Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dozi 600 000 za chanjo zimewasili Lebanon kudhibiti mlipuko wa kipindupindu:WHO 

Chini ya hatua za dharura za WHO shehena ya kwanza ya vifaa tiba kupambana na kipindupindu yawasili Lebanon
WHO
Chini ya hatua za dharura za WHO shehena ya kwanza ya vifaa tiba kupambana na kipindupindu yawasili Lebanon

Dozi 600 000 za chanjo zimewasili Lebanon kudhibiti mlipuko wa kipindupindu:WHO 

Afya

Wakati ugonjwa wa kipindupindu ukiendelea kusambaa kwa kasi nchini Lebanon, hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, limewezesha serikali ya Lebonan kupata dozi 600,000 za chanjo dhidi ya ugonjwa wa Kipindupindu kutoka Kundi la kimataifa la uratibu wa chanjo za kipindupindu, ICG, tayari kwa kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo itakayoanza Jumamosi hii ya tarehe 12 mwezi Novemba.  

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo huko Beirut Lebanon imesema kampeni ya chanjo italenga wakimbizi na jamii zinazowahifadhi wenye umri kuanzia mwaka mmoja na kuendelea, ikilenga asilimia 70 ya wananchi na kila wiki watu 200,000 kupatiwa chanjo katika kipindi cha wiki tatu.    

Mwakilishi wa WHO nchini Lebanon Dkt. Dr Abdinasir Abubakar amesema “Chanjo hizi zitakuwa nyenzo muhimu kuongeza nguvu katika hatua zatu za kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu ambao unasambaa kwa kasi nchini humu.Kuwasili kwa chanjo hizi nchini ni hatua ya wakati na tunashukuru jitihada za pamoja kwa kushirikiana na wizara ya afya ya Lebanon mashirika ya umoja wa Mataifa na wadau wetu wengine nchini humu.” 

WHO imebeba jukumu la gharama zote 

WHO inagharamia gharama yote ya dozi hizo 600,000 kutoka kwa ICG, ambayo inasimamia hifadhi ya kimataifa ya chanjo ya kipindupindu inayotolewa kwa njia ya matone mdomoni, na inatoa mwongozo wa kiufundi kuhusu uteuzi wa maeneo lengwa, uundaji wa mipango midogo midogo na mafunzo ya washirika wa utekelezaji wanaohusika na kutolewa kwa chanjo hiyo.  

WHO na washirika wake pia wanaendelea kusaidia chanjo ya Shanchol dhidi ya kipindupindu iliyotolewa na Sanofi kwa matumizi ya wafungwa na wahudumu wa afya. 

WHO yaonya kuhusu kuongezeka kwa visa vya kipindupindu Lebanon
WHO
WHO yaonya kuhusu kuongezeka kwa visa vya kipindupindu Lebanon

"Chanjo za kipindupindu ni zana muhimu za kulinda watu na kupunguza kuenea kwa mlipuko huo, lakini sio zana pekee tuliyo nayo kupambana na kipindupindu. Tunaweza kuzuia kipindupindu kwa ufanisi kwa kuboresha upatikanaji wa maji salama, usafi wa mazingira na kanuni za usafi. Pia tuhakikishe watu wanapata huduma hizi,” ameongeza Dk Abubakar. 

Huku mpango wa kitaifa wa chanjo ya kipindupindu ukitekelezwa kwa awamu, kuanzia kundi hili, WHO pia itakuwa ikisaidia wizara ya afya ya umma kukamilisha ombi la pili la ICG la nyongeza ya dozi milioni mbili za chanjo ya kipindupindu inayohitajika kwa awamu ya 2 ya kampeni. 

Taarifa za mlipuko wa sasa wa kipindupindu 

Mlipuko wa sasa wa kipindupindu nchini Lebanon ni wa kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 30, ukiakisi kuzorota kwa hali ya uchumi na upatikanaji duni wa maji safi na huduma bora za usafi wa mazingira nchini kote. 

Kufikia tarehe 7 Novemba 2022, visa 2722 vinavyoshukiwa kuwa kipindupindu vimeripotiwa na kati ya hivyo 448 vimethibitishwa kimaabara na vifo 18 vinavyohusiana , CFR 1% viliripotiwa kote nchini.  

Kati ya kesi hizi, asilimia 25% ni Watoto wa umri wa chini ya miaka mitano.