Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makazi ya wakimbizi Uganda yatumia elimu kusongesha amani miongoni mwa wakimbizi

Makazi ya wakimbizi ya Kyangwali yaliyoko wilaya ya Kikuube magharibi mwa Uganda.
UN News
Makazi ya wakimbizi ya Kyangwali yaliyoko wilaya ya Kikuube magharibi mwa Uganda.

Makazi ya wakimbizi Uganda yatumia elimu kusongesha amani miongoni mwa wakimbizi

Utamaduni na Elimu

Nchini Uganda katika makazi ya wakimbizi ya Kyangwali wilaya ya Kikuube magharibi mwa taifa hilo, suala la mchango wa elimu kwenye amani liko dhahiri kwani tulipotembelea katika makazi hayo, Yahya Kato ambaye ni Mwalimu Mkuu katika Shule ya msingi Kasonga kwenye makazi hayo ya wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Sudan anazungumzia kile wanachofanya. 

Amesema wanachofanya wao kuchagiza amani ni kwamba wanasaidia watoto hapo shuleni kwa kuwakusanya pamoja, wakongomani wakiwemo wagegere ambalo ni moja ya kabila kutoka DRC lijulikanalo pia kama wahema na wasudan kusini ambapo wanasoma pamoja, wanacheza pamoja, wanakula pamoja na wakifanya kila kitu.  

Nchini DRC wagegere au wahema wamekuwa na migoogoro ya mara kwa mara ya kikabila na wenzao wa jamii ya walendu. 

Mwalimu Kato amesema kwa kufanya hivyo, watoto hao  wanaanza kujua mapema kwamba inawezekana kuishi kwa amani bila ukabila. 

Akaenda mbali zaidi kuelezea umuhimu wa kuanzia kufundisha amani shuleni akisema kuwa “tunadhani kwamba ikianza shuleni itasaidia jamii zetu. Watoto wakipata marafiki kwenye shule, kwa mfano hapa kwetu kwani shule yetu si ya bweni bali ya kutwa. Watoto wanasoma na wanarudi nyumbani. Mkongomani anapata rafiki msudani. Hii inasaidia jamii zetu kuanza kuishi pamoja kwa amani.”