Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania yaomboleza kwa siku 14, ni kufuatia kifo cha Rais John Magufuli

Tanzania yaomboleza kwa siku 14, ni kufuatia kifo cha Rais John Magufuli

Pakua

Tanzania imeanza maombolezo ya siku 14 huku bendera zikipepea nusu mlingoni kufuatia  kifo cha Rais wa nchi hiyo  Dkt. John Pombe Magufuli  kilichotokea jana saa 12 jioni saa za Afrika Mashariki kutokana na matatizo ya moyo. Mauti yakimkuta Rais Magufuli alikuwa na umri wa miaka 61. Flora Nducha na maelezo zaidi.
 
Mwendazake John Magufuli ameaga dunia katika hospitali ya Mzena iliyoko jijini Dar es salaam ambako alilazwa akisumbuliwa na matatizo ya moyo. 

Kifo chake kilitangazwa usiku wa jana kwa saa za Afrika Mashariki na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan.

“Ndugu wananchi kwa masikitiko makubwa, nawajulisha kuwa leo tarehe 17 Machi mwaka huu wa 2021 majira ya saa 12 jioni tumempoteza kiongozi wetu shupavu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amefariki kwa maradhi ya moyo katika hospitali ya Mzena jijini Dar es salaam alikokuwa akipatiwa matibabu. Mheshimiwa Rasi Magufuli alilazwa tarehe 6 machi mwaka huu katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete kwa tatizo la tatizo la moyo la mfumo wa umeme ambalo alikuwa nalo kwa zaidi ya miaka 10. Aliruhusiwa tarehe 7 machi mwaka huu na kuendelea na majukumu yake. Tarehe 14 machi mwaka huu alijisikia vibaya na kukimbizwa hospitali ya Mzena ambako aliendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi wa taasisi ya moyo ya  ya Jakaya Kikwete hadi umauti ulipomkuta. Mipango ya mazishi inapangwa na mtajulishwa. Nchi yetu itakuwa kwenye maombolezo kwa siku 14 na bendera zitapepea nusu mlingoti.”

Rais Magufuli aliyejulikana kwa jina la utani kama "tingatinga" kutokana na uchapaji kazi wake, wakati wa uhai wake hakusita kuelezea yaliyokuwa moyoni mwake kwa ajili ya maslahi ya umma wa watanzania.

Katika moja ya ziara zake akizungumza na wananchi  Magufuli alisema, “na nataka muamini watanzania mna rais wa kwelikweli, jiwe kwelikweli. Sitishwi wala sitishiki, mimi jukumu langu kwa ajili ya watanzania, ni kuhakikisha ninawavusha watanzania, kutoka mahala pa shida na waende mahali pa raha. Ninajua hiyo ndio itakuwa sadaka yangu ya watanzania ili kusudi hata nikienda huko mbinguni siku moja Mungu atakaponihitaji,  akanichague wewe ulikuwa  kiongozi mzuri unaweza kuwaongoza hata malaika polepole. Inawezekana kuelewa ni vigumu na inawezekana itachukua muda,  lakini baadaye siku moja watakumbuka, na mimi hilo nina uhakika. Na  mara nyingi watanzania wana tabia ya kukumbuka ukishakufa, wanakwambia, ‘Pengo lake halitazibika,”

Hayati Magufuli alizaliwa tarehe 29 Oktoba mwaka 1959 wilaya ya Chato wakati huo ikiwa mkoani Kagera sasa mkoani Geita, Kaskazinna nataka i Magharibi mwa Tanzania, alipata elimu hadi ya shada ya uzamivu (PHD) katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam mwaka 2009 katika masuala ya kemia . 

Baada ya kuwa mwalimu kwa muda mfupi kwenye shule ya sekondari ya Sengerema alichaguliwa kuwa mbunge kupitia chama tawala Chama Cha Mapinduzi, (CCM) mwaka 1995 na kuteuliwa kuwa  Naibu Waziri Ujenzi na Miundombinu mwaka huo huo na nyadhifa zingine alizowahi kushika kabla ya kuwa Rais ni pamoja na Waziri wa Ardhi na Makazi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi na  mwaka 2010 hadi 2015 aliteuliwa kwa mara ya pili kuiongoza Wizara ya Ujenzi , Usafirishaji na Mawasiliano safari hii kama waziri kamili na ndipo umaarufu wake uliposhika kasi.  
 
Mwaka 2015 aligombea kiti cha urais kwa mara ya kwanza na kumshinda mpinzani wake Edward Lowassa kutoka chama cha upinzani cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA na kuiongoza Tanzania kwa miaka 5. 

Mwaka jana 2020 aligombea tena urais na alichaguliwa kuliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kwa miaka mingine 5.
Akiwa madarakani wananchi walimpenda kwa kupambana na ufisadi, kutetea haki za wanyonge, kukusanya kodi, kufuta karo kuanzia shule za msingi hadi kidato na nne, kuijenga Tanzania kwa miundombinu ya kisasa na mambo mengine mengi. 
 
Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania Rais akifariki dunia Makamu wa Rais ndiye anayeshika hatamu kuiongoza nchi kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa uongozi. 

Kwa mantiki hiyo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ndiye atakayekuwa Rais kwa miaka minne ijayo. Hii itamfanya kuwa mwanamke wa kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kushika wadhifa huo wa Urais.

Hayati John Pombe Magufuli alikuwa ni Rais wa Tana kuiongoza Tanzania tangu ipate uhuru mwaka 1961, na ameaacha mjane Janet Magufuli na watoto.  Mola ailaze roho yake mahala pema peponi , Amina.!!
 

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
5'34"
Photo Credit
Ikulu Tanzania