Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Hapa na Pale

Alkhamisi KM alikuwa na mkutano makhsusi na Mjumbe wa Kudumu wa Myanmar katika UM. Kwenye mkutano wao huo KM alimuarifu Mwakilishi wa Myanmar ya kuwa ni matarajio yake, na pia ya jumuiya ya kimataifa, halkadhalika, kwamba Serikali itazingatia, kwa uangalifu mkubwa zaidi, taathira za hukumu watakayotoa kwenye kesi inayomhusu kiongozi wa upinzani Aung San Suu Kyi, na anaamini Serikali itatekeleza jukumu lake adhimu la kumtoa kizuizini mapema iwezekanavyo.

Afrika yaongoza mataifa katika kunyonyesha watoto wachanga: WHO

Shirika la Afya Duniani (WHO) lemeripoti kwamba bara la Afrika ni miongoni mwa maeneo machache ulimwenguni yenye kuongoza kwenye huduma za kunyonyesha watoto wachanga, licha ya kuwa eneo hili linakabiliwa na matatizo aina kwa aina ya kiafya na kiuchumi. WHO imeeleza pindi kiwango cha kunyonyesha watoto katika Afrika kitaongezeka kwa asilimia 90, inakadiriwa watoto wachanga milioni 1.3 wataokoka vifo kila mwaka.

Watu 50,000 wameng'olewa makazi na fujo zilizoipamba JKK mashariki

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) kwenye taarifa iliotangaza Geneva asubuhi ya leo katika mkutano na waandishi habari, imeripoti raia 56,000 wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) walilazimika kung\'olewa makazi katika jimbo la mashariki kufuatia fujo zilizofumka tena kwenye eneo hilo mnamo tarehe 12 Julai.

Hapa na Pale

Baraza la Usalama Alkhamisi limepitisha azimio la kuongeza muda wa operesheni mbili za UM juu ya ulinzi amani katika Cote d\'Ivoire na Darfur, Sudan. Kuhusu Cote d\'Ivoire Baraza lilipiga kura kwa kauli moja kuongeza kwa miezi sita muda wa operesheni za Shirika la UM Kulinda Amani katika Cote d\'Ivoire (UNOCI). Wakati huo huo Baraza limeidhinisha kibali cha kibali cha kuendeleza operesheni za Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) kwa miezi kumi na mbili ijayo, hadi Julai 2010. Kadhalika Baraza la Usalama lilimtaka KM atayarishe mradi wa utendaji wenye vigezo vya kutathminia na kufuatilia maendeleo juu ya namna maazimio ya Baraza yanatekelezwa katika Darfur.

FAO itafadhiliwa dola milioni 2.5 na Saudi Arabia kutayarisha mkutano wa kukomesha njaa

UM umetangaza ya kuwa Saudi Arabia itafadhilia msaada wa dola milioni 2.5 kwa Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) ili kuiwezesha taasisi hii kufanyisha Mkutano Mkuu juu ya Udhibiti Bora wa Akiba ya Chakula Duniani, utakaojumuisha wajumbe kadha wa kadha wa kutoka Mataifa Wanachama kwenye Makao Makuu ya FAO mjini Roma, Utaliana kuanzia tarehe 16 hadi 18 Novemba mwaka huu.