Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sera za uelimishaji kupitia maarifa kukabili janga la mihadarati Afghanistan: UNODC

Mwanaume akiwa amejibanza katika kituo cha matibabu ya uraibu wa mihadarati cha Avienna mjini Kabul nchini Afghanistan
UN News / David Mottershead
Mwanaume akiwa amejibanza katika kituo cha matibabu ya uraibu wa mihadarati cha Avienna mjini Kabul nchini Afghanistan

Sera za uelimishaji kupitia maarifa kukabili janga la mihadarati Afghanistan: UNODC

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Karibu na mitaa yenye shughuli nyingi ya mji mkuu wa Afghanistan Kabul, hatari nyingi hujificha kwenye vivuli, lakini hakuna tishio zaidi kuliko janga la matumizi ya dawa za kulevya ambalo inaangamiza nchi nzima.

Ukitembea katika kile kinachotambulika huko Kabul kuwa kituo cha matibabu ya dawa za kiwango cha hali ya juu inavunja moyo. 

Hali katika kituo hicho chenye vitanda 1,000 ni mbaya. Ufadhili wa kimataifa kwa vituo hivi umekauka tangu Taliban walipotwaa mamlaka, na kusababisha wafanyakazi wanaolipwa ujira mdogo kukosa mafunzo sahihi ya kushughulikia wagonjwa.

Chakula ni adimu hapa na hivyo hutoa lishe kidogo na makabati ya maduka ya dawa ni matupu, miili ya wale wanaotumia dawa kuondoa sumu ya mihadarati mwilini mwao inatisha.

Wakazi wa kituo hiki wanatarajiwa kupitia mpango wa matibabu wa siku 45, ambapo wanapewa huduma za matibabu na ushauri nasaha, kulingana na mamlaka, na kisha kufanyiwa tathmini. 

Hii inafanywa ili kuamua kama wanaweza kurudi kwa familia zao au la. Mtu mmoja aliambia UN News kwamba amekuwa akiishi hapa kwa miezi 6. "Watoto wangu hawana mtu wa kuwalisha", alisema.

Mamlaka za Taliban zimewahamasisha watu hao ambao wengi wao hawana lishe na makazi, kuishi hapa kwa hiari baada ya kuletwa na timu za msaada.

Cha kusikitisha ni kwamba, hali nje ya kuta za jela za kituo cha matibabu zinaweza kuwa ngumu vile vile. 

Zaidi ya kukabiliana na umaskini unaoendelea na ukosefu wa usalama unaoendelea, kutotabirika kwa hali ya hewa inayobadilika haraka kunaweza kuwaadhibu wale wanaoishi mitaani ambao wanakabiliwa na baridi kali na majira ya joto kali.

Hali hii inawafanya kutokuwa na matumaini ya kumaliza kwa zahma zao. 

 

Lango la kuingia kwenye kituo cha taarifa cha UNODC Tashkent, Uzbekistan
UN News / Ezzat El-Ferri
Lango la kuingia kwenye kituo cha taarifa cha UNODC Tashkent, Uzbekistan

 

Kituo cha Maarifa

Lakini ukivuka mpaka katika nchi Jirani ya Uzbekistan, kuna mwanga wa matumaini.

Katika mji mkuu wa kihistoria wa nchi hiyo, Tashkent, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya dawa za kulevya na Uhalifu (UNODC) Kanda ya Asia ya Kati imeleta pamoja kundi la wataalamu waliojitolea kuunda kituo chake cha habari cha kutafiti na kuchambua vitisho vya kimataifa vinavyohusiana na dawa za kulevya na uhalifu. 

Mkuu wa Kituo hicho Salome Flores anasema dhamira ya timu yake iko wazi "kutoa ujuzi ambao una malengo, usio na upendeleo, na uliounganishwa vizuri kwa watu wanaofaa kwa wakati unaofaa."

Hii, aliiambia UN News, inaruhusu watoa maamuzi kufanya hivyo tu kwa kuchukua maamuzi sahihi. 

