Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko Mashariki mwa Afrika yafurusha wakimbizi- UNHCR

Mwanamke huyu kutoka Bujumbura, Burundi sasa anaishi na jamaa yake baada ya nyumba yake kufurika.
© UNHCR/Bernard Ntwari
Mwanamke huyu kutoka Bujumbura, Burundi sasa anaishi na jamaa yake baada ya nyumba yake kufurika.

Mafuriko Mashariki mwa Afrika yafurusha wakimbizi- UNHCR

Msaada wa Kibinadamu

Maelfu ya watu, wakiwa ni pamoja na wakimbizi, wanaendelea kukumbwa na mvua kubwa kufuatia mvua za El Niño na mafuriko makubwa yanayozikumba sehemu nyingi za Afrika Mashariki.  Umoja wa Mataifa unataja wakimbizi walioathiriwa ni wale walioko Tanzania, Somalia na Burundi.

 

Akizungumza na wanahabari mjini Geneva, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) Olga Sarrado amesema shirika hilo lina wasiwasi  kuhusu jinsi maelfu ya wakimbizi na watu wengine waliopoteza makazi wanavyolazimika kukimbia tena kuokoa maisha yao baada ya makazi yao kusombwa na maji.

Kambini Dadaab nako hali si shwari

Nchini Kenya, takribani watu 20,000 katika kambi za wakimbizi za Dadaab wamepoteza makazi yao kutokana na kuongezeka kwa viwango vya maji -wengi wao wakiwa wale waliokimbia Somalia kutokana na ukame.

Baada ya vyoo kuharibika na kuhatarisha kusambaa kwa magonjwa yanayoenezwa na maji machafu, baadhi ya wakimbizi hawa wamekimbilia shule jirani licha ya uharibifu mkubwa katika shule hizo. Wengine wamewakimbilia jamaa na marafiki au sehemu nyingine za kambi baada ya kambi zao kuharibiwa.

Bujumbura, Burundi nako kuna mafuriko, wakimbizi wanahaha

Katika mji mkuu wa kibiashara wa Burundi, Bujumbura, familia za wakimbizi pamoja na raia wengi, ikiwa ni pamoja na wazee, wamekuwa wakilazimika kuhama mara kadhaa kufuatia viwango vya maji kuendelea kuongezeka. Katika maeneo mengine huko Burundi, wengi wamelazimika   kusalia katika nyumba zao zilizofurika maji kufuatia ongezeko la kodi maradufu.

Kwa mujibu wa UNHCR, takriban wakimbizi 32,000 nchini humo wanaishi katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko, huku 500 kati yao wakihitaji msaada wa dharura.

Shirika hilo pia limeelezea jinsi chakula na mahitaji mengine muhimu yanazidi kuwa haba tutokana na ongezeko la ada  ya kutumia mitumbwi kusafirisha bidhaa. 

Nchini Somalia, zaidi ya watu 46,000 waliokimbia kutoka kusini mwa nchi wamelazimika kuhama tena kutokana na mafuriko ya ghafla.

Kigoma Tanzania nako wakimbizi wamekumbwa na mafuriko

Tanzania nayo pia imekumbwa na janga hili ambapo zaidi ya wakimbizi 200,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi walioko  katika kambi za wakimbizi za Nyarugusu na Nduta mkoani Kigoma, kaskazini-magharibi mwa Tanzania nao wameathirika. Ofisi ya UNHCR iliyoko  Kigoma nayo imefurika.

Msemaji huyo wa UNHCR amesema kuwa mafuriko haya yanadhihirisha pengo katika maandalizi na hatua za mapema kwani  fedha zilizopo kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi hazifiki kwa wale wanaolazimika kukimbia makwao wala jamii zinazowahifadhi.Wakati huo huo, nchi hizi zinakumbwa na ukosefu wa mikakati ya kujiandaa, kuhimili, na kukabili majanga yanayoletwa na mabadiliko ya tabianchi. 

Sasa UNHCR inachukua hatua gani?

“UNHCR inashirikiana na serikali za mitaa pamoja na washirika, kupeleka misaada muhimu na kutoa huduma za ulinzi kwa wakimbizi na jamii jirani zilizoathiriwa. Nchini Kenya, shirika hili linatoa misaada kwa wakimbizi kama vile mahema, vyandarua vya kujikinga dhidi ya mbu, taulo za kike, sabuni na mitungi ya maji, likilenga hasa watu wazee na watu wenye ulemavu,” amesema Bi. Sarrado.

Kadhalika, shirika hili linasaidia familia kuhamia maeneo salama hadi maji yapungue. Huko Burundi, UNHCR itashirikiana na serikali kutoa msaada wa mahema na wa kifedha utakaowalenga maelfu ya wakimbizi wa zamani waliorejea nchini humo. Ushirikiano huu pia umelenga Tanzania ambapo shirika hili linasaidiana na washirika wa ndani kukarabati makazi ya wakimbizi; huku nchini Somalia, misaada muhimu ya ulinzi na vitu muhimu ikipelekwa kwa familia za wakimbizi wa ndani.

Shirika UNHCR pia  linasema kuwa mabadiliko tabianchi yanaongeza changamoto za kuishi katika sehemu nyingi za dunia hasa maeneo yaliyo  hatarini  kama vile ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika. Dhoruba zinazidi kuwa zenye uharibifu mkubwa. Mioto ya nyika nayo inazidi kuwa jambo la kawaida huku makali ya mafuriko na ukame yakikithiri. 

Baadhi ya athari hizi ni za kudumu na zinatishia kuendelea kuwa mbaya zaidi, na watu waliolazimika kuhamia wanachukua mzigo mkubwa wa athari hizo.

Mnamo Aprili 2024, kwa mara ya kwanza,UNHCR ilizindua mfuko wa kujengea jamii mnepo dhidi ya  tabianchi kwa lengo la kuimarisha  uthabiti wa wakimbizi, jamii zilizolazimika kuhama, na wenyeji wao dhidi ya ongezeko la madhara ya mabadiliko ya tabianchi  hali ya hewa yanayohusiana na matukio ya kupita kiasi ya hali ya hewa.