Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu lakutana kumuenzi Hayati Magufuli 

Mwendazake John Pombe Magufuli, Rais wa Tanzania
Muhiddin Michuzi
Mwendazake John Pombe Magufuli, Rais wa Tanzania

Baraza Kuu lakutana kumuenzi Hayati Magufuli 

Masuala ya UM

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao rasmi cha kumuenzi na kumkumbuka Rais wa 5 wa Tanzania Dkt. John Magufuli aliyefariki dunia tarehe 17 mwezi uliopita.  

Katika hotuba yake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amemwelezea hayati Magufuli kuwa alijitahidi kupanua huduma za kijamii na kukabiliana na rushwa akisema, “hayati Rais Magufuli alichagiza maendeleo ya miundombinu na viwanda, vitu muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi.” 

Guterres amesema chini ya hayati Magufuli Tanzania ilifikia azma  ya kuwa nchi ya uchumi wa miaka minne kabla ya lengo lililokuwa limewekwa la mwaka 2025. 

Katibu Mkuu pia amegusia elimu akisema kuwa Hayati Magufuli alisaidia kuimarisha mfumo wa elimu na kuongeza viwango vya uandikishaji wa wanafunzi wapya kujiunga na shule za sekondari. 

Halikadhalika serikali yake ya awamu ya tano, iliimarisha usambazaji umeme vijijini ikiwa na lengo la kupanua uwezo wa wananchi kupata umeme nchi nzima. 

Ametuma kwa mara nyingine salamu za rambirambi kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, kwa wananchi na serikali ya Tanzania Pamoja na familia ya hayati Dkt. Magufuli. 

Katibu Mkuu amesema Umoja wa Mataifa  unatambua historia ya muda mrefu ya taifa hilo la Afrika Mashariki katika kusongesha ushirikiano wa kimataifa na amepongeza jinsi inavyojitoa katika ushirikiano huo wa kimataifa na kikanda. 

Katibu Mkuu ametamatisha hotuba yake akisema, “atumia fursa hii kusisitiza na kukazia azma ya Umoja wa Mataifa ya kuendelea kushiriana kwa karibu na Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan, rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania. Tuko Pamoja na wananchi wa Tanzania katika kusongesha maendeleo endelevu na kuunga mkono jitihada zake za ustawi wa wananchi wote.” 

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania apaza sauti

Katika kikao hicho, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Profesa Kennedy Gastorn alipata fursa ya kuzungumza ambapo amemwelezea Hayati Dkt. Magufuli kuwa “alibaini lengo la kizazi chake na katu hakusaliti. Upendo wake kwa Mungu na Taifa lake, imani yake kwa watu wake, vilimfanya awe mtu wa kipekee mwenye heshima na Rais wa wanyonge.”

Profesa Gastorn ameenda mbali kusema kuwa Rais huyo wa 5 wa Tanzania alikuwa mtu aliyevutia watu wengi ulimwenguni kote na alizungumza ukweli kupitia ukweli wa uwajibishaji na wakati huo huo kwa unyenyekevu.
“Miongoni mwa watendaji wenzake alikuwa  muwazi na kila wakati alikuwa mchapakazi, mzalendo wa dhati na kiongozi ambaye hakupenda ubinafsi,” amesema Balozi Gastorn.

Balozi Profesa Kennedy Gastorn, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia wakati wa kikao rasmi cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa cha kumuenzi na kumkumbuka hayati Rais John Magufuli.
UN Webcast Video
Balozi Profesa Kennedy Gastorn, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia wakati wa kikao rasmi cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa cha kumuenzi na kumkumbuka hayati Rais John Magufuli.

Halikadhalika amezungumzia jinsi ambavyo Hayati Dokta Magufuli alikuwa kiongozi mwenye maono na mwanamajumui aliyeamini kuwa kila mtanzania na kila mwafrika na kila binadamu anastahili kitu bora zaidi.
Rais wa 6 wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Mwakilishi huyo wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa amesema awamu ya 5 ikitamatika tarehe 17 mwezi Machi mwaka huu wa 2021, ukurasa mpya ulifunguliwa wa awamu ya 6 tarehe 19 Machi 2021 kwa kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama.

“Tunajivunia kama taifa na tunashukuru kwamba katika hatamu za uongozi, kwa mara ya kwanza tuna Mwanamke ambaye ni Mkuu, ikiwa ni historia. Rais Samia ni mzalendo na mwanasiasa anayezingatia misingi, ana maono na muumini na muungaji mkono wa ushirikiano wa kimataifa,” amesema Profesa Gastorn.

Chini ya uongozi wake, Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Umoja wa Mataifa na misingi yake ambayo ni amani na usalama duniani, haki za binadamu, maendeleo na ustawi wa binadamu, “Rais Samia tayari amechukua hatua za kiuongozi kwa unyenyekevu na ubunifu, kasi na upendo katika kufanikisha ajenda 2030 ya maendeleo endelevu.”