Pia husaidia katika kukuza uelewa wa wigo wa tatizo la madawa za kulevya katika kanda, hasa nchini Afghanistan, ambapo mwaka 2022 uzalishaji wa kasumba uliwakilisha asilimia 9 hadi 14 ya pato la taifa na uzalishaji wa dawa za kulevya unaongezeka kwa kasi.

Kituo hupokea takwimu kutoka kwa vyanzo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na serikali, vyanzo huria, mitandao ya kijamii, utafiti wa kitaaluma, takwimu, na bila shaka kutoka kwa wenzao nchini Afghanistan.

Hata hivyo, zana muhimu zaidi zinazotumiwa na timu katika kazi yake ni mbinu iliyojengwa na UNODC katika miongo mitatu iliyopita ili kutambua mazao kutoka mbali.

Kwa kuchanganya tafiti za msingi, teknolojia ya hali ya juu na picha za satelaiti, shirika hilo linaweza kuunda kile kinachoitwa aina maalum ili kutofautisha zao moja na jingine. 

Hii inaruhusu kubainisha kwa usahihi ambapo kasumba ya poppy inatolewa na kukuzwa.

Aina hizo maalum zilitengenezwa kwa miaka mingi kwa kulinganisha taswira za setilaiti na kile kinachojulikana kama ukweli alisia.

Wataalamu katika shirika hilo la Umoja wa Mataifa waliweza kutengeneza mamia ya aina maalum kwa kutumia mbinu hii ambayo iliwalazimu wapima ardhi kutembelea maeneo maalum kwa GPS ili kuthibitisha uchanganuzi wa awali.

Leo, UNODC ina uwezo wa kutambua mazao mbalimbali kwa usahihi wa hali ya juu sana, ikiwa ni pamoja na ngano, matikiti, alfalfa, pamba, miongoni mwa mengine, na bila shaka kasumba ya poppies. 

Aina hizo maalum zilizotengenezwa zinaweza hata kufahamisha timu ya ubora wa mashamba ya afunyi na mazao yanayotarajiwa.

Alex Nobajas Ganau, afisa habari wa kijiografia katika kituo hicho, ameeleza kuwa picha za satelaiti zinazotumika kwa sasa hazitoi picha tu bali ni pamoja na “taarifa ya ziada ambayo inaweza kutumika kutambua wingi wa klorofili na aina ya zao linalostawi katika kila shamba la kilimo.”

Kazi ya timu ni ya kiufundi na nyeti sana. Kulinda takwimu ni muhimu sana ili kuepuka athari mbaya kwa wakulima, hasa kutokana na hali ya sasa ya kisiasa nchini Afghanistan.

Bwana Ganau amesema takwimu mbichi haishirikiwi kamwe kwenye mtandao au kuunganishwa kwenye seva kwa hivyo haziwezi kudukuliwa. 

Ameongeza kuwa takwimu zilizojumlishwa zinashirikiwa, "kwa hivyo badala ya kuwa na mashamba binafsi, tunayafanya kwa wilaya au mkoa."

 

PHOTO: Credit: 

Afisa wa UNODC Ahmed Esmati akitathimini picha za satelite za Afghanistan katika ofisi yake mjini Tashkent.
UN News / David Mottershead
Afisa wa UNODC Ahmed Esmati akitathimini picha za satelite za Afghanistan katika ofisi yake mjini Tashkent.

Timu A

Katika kiini cha kituo hiki kuna Waafghani wanne walio na uzoefu wa ardhini kwa miongo kadhaa. 

Walikuwa sehemu ya timu ya UNODC nchini Afghanistan ikifanya ziara na tafiti hadi shirika hilo lilipoamua kusitisha shughuli hizo baada ya Taliban kuingia madarakani. 

Wanawasiliana mara kwa mara na wenzao ambao wamesalia nchini humo na wanatoa takwimu muhimu, haswa kuhusu bei ya dawa.

Kama wapima ardhi na wachambuzi, jukumu la wenzao wa Afghanistan limekuwa muhimu katika uundaji wa mazao sahihi ambayo husaidia kufuatilia kilimo cha kasumba.

