Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haiti: Magenge ya wahalifu “yana silaha nzito kuliko polisi”

Silaha za moto zilizopokonywa wakati wa ukaguzi wa mpaka.
UNODC
Silaha za moto zilizopokonywa wakati wa ukaguzi wa mpaka.

Haiti: Magenge ya wahalifu “yana silaha nzito kuliko polisi”

Amani na Usalama

Baadhi ya magenge ya wahalifu nchini Haiti yana silaha nzito kuliko polisi wakati huu ambapo makundi ya wahalifu “yanazidi kuwa nguvu, utajiri na kujitawala” kwa kutumia silaha zinazoingizwa kwenye taifa hilo la Karibea kinyume cha sheria, wamesema wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

Matokeo yake, taifa hilo limetumbukia kwenye janga la kisiasa na kibinadamu linaloendelea. Kwa sasa kuna “kiwango kikubwa cha ukosefu wa utawala wa kisheria,” amesema Mwakilishi wa kikanda wa ofisi  ya Umoja wa Mataifa ya kukabili dawa za kulevya na uhalifu, UNODC Sylvie Bertrand akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Kuanzia silaha aina ya AK-47 inayotegenezwa Urusi hadi AR-15 kutoka Marekani hadi bunduki aina ya Galil kutoka Israeli. Ongezeko la uingizaji silaha  hizo kiharamu limepanga moto nchini Haiti tangu mwaka 2023, imesema UNODCkupitia ripoti yake mpya  kabisa kuhusu biashara haramu ya silaha nchini Haiti.

Idadi kubwa ya silaha hizi ndio zinahusishwa na matukio ya hivi karibuni ya mashambulizi kutoka kwa walengaji, uporaji kupindukia, utekaji nyara na mashambulizi kwenye magereza ambayo yaliwezesha maelfu ya wafungwa kutoroka, na wakati huo zaidi ya wahaiti 362,000 kukimbia makazi yao na kusalia wakimbizi.

Watu waliohama makazi yao wakiwa katika uwanja wa ndondi katikati mwa jiji la Port-au-Prince baada ya kukimbia nyumba zao wakati wa mashambulizi ya magenge mnamo Agosti 2023.
© UNOCHA/Giles Clarke
Watu waliohama makazi yao wakiwa katika uwanja wa ndondi katikati mwa jiji la Port-au-Prince baada ya kukimbia nyumba zao wakati wa mashambulizi ya magenge mnamo Agosti 2023.

Uwezo mkubwa wa silaha kuliko polisi

Baadhi ya magenge yanatumia silaha zilizoingizwa Haiti kiharamu kuchochea juhudi za kupanua maeneo yao na kudhibiti maeneo ya kimkakati ambayo  yanasongesha juhudi za kukomesha uingizaji kiharamu wa silaha nchini humo, amesema mtaalamu huru na mwandishi wa ripoti kuhusu Masoko ya Uhalifu  Haiti Robert Muggah.

“Tuna hali isiyokubalika na isiyotulia nchini Haiti, pengine hali mbaya zaidi ambayo nimewahi kushuhudia kwa zaidi ya miaka 20 nikifanya kazi nchini humu,” amesema Bwana Muggah.

Zikiwa zinasafirishwa zaidi kiharamu kutoka Marekani,  “silaha hizi hatari” zinamaanisha kwamba magenge ya uhalifu yana silaha nzito kuzidi zile za Polisi wa Kitaifa Haiti,” kwa mujib uwa jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa waliopatiwa jukumu la kufuatilia vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya Haiti, vilivyowekwa mwaka 2022 kufuatia kushamiri kwa ghasia zinazoendeshwa na magenge ya  uhalifu.

Tatizo ni kwamba kadri silaha zinavyoingia, magenge zaidi ya uhalifu yanapanua ngome zao kwenye maeneo kama vile bandari na barabara, na hivyo kusababisha mamlaka kushindwa kuzuia usafirishaji  haramu wa silaha, amesema Bi. Bertrand wa UNODC.

