Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano Khartoum; UN yataka yasitishwe ili kunusuru raia

Mji mkuu wa Sudan, Khartoum (Picha ya Maktaba)
UN News/Abdelmonem Makki
Mji mkuu wa Sudan, Khartoum (Picha ya Maktaba)

Mapigano Khartoum; UN yataka yasitishwe ili kunusuru raia

Amani na Usalama

Kufuatia ripoti ya mapigano katika ya vikosi vya jeshi vinavyopingana kwenye mji mkuu wa Sudan, Khartoum, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo wametoa taarifa za kulaani vikali ghasia hizo huku maafisa wengine waandamizi wakielezea wasiwasi wao.

Kauli za viongozi hao zinafuatia ripoti ya kwamba Jumamosi asubuhi, kuliibuka mapigaon kati ya kikosi cha jeshi kiitwacho Rapid Support Forces (RSF) na jeshi la serikali ya Sudan, Sudanese Armed Forces (SAF) kwenye maeneo mengi ya mji huo mkuu.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa RSF wanadai kuwa wamedhibiti uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum, halikadhalika uwanja wa ndege wa Merowe, uwanja wa ndege wa al-Obeid na Kasri ya Rais.

RSF ni jeshi huru nchini Sudan, ambalo limechipuka kutoka wanamgambo wa Janjaweed waliokuwa zamani wameshika hatamu kwenye jimbo la Darfur nchini humo.

Jeshi hilo huru limekuwa likishiriki kwenye mazungumzo yenye lengo la kuanzisha kipindi cha mpito kuelekea serikali ya kiraia kutoka utawala wa kijeshi uliokuwa madarakani tangu mwaka 2021 kulikofanyika mapinduzi ya kijeshi.

Sitisheni chuki

Kwa mujibu wa taarifa  iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na msemaji wa Katibu Mkuu, Bwana Guterres anatoa wito kwa viongozi wa RSF na SAF kusitisha mara moja chuki, warejeshe utulivu na kuranza mazungumzo ili kurejea kwenye mwelekeo wa mpito wa kuweka serikali ya kiraia.

Ujumuishaji wa RSF kwenye jeshi la serikali limekuwa moja ya jambo linalojadiliwa, kama sehemu ya mkataba wa kisiasa ulioratibiwa na Umoja wa Mataifa na kutiwa saini mwezi Februari baada ya miezi lukuki ya mashauriano.

Hata hivyo, akihutubia Baraza la Usalama  tarehe 20  mwezi uliopita wa Machi, Volker Perthes, ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan na Mkuu wa ujumbe wa UN wa kufanikisha mpito nchini Sudan, (UNITAMS), alionya kuwa mvutano kati ya jeshi la serikali na RSF umeongeza katika wiki za karibuni na kutoa wito wa kusitishwa kwa mwelekeo huo.

Katika staarifa yake  kuhusu mapigano ya sasa, Bwana Perthes amewasiliana na pande zote na kuwasihi wasitishe mara moja mapigano na wahakikishe usalama wa wananchi wa Sudan na kuepusha nchi hiyo na vurugu.

Ghasia zaidi zitafanya hali kuwa mbaya zaidi

Bwana Guterres pia ameonesha wasiwasi wake kuhusu madhara ya kuendelea kusambaa kwa mapigano kwa raia akisema kutazidisha machungu kwa raia ambao tayari hivi sasa hali ya kibinadamu ni mbaya nchini humo.

Wasiwasi huo pia umeonesha Jumamosi na Mratibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Martin Griffiths kupitia ujumbe wake uliochapishwa kwenye Twitter.

Katika  ujumbe huo , Bwana Griffiths amesema ghasia zadi kutaongeza ‘chumvi kwenye kidonda’ kwa takribani watu milioni 16 nchini Sudan ambao ni takribani theluthi moja ya watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu.

Kwa upande wake Volker Türk, Kamisha Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu naye kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema wananchi wa Sudan wanastahili jambo bora zaidi. Sauti yenye tafakuri inahitajika haraka ili kukomesha ghasia na kurejea kwenye njia ya matumaini ya amani na mpito wa kuwa na utawala wa kiraia.