Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu na Amani: Wakimbizi waelezea jinsi elimu ilivyobadili mtazamo wao hasi dhidi ya watu wengine

Aristote Muhawe ni mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akiishi katika makazi ya wakimbizi ya Kyangwali magharibi mwa Uganda. Hapa anasoma shule ya sekondari pamoja na wakimbizi kutoka Sudan Kusini.
UN News
Aristote Muhawe ni mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akiishi katika makazi ya wakimbizi ya Kyangwali magharibi mwa Uganda. Hapa anasoma shule ya sekondari pamoja na wakimbizi kutoka Sudan Kusini.

Elimu na Amani: Wakimbizi waelezea jinsi elimu ilivyobadili mtazamo wao hasi dhidi ya watu wengine

Utamaduni na Elimu

Nafasi ya elimu katika kuchagiza amani miongoni mwa wakimbizi na  jamii zinazowahifadhi imedhihirika huko Uganda wilayani Kikuube magharibi mwa nchi ambako kuna makazi ya wakimbizi ya Kyangwali. Hilo limethibitika wakati huu dunia kesho Januari 24 ikiadhimisha siku ya elimu duniani maudhui yakiwa kujifunza kwa ajili ya amani. 

Elimu imenisaidia kuondokana na fikra potofu dhidi ya watu wa nchi zingine  

Aristote Muhawe, kijana mkimbizi kutoka Jamhuri ua Kidemokrasia ya Congo (DRC) amesema elimu imemsaidia kubadili mtazamo wake kuhusu mambo mengi hasa watu kutoka nchi tofauti na tamaduni tofauti.  

“Nilikuwa nikiona mtu mkwa mfano mweusi na mrefu sana na kuhisi kuwa si mtu mzuri wa kukaa naye. Lakini unapokuwa shuleni kwenye mijadala unakuta kwamba ni mtu mzuri na mnakaa pamoja kwa amani. Shule zinatusaidia sana kukuza umoja na kuepuka uauzi wa aina yoyote ile,” amesema Muhawe.  

Nafasi ya elimu katika kujenga amani haiwezi kupuuzwa- UNHCR  

Shirika la Umoja wa Mataufa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini humo linasema umuhimu wa kudumisha elimu hauwezi kupuuzwa katika juhudi za kuchagiza amani hasa kwenye makazi hayo ya wakimbizi yanayohifadhi wakimbizi kutoka Sudan Kusini na DRC.  

Akizungumza na John Kibego wa redio washirika  - Kazi-njema redio, Olga Nora Ruza, afisa anayehusika na masaula ya elimu kutoka UNHCR kwenye makaazi ya wakimbizi ya Kyangwali amesema licha ya changamoto za uhaba wa rasilimali, wanashirikiana na wadau wote kuhakikisha watoto wanaendelea wanahudhuria shule.  

Ameongeza kuwa wanahakikisha kuwa hata wale ambao hawakuhudhuria elimu ya msingi, wanawatafutia fursa za kupata ujunzi wa aina mpalimbali wa kiufundi ili waweze kustawi na kuishi kwa amani.  

Tophace Chaali, Kamandanti wa makazi ya wakimbizi ya Kyangwali magharibi mwa Uganda kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu nchini Uganda akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.
UN News
Tophace Chaali, Kamandanti wa makazi ya wakimbizi ya Kyangwali magharibi mwa Uganda kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu nchini Uganda akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

“Tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha elimu inaendelea kwani ni njia muhimu ya kuhakikisha amani na ustawi miongoni mwa wakimbizi. Unajua hao ni watu waliotoka katika nchi zenye migogoro na wakipata ujuzi fulani wanastawi na amani inadumu,” amesema Bi Olga.  

Ameongeza kuwa kutokana na changamoto ya msongamano wa wanafunzi madarasani, wamekubaliana na wizara ya elimu ya Uagnda kuwagawanya watoto hao wasome kwenye awamu tofauti.  

Kiu ya elimu yasababisha wanafunzi kusoma kwa awamu  

“Wengine wanasoma asubuhi huku awamu ya pili ikikaribishwa adhuhuri. Tunawahamasisha wazazi katika jamii kuhusu hilo na wanaitikia. Walimu pia tunawapatia mafunzo ya kuweza kusimamia darasa lenye iddi kubwa ya wanafunzi,” amesema afisa  huyo wa UNHCR.  

Tweet URL

Amani miongoni mwa wakimbizi ni amani kwa jamii na taifa zima Uganda  

Naye Tophace Chaali, Kamandanti wa makazi haya ya wakimbizi ya Kyangwali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu nchini Uganda amefichua kuwa shule moja ya msingi itwayo Mara-tatu imesheheni wanafunzi 7,000 ambao wanakumbana nao kuwafunza.  

Amesema ingawa inaonekana kuwa ni vigumu, wamezoea na sasa elimu inaendelea.  

Kwa mujibu wake, amani katika jamii ya wakimbizi ni amani katika jamii ya wenyeji na pia amani ya kitaifa.  

Bi Chaaali ameongeza kuwa kama serikali, wamekuwa wakihakikisha kuwa harakati zote zinazolenga kuchagiza amani na amendeleo katika makaazi ya wakimbizi, wenyeji pia wanahusishwa.  

“Kwenye sherehe za kitaifa na Kimataifa, wakimbizi na wenyeji wanasjirikiashwa, michezo ya kitamaduni, chakula na kadhalika hata shuleni wanashirikishwa,” asema Bi Chaali.  

Naye Antonia Nyirakabanza, mwalimu mkimbizi kwenye shule ya msingi ya Kasonga anasema, kuna wakati maalumu kila asubuhi wa kuwafunza watoto kuhusu umuhimu wa kuishi kwa amani na pia kwendelea na elimu.  

“Kuna wakati wa ushauri wa watoto hao tukijikita kwenye suala la amani. Tunawahimiza kuendelea na elimu kwani ndio wanakuwa watu wa maana katika jamii,” alisema Nyirakananza.