Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majanga duniani ni matokeo ya kushindwa kuchagua jambo sahihi la kufanya - Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia mkutano wa viongozi wa Umoja wa Nchi zisizofungamana na Upande Wowote, NAM huko Kampala, Uganda, 20 Januari 2024
UN
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia mkutano wa viongozi wa Umoja wa Nchi zisizofungamana na Upande Wowote, NAM huko Kampala, Uganda, 20 Januari 2024

Majanga duniani ni matokeo ya kushindwa kuchagua jambo sahihi la kufanya - Guterres

Amani na Usalama

Mapigano, umaskini, ukosefu wa usawa, mivutano ya kijiografia na kisiasa, na janga la tabianchi ni matokeo ya kile ambacho dunia inachagua kufanya au inashindwa kuchagua kufanya, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres hii leo huko Kampala nchini Uganda. 


 

Tweet URL

Akihutubia mkutano wa 19 wa Umoja wa nchi zisizofungamana na  upande wowote, NAM, Guterres amesema licha ya changamoto zote hizo, dunia ikiongozwa na maamuzi na misingi ya NAM iliyoanzishwa mwaka 1961wakati dunia ina mgawanyiko mkubwa kuwahi kutokea, inaweza kupata majawabu hasa kwa kuwajibisha viongozi wa dunia kutimiza ahadi walizotoa kukabili changamoto hizo.

Mathalani amesema katika zama za sasa za ukosefu wa matumaini na utulivu ninaona fursa mpya kwa nchi na NAM kushika nafasi ya kuongoza kwenye utatuzi wa changamoto zilizoko akigusia zaidi maudhui ya mkutano huo Kuimarisha ushirikiano kwa maslahi ya pamoja ya utajiri wa dunia.” 

Guterres amesema kivitendo, maudhui hayo yana maana kuu mbili, ambazo amesema zikizingatiwa zitaondoa dunia hapa iliko na kuisongesha kwenye mwelekeo sahihi.

Mosi: utajiri ulioko duniani unategemea amani.

“Amani inamaanisha kujikita katika kuzuia, kuzungumza, kusuluhisha na kupona mgawanyiko na kutatua mizozo,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa yote haoy yanahitaji taasisi zinazoakisi dunia ya leo si dunia ya miaka 80 iliyopita, “Baraza la Usalama ni mfano mkuu.”

Guterres amesema NAM imekuwa mstari wa mbele kuangazia mfumo wa Baraza la Usalama unaokwamisha na kuzuia majawabu fanisi kutokana na mivutano ya kijiografia na kisiasa.

“Twawezaje kukubali kuwa bara la Afrika halina hata mjumbe mmoja wa kudumu?” amehoji Katibu Mkuu.

Hivyo amesema mkutano wa mwezi Septemba mwaka huu kuhusu Zama Zijazo utakuwa ni fursa adhimu ya kuzingatia marekebisho ya taasisi za usimamizi duniani na kusongesha mawazo ya kujenga upya kuaminiana na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

Pili: Amani inahitaji maendeleo endelevu

Katibu Mkuu ameeleza wajumbe kuwa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs unarudi nyuma badala ya kusonga mbele.

“Watu wana njaa, jamii hazina huduma za afya, maji safi na salama, umeme na huduma bora za kujisafi,” ameeleza Katibu Mkuu akiongeza kuwa familia zinahaha kujikimu bila hata ya kuwa na mifumo ya hifadhi ya jamii huku watoto wakikosa elimu.

“Twawezaje kukubali kuwa bara la Afrika halina hata mjumbe mmoja wa kudumu?” - António Guterres, Katibu Mkuu - UN

Amesema nchi zinazoendelea zinahitaij rasilimali fedha kukabili changamoto hizo  hivyo kinachotakiwa haraka ni msamaha wa madeni na kupatiwa haki ambayo haijatumika ya kibali maalum cha kukopa fedha.

Hii ina maana kurekebisha mfumo wa fedha duniani uliopitwa na wakati, usio wa haki, unaopendelea waasisi hasa nchi tajiri na ambao umethibitisha kuwa hauna uwezo wa kupatia hifadhi ya jamii hasa nchi zinazoendelea zilizotwama kwenye madeni.”

Hivyo Guterres amesema viongozi wa NAM wanaweza kutumia ushawishi wao kukumbusha waliotoa ahadi mwezi Septemba mwaka jana wakati wa mkutano wa viongozi kuhusu SDGs ambako azimio la kisiasa lilipitishwa la kutenga dola bilioni 500 kila mwaka.

Halikadhalika washiriki wa mkutano huo wa SDGs waliunga mkono marekebisho ya taasisi za Brettons ambazo ni Benki ya Dunia na shirika la fedha duniani ili mfumo wake uendane na mazingira ya sasa ya kiuchumi badala ya kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, taasisi hizo zilipoundwa.

Ahadi nyingine ilitolewa kwenye mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28 huko Dubai, Falme za Kiarabu, ya kuanza kutekeleza Mfuko wa Uharibifu na Hasara itokanayo na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

“Nasihi NAM iwajibishe viongozi ili mwaka huu watekeleze ahadi hizi,” amesema Guterres.

GAZA

Tweet URL

Katibu Mkuu ametumia pia hotuba yake ya kurasa tano kurejelea wito wake wa kutaka sitisho la mapigano Gaza kwa minajili ya kufanikisha usaidizi wa kiutu huku akisema suluhu la uwepo wa mataifa mawili kwa pamoja, yaani Palestina na Israel ndio jawabu mujarabu.

“Kukataa kukubali jawabu la mataifa mawili kwa waisraeli na wapalestina na kupinga haki ya utaifa kwa wapalestina, havikubaliki,” amesisitiza Guterres.

Amesema kitendo cha kukataa kitarefusha mzooz ambao tayari umekuw tishio kubwa la amani na usalama duniani; unaongeza mgawanyiko; na kuchipusha makundi yenye misimamo mikali kila mahali.

“Haki ya wapalestina kujenga taifa lao wenyewe laziama ikubaliwe na watu wote,” amesema Guterres.

Kuhusu NAM

Umoja wa Nchi zisizofungamana na Upande Wowote, NAM ulianzishwa mwaka 1961 huko Belgrade, Serbia wakati kukiwa na vita baridi kati ya Marekani na Urusi na hivyo mataifa ambayo hayakutaka kuegemea upande wowote yalianzisha NAM kufuatia mkutano wao wa Bandung nchini Indonesia mwaka 1955 ukileta pamoja viongozi wa nchi za Asia na Afrika.

Waasisi wa NAM walikuwa marais Jawaharlal Nehru wa India, Josip Broz Tito al maaruf Tito wa iliyokuwa Yugoslavia, Sukarno wa Indonesia, Gamal Abdel Nasser wa Misri na Kwame Nkrumah wa Ghana.