Bi. Flores ameiambia UN News kuwa “Wafanyikazi wanaofanya kazi katika kituo cha habari cha UNODC wamejitolea sana katika kazi yao. Wenzetu wa Afghanistan wamekuwa wakilifanyia kazi hili kwa muda mrefu sana. Kwa hiyo, tunafaidika kutokana na uzoefu wao na tunafaidika na hamasa yao”.

Kufanya kazi katika uwanja huu ni biashara hatari haswa kwa raia wa Afghanistan.

Saddiqi si jina lake halisi kwani ameomba kulinda utambulisho wake wakati huu familia yake inaendelea kuishi Afghanistan.

Akibainisha hali ya kiufundi ya kazi yake na ulinzi aliopewa kama mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa, amesisitiza kuwa "hali nchini Afghanistan ni tofauti".

Saddiqi anasema anajivunia kazi anayoifanya UNODC, ambayo ina manufaa makubwa kwa nchi yake, na anatumai kuwa "polepole, kila kitu kitakuwa bora inshallah."

Kama Sadiqi, Ahmed Esmati amekuwa akifanya kazi katika ofisi ya UNODC kwa zaidi ya miaka 16 na alianza kama mhakiki. 

Alibahatika kuitoa familia yake kutoka Afghanistan. Esmati anasema wenzake kadhaa walipoteza maisha wakiwa kazini wakati tafiti hizo zikiendelea.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa kazi yao ya kuthibitisha takwimu za satelaiti na kutoa ukweli wa msingi ilikuwa muhimu katika kujenga uwezo wa kufanya shughuli za UNODC za kutambua kutokea mbali, ambazo ni za kipekee kabisa.

“Kabla ya kufanya kazi hii, tulitegemea wakulima na wazee wa vijiji walikuwa wanasema nini kuhusu kilimo cha afyuni. Lakini kwa njia hii ya kufuatilia kutoka mbali na kitambulisho cha afyuni kupitia taswira ya setilaiti, hakuna nafasi ya kuchezea takwimu au  kutoa takwimu bandia,” Esmati anaiambia UN News.

Shamba la kasumba katika jimbo la Kapisa nchini Afghanistan (Kutoka maktaba)
UNODC
Shamba la kasumba katika jimbo la Kapisa nchini Afghanistan (Kutoka maktaba)

Usahihi wa takwimu

Afghanistan ndio msambazaji mkubwa zaidi wa kasumba duniani, ikichukua asilimia 80 ya soko la kimataifa. 

Matumizi ya dawa za kulevya yamekithiri nchini humo. Kwa hivyo, kituo kimejikita zaidi katika ufuatiliaji wa uzalishaji na ukuzaji wa dutu yenye faida kubwa ya mimea ambayo hutumiwa kutengeneza mihadarati aina ya heroini.

Kufuatia mabadiliko ya kisiasa nchini Afghanistan mwezi Agosti 2021, UNODC ilimaliza tafiti zake za msingi, na mageuzi ya kituo cha taarifa yakaanza, kulingana na Ashita Mittal, mwakilishi wa Kanda ya Asia ya Kati.

"Kama Umoja wa Mataifa, tunaamini katika kutoegemea upande wowote kwa takwimu na nafasi yetu, kwa sababu ni jukumu letu kwamba ikiwa tunataka ushahidi wa kufahamisha sera na utendaji, tunahitaji kuwa na takwimu zenye ubora ambazo zinaweza kuthibitishwa."

 

Mtafiti wa UNODC akithibitisha tunda la afyuni katika eneo la Sukhrud Afghanistan
UNODC
Mtafiti wa UNODC akithibitisha tunda la afyuni katika eneo la Sukhrud Afghanistan

Mabadiliko katika soko?

Kufuatia miaka ya kuongezeka kwa uzalishaji na kilimo cha kasumba, ushahidi unaonyesha kwamba 2023 utashuhudia kupungua kwa kasi kutokana na marufuku ambayo imekuwa ikitekelezwa vikali na Taliban.

