Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DARFUR: Kwa vipi imekuwa janga la kibinadamu na mgogoro wa haki za binadamu

Walinda amani kutoka UNAMID wakitoa ulinzi kwa wanawake wenyeji wa kijiji cha Aurokuom eneo la Zalingei, Darfur Kati. (Maktaba)
UNAMID/Amin Ismail
Walinda amani kutoka UNAMID wakitoa ulinzi kwa wanawake wenyeji wa kijiji cha Aurokuom eneo la Zalingei, Darfur Kati. (Maktaba)

DARFUR: Kwa vipi imekuwa janga la kibinadamu na mgogoro wa haki za binadamu

Amani na Usalama

Kuzuka kwa mzozo miezi 9 iliyopita nchini Sudan kumesababisha "Muungano wa janga la kibinadamu linalozidi kuwa baya na mgogoro mkubwa wa haki za binadamu", kwa mujibu wa afisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa na eneo la Darfur limeathiriwa vibaya sana.

Takriban watu milioni tisa wanahitaji msaada wa kibinadamu huko na duru za habari zinaonyesha kuwa watu wengine wapatao 4,000 wamelengwa na kuuawa kwa sababu ya makabila yao.

Sasa kuna wasiwasi kwamba Darfur inarejea katika miaka ya mapigano ya kikatili yaliyoshuhudiwa miongo miwili iliyopita ambayo yalisababisha vifo vya watu 300,000 na mamilioni ya watu wengine kuyahama makazi yao.

Mambo 5 kuhusu janga la kibinadamu Darfur

  1. Mzozo wa Darfur ni janga la kibinadamu linaloathiri zaidi ya watu milioni 8
  2. Kuongezeka kwa ghasia kunazua hofu ya kurejea kwa ukatili wa mwaka 2003 wakati waasi walipoipinga serikali ya Sudan. Watu wapatao 300,000 walipoteza Maisha, mamilioni walifurushwa makwao na wakimbizi 400,000 walilazimika kukimbilia nchi jirani.
  3. Vurugu zilipungua mara kwa mara wakati wa ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika UNAMID. UNAMID ilifanya kazi kuanzia 2007 hadi 2020.
  4. Aprili 2023 mzozo ulizuka upya kati ya jeshi la Wapiganaji wa Msaada wa Haraka (RSF) na Wanajeshi wa jeshi la serikali ya Sudan (SAF). Mamilioni ya watu wamekimbia makazi yao au kukimbilia nchi jirani
  5. Mashirika 5 ya Umoja wa Mataifa yametaka pande zote kusitisha uhasama na kuruhusu utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa usalama na kwa haraka.