Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UDADAVUZI: Jinsi UN inavyochagiza 'dhamira ya kimataifa ya kupambana na rushwa'

Mwanamke mchuuzi wa matunda anaandamana kupinga ufisadi nchini Ghana
Unsplash/Nathaniel Tetteh
Mwanamke mchuuzi wa matunda anaandamana kupinga ufisadi nchini Ghana

UDADAVUZI: Jinsi UN inavyochagiza 'dhamira ya kimataifa ya kupambana na rushwa'

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Leo ni siku ya kimataifa ya kupinga rushwa. Nchi kote ulimwenguni zinahitaji kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha kuna “dhamira ya kimataifa ya kupambana na ufisadi” kulingana na mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu UNODC).

Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC, Ghada Waly, ameyasema hayo kabla ya kile anachoeleza kuwa mkutano wa "hatua muhimu" unaofanyika Atlanta nchini Marekani ambao unajadili jinsi ya kuboresha ushirikiano wa kimataifa kuzuia na kukabiliana vyema na rushwa.

Amesema “inakubalika kote kwamba ufisadi huelekeza kwingine rasilimali muhimu, huzuia huduma muhimu, huwezesha uhalifu wa kupangwa, na huongeza ukosefu wa usawa na malalamiko.”

Umoja wa Mataifa unapoadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Rushwa au Ufisadi, haya ndiyo unayohitaji kujua kuhusu kwa nini kupambana na ufisadi ni muhimu na jinsi Umoja wa Mataifa unavyochangia katika juhudi hizo.

Bango lenye ujumbe wa ufisadi nchini Namibia
Bank ya Dunia/Philip Schuler
Bango lenye ujumbe wa ufisadi nchini Namibia

Rushwa ni nini na tatizo ni kubwa kiasi gani?

Ufisadi, kulingana na UNODC, ni "dhana nyeti na inayoendelea, inayoashiria mambo tofauti kwa watu tofauti. Kwa njia moja au nyingine, huathiri sehemu zote duniani”.

Inajumuisha shughuli nyingi ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya mamlaka ya umma, ofisi au mamlaka kwa manufaa binafsi, kupitia hongo, unyang'anyi, biashara ya ushawishi, upendeleo, ulaghai au ubadhirifu.

Kiwango cha kila mwaka cha hongo duniani kote kinakadiriwa kufikia dola trilioni moja. 

Ufisadi unasababisha uchumi wa dunia kupoteza dola trilioni 2.6, ikiwa ni zaidi ya asilimia tano ya Pato la Taifa.

Unaweza kudhoofisha kazi za msingi za umma na ubora wa maisha ya watu unaowanyima haki zao na kupata huduma.

Pia huzifanya nchi kuwa maskini na kudumaza ukuaji wa uchumi, hata wa kanda nzima, na kuruhusu uhalifu uliopangwa, ugaidi na shughuli nyingine haramu kushamiri.

Tangazo nje ya hospitali katika mji mkuu Monrovia,Liberia, ikiwahimiza wagonjwa wasitoe hela kwa madaktari kwa huduma yoyote.
UNICEF/Pirozzi
Tangazo nje ya hospitali katika mji mkuu Monrovia,Liberia, ikiwahimiza wagonjwa wasitoe hela kwa madaktari kwa huduma yoyote.

Je, watu wanaathirika vipi?

Ushahidi kutoka kote duniani unaonyesha kuwa ufisadi unaathiri vibaya watu maskini.

Katika nchi nyingi, waombaji wa leseni za madereva, vibali vya ujenzi na nyaraka zingine za kawaida wamejifunza kutarajia "malipo ya ziada" kutoka kwa watumishi wa umma.

Katika kiwango cha juu, kiasi kikubwa zaidi hulipwa cha hongo kwa mikataba ya umma, haki za uuzaji au kuzuia ukaguzi na utepe.

Rushwa hasa inaathiri wanawake na watoto kwa sababu inaelekeza rasilimali kutoka kwenye miradi mingi inayokusudiwa kumaliza umaskini.

Kiasi kikubwa cha pesa kinapotea kutokana na ufisadi ambazo zingeweza kutumika kuboresha hali ya maisha na kuongeza upatikanaji wa nyumba, afya, elimu, na maji safi.

Inahofiwa kwamba kutokana na kuongezeka kwa rushwa, nchi zitapata ugumu zaidi wa kupiga hatua kuelekea shabaha ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, 17 yaliyokubaliwa na nchi kote duniani ili kukomesha umaskini, kuboresha maisha na matarajio ya kila mtu, kila mahali, huku wakilinda sayari.

Umoja wa Mataifa unasema ufisadi ni hatia, ukosefu wa nidahmu na usaliti wa imani ya umma.
UN News/Daniel Dickinson
Umoja wa Mataifa unasema ufisadi ni hatia, ukosefu wa nidahmu na usaliti wa imani ya umma.

Je, rushwa, SDGs na hasa zaidi mazingira vinahusiana vipi?

Kulinda watu na sayari inawakilisha lengo kuu la SDGs na itakuwa mada inayoangaziwa huko Atlanta.

Rushwa inarudisha nyuma maendeleo katika mambo yote mawili kwani inachochea uharibifu wa mazingira, ikiwa ni pamoja na uchimbaji haramu wa madini, uharibifu na unyonyaji wa wanyamapori, misitu, na viumbe vya baharini, shughuli za uhalifu ambazo zinaweza kuongeza faida kwa vikundi vya uhalifu wa kupangwa.

