Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani Sudan Kusini (UNMIS) limekaribisha amri ya utendaji iliotangazwa na Raisi Omar al-Bashir wa Sudan kusimamisha, haraka, zile sheria za ukaguzi na uchunguzi wa magazeti katika nchi. UNMIS iliripoti pindi uamuzi huo utatekelezwa utasaidia kuendeleza na kuimarisha mapendekezo ya Mapatano ya Amani ya Jumla (CPA) baina ya eneo la kaskazini na kusini, na kuandaa mazingira bora ya kutayarisha uchaguzi wa vyama vyingi uliopangwa kufanyika Aprili 2010.

KM ameridhika na mahojiano ya awali kwenye kikao cha mwaka cha BK

KM Ban Ki-moon alifanya mahojianio na waandishi habari kwenye Makao Makuu ya UM, leo asubuhi, na aliwaambia wanahabari kwamba maendeleo makubwa yalipatikana tangu kikao cha 64 cha Baraza Kuu (BK) kuanza rasmi wiki iliopita, ambapo viongozi wa dunia walifikia maafikiano kadha kwenye juhudi zao za kutafuta suluhu ya kuridhisha ya masuala makuu yanayotatanisha ulimwengu wetu, ikijumlisha udhibiti wa madhara yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa, ukomeshaji wa silaha za maangamizi za kinyuklia na kwenye mizozo ya kifedha katika soko la kimataifa.

Ukame katika Uganda unaitia wasiwasi WFP

Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti rasmi hii leo kuingiwa wasiwasi kuhusu mfululizo wa mvua haba katika Uganda kwenye majira ya mvua, hali iliosababisha watu milioni mbili kukosa uwezo wa kupata chakula na kuomba wasaidiwe chakula na mashirika ya kimataifa kunusuru maisha.