Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya wahudumu wa afya 10,000 barani Afrika wameambukizwa COVID-19: WHO

Muhudumu wa afya mjini Brazzaville nchini Jamhuri ya Congo akivaa vifaa vya kujinginga dhidi ya Corona
WHO
Muhudumu wa afya mjini Brazzaville nchini Jamhuri ya Congo akivaa vifaa vya kujinginga dhidi ya Corona

Zaidi ya wahudumu wa afya 10,000 barani Afrika wameambukizwa COVID-19: WHO

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO leo limeonya kuhusu tishio la janga la ugonjwa wa corona au COVID-19 kwa wahudumu wa afya barani Afrika.

Shirika hilo limesema wahudumu wa afya zaidi ya 10,000 katika nchi 40 ambao wamekuwa wakipambana na COVID-19 nao wameambukizwa virusi hivyo ikiwa ni ishara ya changamoto wanazokabiliana nazo wahudumu wa afya walio msitari wa mbele kupambana na janga hilo.

Taarifa hii imekuwa wakati ambapo idadi ya wagonjwa barani Afrika inaonekana kushika kasi. Hadi kufikia sasa kumeripotiwa wagonjwa zaidi ya 750,000 wa COVID-19 na vifo zaidi ya 15,000.

WHO inasema katika baadhi ya nchi zinakaribia kufikia idadi mbaya ya maambukizi ambayo itaongeza shinikizo katika mifumo ya afya ambayo mingi ni duni. Mathalani Afrika Kusini kwa sasa ni miongoni mwa nchi zilizoathirika vibaya sana duniani.

Shinikizo kwa mifumo ya afya

Akizungumzia hali hiyo mkurugenzi wa WHO kanda ya afrika Dkt. Matshidiso Moeti, amesema “Ongezeko la wagonjwa wa COVID-19 tunalolishuhudia Afrika  linaongeza shinikizo kubwa katika huduma za afya barani humo. Na hii inaathi mbaya bayana kwa watu wanaofanyakazi katika mifumo hiyo na hakuna mifano tena zaidi ya kwamba wahudumu hawa wanaopata maambukizi idadi yao inaongezeka.”

Hadi sasa takribani asilimia 10 ya wagonjwa wote duniani ni wahudumu wa afya ingawa kuna tofauti kubwa baina ya nchi na nchi.

Nchini Ethiopia wahudumu wa afya wakijihusisha na kutibu wagonjwa wa COVID-19
WHO
Nchini Ethiopia wahudumu wa afya wakijihusisha na kutibu wagonjwa wa COVID-19

Barani Afrika amesema taarifa kuhusu maambukizi miongoni mwa wahudumu wa afya bado ni ndogo lakini takwimu za awali zimebaini kwamba ni zaidi ya asilimia 5 ya wagonjwa katika nchi 14 za afrika zilizo Kusini mwa Jsangwa la Sahara pekee, na nne kati ya nchi hizo wahudumu wa afya ni zaidi ya asilimia 10 ya wagonjwa wote wa COVID-19.

Changamoto zinazowakabili wahudumu wa afya

Kwa mujibu wa WHO upungufu wa vifaa vya kujilinda au hatua duni za kuzuia na kuthibiti ugonjwa huo zinaongeza hatari ya maambukizi kwa wahudumu wa afya. Ongezeko la kimataifa la mahitaji ya vifaa hivyo Pamoja na vikwazo vya kimataifa vya usafiri vimechangia upungufu wa upatikanaji wa vifaa hivyo muhimu.

Pia imeelezwa kwamba wahudumu wa afya wanaweza kuambukizwa na wagonjwa ambao hawana dalili na wako katika vituo vya afya kwa ajili ya kupatiwa huduma zingine.

Pia maambukizi yanasambaa endapo wahudumu wa afya wanapelekwa kwenye vitengo vya COVID-19 bila kupewa muongozo unaostahili au sababu ya kazi kuwa nyingi na kuwasababishia uchovu unaopelekea washindwe kuzingatia masharti wakati wakitoa huduma.

Pia imebainika kwamba katika nchi nyingi za Afrika hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi katika vituo vya afya bado hazitekelezwi kikamilifu.

“Ambukizo moja tu kwa wahudumu wa afya ujue hayo ni maambukizi mengi. Wauguzi na wahudumu wengine wa afya ni mama zetu, kaka na dada zetu. Wanasaidia kuokoa Maisha yaliyo hatarini dhidi ya COVID-19. Lazima tuhakikishe kwamba wana vifaa , ujuzi na taarifa wanazohitaji kwa ajili ya kujilinda, kulinda wagonjwa na kuhakikisha wafanyakazi wenzao wako salama.”

Inachokifanya WHO barani humo

WHO imekuwa ikishirikiana kwa karibu na wizara za afya barani humo ili kupunguza maambukizi miongoni mwa wahudumu wa afya tangu kuzuka kwa mlipuko huo.

Shirika hili limetoa mafunzo kwa wahudumu wa afya zaidi ya 50,000 barani Afrika ya kuzuia na kudhibiti maambukizi, huku likiwa na mipango ya kutoa mafunzo kwa wengine 200,000 zaidi na kutoa mwongozo kuhusu miakati bora ya huduma na matibabu.

Pia WHO inasaidia kuziba pengp a vifaa vya ujilinda na kwa sasa vifaa milioni 41 viko tayari kusafirishwa kutoka China kwenda kukidhi mahitaji ya nchi 47 za Afrika. Na awamu ya kwanza kwenda kwa nchi 23 za Afrika itaondoka mwishoni mwa juma.