Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Hapa na pale

Tarehe 31 Agosti ni siku ya mwisho ya uraisi wa duru wa Baraza la Usalama kwa Uingereza. Kuanzia tarehe mosi Septemba uraisi wa Baraza la Usalama utakabidhiwa Marekani. Ijumatano Balozi Susan Rice wa Marekani anatarajiwa kutangaza mradi wa kazi na ajenda ya Baraza la Usalama kwa mwezi Septemba.

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon wiki ijayo atafanya ziara ya siku mbili katika Svalbard, Norway, ili kujionea binafsi athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika eneo la Kaskazini ya dunia la Akitiki (Arctic). Kwanza KM atakwenda eneo la Ny-Alesund, liliopo Kaskazini kwenye fungu la visiwa vya Svalbard, ambapo atazuru steshini ya uchunguzi juu ya mazingira ya ncha ya dunia, kabla hajaelekea Kaskazini juu zaidi ambapo atapatiwa taarifa mpya za kisayansi kuhusu namna majabali ya barafu yanavyodhibiti na kurekibisha shughuli za Bahari ya Akitiki na kuathiri mabadiliko ya hali ya hewa ya ulimwengu.

Taarifa juu ya hali ya maambukizi ya A/H1N1 katika dunia

Shirika la Afya Duniani (WHO) kwenye taarifa ya wiki kuhusu hali ya maambukizo ya homa ya mafua ya A/H1N1 llimeeleza ya kwamba katika nchi za kizio cha kusini ya dunia, ikijumlisha Chile, Argentina, New Zealand na Australia maambukizo ya maradhi yameshapita kilele na hivi sasa yameselelea kwenye kigezo wastani, wakati mataifa ya Afrika Kusini na Bolivia yanaendelea kukabiliwa na ongezeko la homa ya mafua.

Siku 100 zimesalia kabla ya Mkutano wa COP-15 kudhibiti taathira za mabadiliko ya hali ya hewa

UM umetoa mwito maalumu wenye kuwataka mamilioni ya umma wa kimataifa kutia sahihi zao, kwenye mtandao, ili kuidhinisha lile ombi la kuzihimiza serikali wanachama Kukamilisha Makubaliano juu ya waraka wa Mkutano wa COP-15, yaani ule Mkutano Mkuu utakaofanyika mwezi Disemba katika mji wa Copenhagen, Denmark kuzingatia mkataba mpya wa udhibiti bora wa mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni.