini Sudan bila shaka kunapaswa kuwa lengo kuu sio tu kwa Baraza la Usalama, lakini muhimu zaidi kwa watu wa Sudan wenyewe.”

Kuhusu azimio hilo

Azimio hilo linatoa wito kwa pande zote “kuhakikisha kwamba vikwazo vyovyote vinaondolewa na kwamba fursa kamili ya kibinadamu ya ufikiaji wa haraka kwa wenye uhitaji wa misaada ya kibinadamu, kwa usalama na kusikozuiliwa wa kunawezeshwa, ikiwa ni pamoja na kuvuka mipaka na njia za mawasiliano, na kuzingatia wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa za kibinadamu.”

Sheria hizo za kimataifa ni pamoja na wajibu wa kulinda raia na miundombinu ya kiraia, na ahadi chini ya Azimio la Kujitolea Kulinda Raia nchini Sudan, linalojulikana kama "Azimio la Jeddah."

Azimio hilo linahimiza Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Ramtane Lamamra, kutumia ofisi zake nzuri na washirika n anchi jirani ili kukamilisha na kuratibu juhudi za amani za kikanda.