Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto waliouawa Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, idadi haijawahi kushuhudiwa

Moja ya familia iliyotawanywa kutoka Al Ganoub Oktoba 2023.
OCHA/Manal Massalha
Moja ya familia iliyotawanywa kutoka Al Ganoub Oktoba 2023.

Watoto waliouawa Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, idadi haijawahi kushuhudiwa

Amani na Usalama

Mwaka huu umekuwa mwaka mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa kwa watoto katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, huku ghasia zinazohusiana na migogoro zikifikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa, amesema Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Adele Khodr.  


 

Katika taarifa aliyoitoa leo Desemba 28 huko Amman, Jordan, Bi. Khodr amesema, watoto 83 wameuawa katika muda wa wiki kumi na mbili zilizopita - zaidi ya mara mbili ya idadi ya watoto waliouawa katika mwaka wote wa 2022, huku kukiwa na ongezeko la operesheni za kijeshi na utekelezaji wa sheria. Zaidi ya watoto 576 wamejeruhiwa na wengine wameripotiwa kuzuiliwa. Zaidi ya hayo, Ukingo wa Magharibi umeathiriwa sana na vizuizi vya kutembea na ufikiaji wa maeneo mengine. 

"Wakati ulimwengu ukitazama kwa mshtuko hali katika Ukanda wa Gaza, watoto katika Ukingo wa Magharibi wanapitia jinamizi lao wenyewe. Kuishi kwa hisia za hofu na huzuni, ni jambo la kawaida sana kwa watoto walioathiriwa. Watoto wengi wanaripoti kuwa hofu imekuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku, huku wengi wakiogopa hata kutembea kwenda shuleni au kucheza nje kutokana na tishio la kupigwa risasi na vurugu zingine zinazohusiana na migogoro. UNICEF ina wasiwasi mkubwa kuhusu haki ya watoto katika Ukingo wa Magharibi ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki ya usalama na ulinzi, na haki yao ya asili ya kuishi.” Amesema kwa masikitiko Bi. Khodr 

"Watoto wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, wamekuwa wakikumbwa na ukatili kwa miaka mingi, lakini nguvu ya ukatili huo imeongezeka sana tangu mashambulizi ya kutisha ya Oktoba 7, ghasia zinazohusiana na migogoro zimesababisha vifo vya watoto 124 wa Kipalestina na watoto  6 wa Israel tangu kuanza kwa 2023. 

Kiongozi huyo wa UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini amesisitiza, "Ukiukaji mkubwa dhidi ya watoto, hasa mauaji na kusababisha ulemavu, havikubaliki. UNICEF inazitaka pande zote kutii wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu na kuwalinda watoto dhidi ya ghasia zinazohusiana na migogoro na kulinda haki yao ya msingi zaidi ya kuwa hai. Watoto hawapaswi kamwe kuwa walengwa wa unyanyasaji, bila kujali ni nani au wapi. Kukomesha vurugu za mara kwa mara ndiyo njia bora ya kuhakikisha watoto wanaweza kukua kwa amani na usalama. 

"Mateso ya watoto katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, yasifunikwe nyuma ya mzozo wa sasa - ni sehemu yake." Amesisitiza Adele Khodr.