Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Uamuzi wa Tanzania kuongeza muda wa makazi kwa Waburundi wapongezwa na UNHCR

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limekaribisha uamuzi wa Serikali ya Tanzania wa kuruhusu muda zaidi wa kukaa nchini, kwa baadhi ya wahamiaji wa Burundi 36,000 wanaotaka kurejea makwao, kwa khiyari, kutoka kambi ya Mtabila iliopo wilaya ya Kasulu, kaskazini-magharibi katika Tanzania, kambi ambayo ilipangwa kufungwa mnamo tarehe 30 Juni 2009.

Hapa na pale

KM anatarajiwa kuzuru rasmi Myanmar kuanzia tarehe 03 - 04 Julai, kwa kuitika ombi la Serikali. Atakapokuwepo huko atakutana, kwa mashauriano ya ana kwa ana, na viongozi wakuu wa Serikali ambapo wanatarajiwa kuzungumzia masuala kadha yenye umuhimu kwa UM na jamii ya kimataifa. Alitilia mkazo kwenye mazungumzo yao mambo matatu yatapewa umuhimu wa hadhi ya juu, kwa kulingana na hali ya kisiasa ilivyo nchini kwa hivi sasa. Masuala hayo yanahusu, awali, kuachiwa wafungwa wote wa kisiasa, ikijumlisha Daw Aung Suu Kyi; kurudisha mazungumzo ya upatanishi kati ya Serikali na Wapinzani; na kusailia maandalizi ya uchaguzi wa taifa ulio huru na wa haki.

Bodi la Utawala UNCTAD kutathminia ufufuaji wa kilimo Afrika

Bodi la Utawala la Shirika la UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD) linatarajiwa Ijumanne jioni kukutana Geneva, kufanya tathmini kuhusu juhudi za kufufua kilimo katika bara la Afrika, huduma ambazo zimezorota katikati ya kipindi kilichopambwa na athari haribifu zilizoletwa na mizozo ya uchumi dhaifu kwenye soko la kimataifa.