Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga Gaza: Kiwango gani kifikie ndio iwe imetosha? Ahoji Rais wa UNGA78 akiwa Uganda

Rais wa Baraza Kuu la UN, Balozi Dennis Francis (wa pili kushoto) akihutubia ufunguzi wa mkutano wa 19 wa Umoja wa Nchi zisizofungamana na upande wowote, NAM huko Kampala nchini Uganda 19 Januari 2024
OPGA
Rais wa Baraza Kuu la UN, Balozi Dennis Francis (wa pili kushoto) akihutubia ufunguzi wa mkutano wa 19 wa Umoja wa Nchi zisizofungamana na upande wowote, NAM huko Kampala nchini Uganda 19 Januari 2024

Janga Gaza: Kiwango gani kifikie ndio iwe imetosha? Ahoji Rais wa UNGA78 akiwa Uganda

Amani na Usalama

Dunia ikikabiliwa na changamoto kubwa na lukuki zinazohitaji ubunifu, maridhiano na majawabu fanisi, kinachofanyika ni kinyume chake kwani mgawanyiko unaongezeka na fursa za kupata majawabu zinazidi kuwa finyu, amesema Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Dennis Francis.

Tweet URL

Balozi Francis amesema hayo huko Kampala, mji mkuu wa Uganda barani Afrika wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 19 wa Umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote, NAM, umoja ambao ulianzishwa mwaka 1961 wakati wa vita baridi kati ya Urusi na Marekani.   

Pengo la ukosefu wa usawa linakuwa mazalia ya chuki, ilhali ukosefu wa kutoaminiana na mivutano ya kijiografia unakwamisha juhudi za kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030,” amesema Balozi Francis mbele ya wajumbe wa NAM ambao ni nchi 120.  

Hoja za uhalali wa UN mizozo ikiendelea  

Mizozo kuanzia Ukraine, Mashariki ya Kati hadi barani Afrika inafichua ukomo wa utendaji kazi wa mfumo wa kimataifa, amesema Rais huyo wa Baraza Kuu la UN akiongeza kuwa, “hii inaibua hoja halali kabisa ya umuhimu na maadili ya Umoja wa Mataifa wenyewe, kwa minajili ya uwezo wake wa kutatua mizozo ya kimataifa na iwpao jamii ya kimataifa inaweza kutimiza ahadi yake ya amani na ustawi kwa wote.”  

Ametanabaisha kuwa ni dhahiri shairi kwamba dunia hivi sasa imegawanyika na hivyo kukwamisha mifumo iliyozoeleka iliyopitishwa na Umoja wa Mataifa ya kutatua mizozo mikubwa.  

Hata hivyo amesema ingawa ni lazima kusaka mikakati na mbinu mpya za kufanikisha utoaji huduma wenye matokeo, jambo moja la kuepusha ni kupoteza uwezo wetu wa kusaka azma ya uwepo wetu na kuchukua hatua kwa pamoja wakati unapolazima kufanya hivyo.” 

Gaza lini tutasema inatosha? 

Ametolea mfano vita huko Gaza akisema ana wasiwasi mkubwa na anachukizwa na kinachoendelea hivyo “natoa wito kwa NAM ishinikize ushawishi wake ili kumaliza mauaji yanayoendelea na ambayo kila mmoja anashuhudia.”   

Balozi Francis amesema “kinachoendelea Gaza kinatuwajibisha tujiulize: kiasi gani kinatosheleza? Na hoja ya kutosheleza inaweza kutumika kwenye mazingira haya?”  

Jamii wamepoteza makazi yao Gaza, wanasaka hifadhi kwingineko.
© UNRWA/Ashraf Amra
Jamii wamepoteza makazi yao Gaza, wanasaka hifadhi kwingineko.

Ametumia mkutano huo kurejelea wito wake wa pande husika kujiepusha na hatua zozote zinazoweza kusambaza mzozo huo huko Mashariki ya Kati na nchi jirani m huku akirejelea tena wito wake wa kutaka sitisho la mapigano kwa misingi ya kibinadamu na mateka wote waachiliwe huru. 

Amesisitiza kuwa historia ya Umoja wa Nchi zisizofungamana na upande wowote ni somo ambalo bado lina mantiki hata leo hii kwa kuzingatia kuwa umoja huo ulianzishwa wakati wa mgawanyiko mkubwa duniani, zama ambazo dunia ilikuwa hatarini kusambaratika.  

Amesema kwa kuzingatia azma ya NAM ya kusongesha na kuchechemua amani, ikiwakilisha zaidi ya nusu ya idadi ya watu duniani, “ina dhima ya kipekee katika kuongoza kuelekea dunia yenye usalama zaidi, ustawi kwa wote ambako utulivu na amani vimeshamiri.”  

Maudhui ya mwaka huu ya mkutano huo wa viongozi wa NAM ulioanza leo na ukitarajiwa kumalizika kesho Januari 20, ni “Kuimarisha ushirikiano kwa maslahi ya pamoja ya utajiri wa dunia.”  

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres tayari amewasili Kampala kushiriki mkutano huo Jumamosi ya tarehe 20 Januari 2024 na kisha Jumapili atashiriki mkutano wa kundi la nchi 77 na China au G77+China.