Ufisadi pia hudhoofisha ulinzi na usalama na hunyima serikali vyanzo muhimu vya mapato, pamoja na kupora mali za jamii za wenyeji.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC Ghada Wally amesema kupambana na rushwa ni "msingi muhimu wa juhudi zetu za kufikia SDGs."

Je, sekta binafsi ina nafasi gani katika kupunguza rushwa?

Wawakilishi kutoka sekta ya kibinafsi watahudhuria mkutano huo na kulingana na Bi Wally wana jukumu muhimu katika kupunguza ufisadi. 

"Uadilifu wa biashara ni nguvu kubwa ya kuhifadhi na kurejesha uaminifu. Inazuia rushwa kupenya katika sekta nzima na kuingia katika utamaduni wa kitaasisi,” ameongeza kuwa unazuia athari za rushwa kwenye ushindani na unapunguza hatari ya kisheria, kifedha na sifa kwa makampuni.

Rushwa inapoenea, uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje hukatishwa tamaa na wafanyabiashara wanasitasita kuwekeza katika masoko ya kitaifa ambapo ushindani si wa haki au uwazi.

Hilo linaumiza uchumi wa kitaifa na kuathiri watu ambao serikali zimechaguliwa kuwahudumia.

Hakuna nchi au eneo ambalo haliwezi kukabiliwa na ufisadi, changamoto ambayo inakwamisha maendeleo.
Picha: UNODC
Hakuna nchi au eneo ambalo haliwezi kukabiliwa na ufisadi, changamoto ambayo inakwamisha maendeleo.

Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Rushwa ni upi?

Washiriki mjini Atlanta wanakutana ili kukagua utekelezaji wa mapambano dhidi ya ufisadi duniani

ahadi zilizoainishwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Rushwa. Ulipitishwa mnamo Oktoba 2003 na kuanza kutekelezwa Desemba 2005, ni chombo cha kwanza na cha kipekee duniani kinachofunga kisheria kupambana na ufisadi.

Kwa ufuasi wa karibu kote ulimwenguni, ulioidhinishwa na mataifa 190 wanachama wa Umoja wa Mataifa, Mkataba unaamuru kuharamisha vitendo vingi vya rushwa, ndani  ya nchi na kimataifa.

Chini ya Mkataba huo, Mataifa :

• Yanawajibika kisheria kuzuia na kuhalalisha rushwa,

• kukuza ushirikiano wa kimataifa,

• kusaka na kurejesha mali zilizoibiwa na

• kuboresha usaidizi wa kiufundi na upashanaji habari katika sekta ya binafsi na za umma.

 

Ghada Waly, mkuu wa UNODC amesema mkataba huo "unaashiria maono yetu ya pamoja ya ulimwengu ambapo uadilifu, uwazi na uwajibikaji vinashinda dhuluma, uchoyo na ukosefu wa usawa."

Je, kumekuwa na mafanikio yoyote katika kurejesha mapato ya rushwa?

Katika kipindi cha miaka 13 iliyopita, inakadiriwa kuwa dola bilioni 4.3 za mapato ya ufisadi zimerejeshwa kwa nchi kote ulimwenguni.

Marekani imeripoti kiasi kikubwa zaidi cha fedha zilizochukuliwa, zilizokamatwa na kurejeshwa makwao. 

Uswisi, Singapore na Liechtenstein pia ni kati ya zile ambazo zimerudisha mali kubwa kwa nchi zao za asili.

Nigeria na Malaysia ziliripoti kupokea kiasi kikubwa zaidi cha mali zinazohusiana na ufisadi kutoka kwa mamlaka za kigeni. 

Kati ya mwaka 2018 na 2023, Malaysia ilipata zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.2 za mali zinazohusiana na ulaghai mkubwa uliohusisha hazina ya serikali. Nigeria iliripoti kupokea dola bilioni 1.2 katika mapato ya rushwa yaliyorejeshwa makwao.

Hata hivyo, Mataifa mengi yanaendelea kukabiliwa na matatizo katika kurejesha mali chini ya mkataba huo na wajumbe wanaokutana Atlanta, watajaribu kukubaliana na jinsi ya kuondoa vikwazo hivyo.

UNCAC yatimiza miaka 20katika kuiunganisha dunia kupambana na ufisadi
© UNODC
UNCAC yatimiza miaka 20katika kuiunganisha dunia kupambana na ufisadi

Kwa hivyo, nini kitatokea huko Atlanta?

Zaidi ya washiriki 2,000 kutoka serikalini, mashirika ya kiserikali, wanazuoni, mashirika ya kiraia, na sekta binafsi watakutana katika kikao cha kumi cha Mkutano unaofanyika kila baada ya miaka miwili wa nchi wanachama (CoSP10) wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Ufisadi.

Mkutano huo unaonekana kuwa hatua muhimu katika kukagua utekelezaji wa ahadi za kimataifa dhidi ya ufisadi kwa sababu unaambatana na maadhimisho ya miaka 20 ya Mkataba huo. 

Hili pia ni tukio la kwanza la aina hiyo kufanyika nchini Marekani.

Mkutano huo unazipa nchi wanachama fursa ya kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya rushwa na pia kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.