Hii ni moja ya matokeo muhimu katika ripoti ya dunia ya dawa za kulevy ya 2023. UNODC inataja rekodi ya usambazaji haramu wa dawa na mitandao ya biashara inayozidi kwa kasi lakini inatahadharisha kwamba ingawa faida za uwezekano wa kupungua kwa kilimo haramu cha kasumba nchini Afghanistan mwaka huu zitakuwa za kimataifa, itakuwa kwa gharama ya wakulima wengi ambao hawana njia mbadala ya kuzalisha mapato.

Kwa mantiki hiyo, Bibi Mittal amesisitiza umuhimu wa kituo hicho sio tu kwa Umoja wa Mataifa, kanda, na jumuiya ya kimataifa, bali pia kwa mamlaka zenyewe.

"Tutathibitishaje kwamba marufuku ya Taliban kwa kilimo cha afyuni ni nzuri? Ni kwa njia ya ushahidi wa uhakika tu ndipo tutaweza kuwasilisha ukweli kwa jumuiya ya kimataifa,” Bi. Mittal ameiambia UN News.

Mwakilishi huyo wa kikanda amesisitiza kuwa bado ni mapema mno kujua iwapo matokeo ya marufuku ya kilimo cha kasumba yatadumu, kwani hilo litahitaji uchambuzi wa kituo cha taarifa katika miaka ijayo.

Lakini kwa mamlaka ya Taliban kushikilia kilimo cha kasumba, kuna dalili kwamba soko linabadilika. 

SDawa bandia na mishtuko ya methamphetamine inaongezeka katika eneo lote, ikiongezeka mara nne nchini Tajikistan na kuongezeka mara 11 nchini Kyrgyzstan.

Bi Mittal anasema "Hali nchini Afghanistan ni kwamba kwa sababu ya marufuku ya kilimo cha afyuni, inawezekana kabisa kwamba wafanyabiashara watajaribu kutumia soko hilo kwa kuongeza uzalishaji wa methamphetamines."

Kuna baadhi ya wasiwasi kwamba uzalishaji wa methamphetamines unaweza kuendeshwa na mmea wa ephedra ambao hukua porini katika eneo hili la dunia.

"Lakini huo ni uwezekano mmoja tu," anaongeza mkuu wa kituo cha taarifa, Bi. Flores. "Pia inaweza kutoka kwa kemikali. Inaweza kutoka kwa dawa za baridi au kutoka kwa wingi wa ephedrine. Kwa hivyo, tunajaribu kuelewa jinsi watu au wasafirishaji wanavyozalisha methamphetamines. Na bila shaka tukiweza kulielewa hilo basi tutaweza kuwajulisha wenye mamlaka ili wachukue hatua”.

Mkulima wa zamani wa kasumba akilima nyanya katika jimbo la Nangarhar Afghanistan
UN News / David Mottershead
Mkulima wa zamani wa kasumba akilima nyanya katika jimbo la Nangarhar Afghanistan

Maendeleo mbadala kama suluhisho

Tangu wapiganaji wa Taliban warudi madarakani Agosti 2021, Umoja wa Mataifa umekuwa ukifanya kazi chini ya "Mfumo wa mpito wa ushirikiano" nchini humo, kwa kiasi kikubwa ukiweka kikomo kazi yake kwa mahitaji ya msingi ya kibinadamu huku ukibainisha njia bunifu za kutekeleza shughuli zake za maendeleo kupitia washirika wanaotekeleza, bila kuunga mkono moja kwa moja mamlaka ya Taliban.

UNODC inafanya kazi nchini Afghanistan kupitia washirika wake wa utekelezaji ili kujenga uwezo miongoni mwa wakulima na jamii zilizo hatarini.

Katika nchi hii iliyokumbwa na umaskini, mkulima anaweza kupata takriban senti 30 kwa kilo saba za nyanya na kwa bei ya sasa ya kilo moja ya kasumba inazunguka karibu dola 360, kilimo cha kasumba kinasalia kuwa cha kuvutia na chenye faida kubwa.

Kituo cha taarifa kinatekeleza jukumu muhimu katika kubainisha ni wapi kuna mahitaji ya programu mbadala za maendeleo.

