Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UN yahaha kuisaidia Zambia dhidi ya kipundupindu 

Mtoto kutoka Mtedera Zambia akipweza chanjo ya kipindupindu
Picha ya Gavi Alliance/Duncan Graham-Rowe
Mtoto kutoka Mtedera Zambia akipweza chanjo ya kipindupindu

Mashirika ya UN yahaha kuisaidia Zambia dhidi ya kipundupindu 

Afya

Baada ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Zambia, Kikosi Kazi cha Umoja wa Mataifa kikiongozwa na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo Beatrice Mutali wanaisaidia serikali ya Zambia kukabiliana na ugonjwa huo ambao umetokea huku kukiwa na mafuriko makali yaliyowafurusha zaidi ya watu 170,000 katika wilaya 22 za nchi hiyo barani Afrika.  

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric jioni ya Ijumaa hii jijini New York Marekani amewaeleza waandishi wa habari kuwa mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia watoto UNICEF na la afya ulimwenguni, WHO yana yanaendelea kutoa usaidizi wa karibu kwa waathirika.  

“Tunakabiliana na mlipuko wa kipindupindu katika wilaya tatu, ambapo wagonjwa 90 na vifo vitatu vimerekodiwa.” Ameeleza Dujarric.  

Mafuriko yaliyotokea yalitatiza huduma za msingi, kama shule na hospitali  na hali hiyo pia imeathiri kilimo na mifugo na kuharibu miundombinu muhimu, kama barabara, madaraja, shule, zahanati na nyumba. 

Dujarric amesema, “timu yetu inatoa usaidizi wa kiufundi kwa mamlaka huku ikikusanya ufadhili ili kuziba pengo la dola milioni 32 kwa ajili ya mawasiliano hatarishi, maji na kujisafi, chakula na bidhaa nyinginezo, miongoni mwa mahitaji mengine.” 

Tangu Desemba, UNICEF imetoa tani 4.5 za klorini ya punjepunje na chupa 20,000 za klorini ya maji kwa ajili ya matibabu ya maji ya nyumbani, na mikebe 250 ya dawa za kuua vijidudu vinavyosababisha maradhi , na vifaa vingine muhimu ili kuweka maji salama. 

Kwa upande wake, WHO inafanya kazi na mamlaka ya Zambia ili kuimarisha uwezo wa kutathmini pamoja na ufuatiliaji, ufuatiliaji wa watu walioambukizwa, na maandalizi ya maabara kwa chanjo dhidi ya kipindupindu. 

Nchi nyingine ya bara la Afrika ambayo hivi karibuni imetangazwa na WHO kuwa iko katika makabiliano na mlipuko mpya wa kipundupindu ni Malawi ambayo hadi kufikia wiki hii watu 36, 943  wameugua kipindupindu katika wilaya zote 29 za Malawi tangu mwezi Machi mwaka jana 2022, huku vifo 1210 vikuhusishwa na kipindupindu ambapo WHO inasema mlipuko wa sasa umesababisha vifo zaidi katika historia ya ugonjwa huo nchini humo.