Bi. Flores amekazia umuhimu wa kuwapatia wakulima mapato yanayofaa na kuchukua nafasi ya “zao haramu kwa zao lililo halali.”

"Ikiwa tunajua eneo la kijiografia, tunaweza kulenga rasilimali na juhudi. Tunaweza pia kuelewa sifa za eneo, jiografia, na kupendekeza njia mbadala zinazofaa za kilimo cha afyuni," ameielezea UN News.

Bi. Mittal anaongeza kuwa uwekezaji muhimu zaidi ambao jumuiya ya kimataifa inaweza kufanya ni katika "kupunguza udhaifu katika ncha zote mbili za wigo." Amebainisha kuwa wasafirishaji haramu "siku zote wanatafuta maeneo dhaifu na watu walio hatarini zaidi", na kwa hivyo, mengi zaidi yanahitajika kufanywa ili kuzuia kulima na matumizi ya kasumba.

“Bila uwekezaji wa aina hii, uchumi haramu utaendelea kustawi. Ukisimamisha shughuli moja haramu, inaweza kubadilishwa na nyingine kwa sababu watu wanapaswa kuhakikisha kuwa kuna chakula mezani," anasema.

Makazi yaliyojengwa kwa mstari katika ukingo wa mji wa Kabul
UN News / David Mottershead
Makazi yaliyojengwa kwa mstari katika ukingo wa mji wa Kabul

Wahalifu wanaohamasishwa na faida

Kwa miongo kadhaa, kasumba imesafiri kutoka Afghanistan kupitia Asia ya Kati na njia ya kaskazini hadi katika masoko mengine, ikiwa ni pamoja na Ulaya, hata kufikia Kusini Mashariki mwa Asia, Mashariki ya Kati na Afrika.

Ufuatiliaji wa biashara ya dawa za kulevya katika eneo hili bado ni muhimu sana, kwani wafanyabiashara hutafuta njia mpya za kusafirisha bidhaa zao na kuongezeka kwa dawa bandia kunaleta shida na athari zinazowezekana kimataifa.

Bi. Mittal amesisitiza kuwa faida ndiyo huendesha shughuli haramu, na faida kubwa zaidi hupatikana nje ya nchi zinazozalisha kama vile Afghanistan.

Hata baada ya kupiga marufuku, bei ya kilo moja ya kasumba katika majira ya chipukizi ya 2023 ni karibu dola 368, wakati kilo ya heroini inaweza kuzidi dola 48,000 katika mitaa ya London.

"Kwa hivyo, ingawa tunaweza kulaumu na kuweka jukumu kwa Afghanistan, ambayo haizalishi kemikali za awali, tunahitaji kuwa na jukumu la pamoja katika kushughulikia suala hili," anasema.

Kukabiliana na vitisho vinavyoendelea

Bi. Flores amesema timu yake inalenga kufuatilia na kuchambua vitisho vyote vya kimataifa katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na biashara haramu ya binadamu ambayo ni hatari inayoongezeka na mtiririko wa watu wanaohama kutoka Afghanistan, pamoja na utoroshaji wa silaha, uchimbaji haramu, usafirishaji wa wanyamapori na dawa bandia kama mwelekeo unaokua katika eneo hili.

Kulingana na mkuu wa kituo cha taarifa "Vitisho vya kimataifa vinabadilika, na uhalifu uliopangwa hubadilika. Mamlaka zinaposhughulikia masuala haya, masoko haramu yanaweza kubadilika.”

Matarajio ya suluhu ya kidiplomasia kati ya jumuiya ya kimataifa na mamlaka ya taliban nchini Afghanistan yanaendelea kuwa ya kusikitisha, huku masuala ya haki za binadamu yakibaki kuwa kigezo kikuu cha kuzingatia.

Kwa kukosekana kwa maendeleo endelevu ya kweli nchini Afghanistan, shughuli haramu zinaweza kuendelea kama janga la tauani nchini humo kuambukiza ulimwengu, na kufanya kazi ya kituo cha taarifa kuwa muhimu katika kushughulikia changamoto hizi.