Ambulensi katika Hospitali Kuu huko Port-au-Prince ikionekana kuwa na dalili za kushambuliwa.
© UNOCHA/Giles Clarke
Ambulensi katika Hospitali Kuu huko Port-au-Prince ikionekana kuwa na dalili za kushambuliwa.

Matokeo yake ni nini?

Baadhi ya madhara yake ni kuzidi kuibuka kwa ghasia zinazosababishwa na magenge nchini Haiti.

Uchambuzi ulioungwa mkono na Umoja wa Mataifa umebaini kuwa nusu ya wananchi wote milioni 11.7 nchini Haiti wanahitaji msaada wa chakula, na idadi kubwa ya wananchi wa Haiti wanazidi kukimbia kusaka usalama. Hospitali zinaripotiwa kuzidi kupokea watu waliouawa kwa risasi au wenye majeraha ya risasa.

“Ongezeko la idadi ya silaha zinazosambaa na vilevile silaha za kisasa linakuwa na athari kwenye aina na ukubwa wa majeraha,” mhudumu wa afya aliwajulisha wataalamu hao kutoka Umoja wa Mataifa.

Moto ukiwaka wakati wahaiti walipoandamana mwaka 2022 kutokana na serikali kushindwa kuwapatia usalama kwenye mji mkuu Port -au-Prince. (MAKTABA)

Watu waandamana katika mitaa ya Port-au-Prince katika Haiti iliyokumbwa na mzozo.
© UNICEF/Roger LeMoyne and U.S. CDC
Watu waandamana katika mitaa ya Port-au-Prince katika Haiti iliyokumbwa na mzozo.

Maeneo yanayodhibitiwa na magenge ya uhalifu

Takribani makundi yenye silaha kati ya 150 hadi 200 yanaendesha operesheni zao nchini Haiti, taifa ambalo linatumia kwa pamoja kisiwa cha Hispaniola na Jamhuri ya Dominika, amesema Muggah, ambaye pia ni mtaalamu wa usalama na maendeleo.

Kwa hivi sasa magenge takribani 23 ya uhalifu  yanaendesha operesheni zao kwenye mji mkuu ​​Port-au-Prince, na yamejigawa kwenye makundi mawili makubwa ya wabia: G-Pèp, likiongozwa na Gabriel Jean Pierre, akijulikana pia Ti Gabriel, na Familia ya G9 na washirika, likiongozwa na Jimmy Chérizier, al maaruf Barbecue.

Katika miezi ya karibuni, makundi haya mawili kinzani, yaliungana kwenye mashambulizi wanayoratibu kwa pamoja, wakilenga uwanja wa ndege, Polisi wa Kitaifa, hospitali, shule, vituo vya polisi, ofisi za kodi na bandari, ili kushinikiza utashi wao wa kupanua maeneo yao ya umiliki, alieleza Bwana Muggah.

“Wahalifu wanadhibiti maeneo ya kimkakati kwenye mji mkuu na barabara kuu kuelekea Port-au-Prince hadi kwenye bandari na mipaka ya ardhini, miji ya pwani ambako tunaona matukio mengi ya usafirishaji haramu,” amesema Muggah.

Gari lililochomwa imetumika kama kizuizi kwenye barabara huko Port-au-Prince. Kukiwa na zaidi ya magenge 150 yanayofanya kazi ndani na nje ya nchi, barabara zote zinazoingia na kutoka katika mji mkuu wa Haiti sasa ziko chini ya udhibiti wa magenge.
© UNOCHA/Giles Clarke
Gari lililochomwa imetumika kama kizuizi kwenye barabara huko Port-au-Prince. Kukiwa na zaidi ya magenge 150 yanayofanya kazi ndani na nje ya nchi, barabara zote zinazoingia na kutoka katika mji mkuu wa Haiti sasa ziko chini ya udhibiti wa magenge.

Mahitaji: Silaha za risasi pan ana zisizoweza kufuatiliwa

Usafirishaji haramu wa silaha ni biashara yenye faida nono, hata iwe ni kwa kiwango kidgo, kwa kuwa mahitaji  ya silaha yanaongezeka na bei ni za juu, lilibaini jopo hilo la wataalamu.

Mathalani, bunduki yenye upana wa milimeta 5.56 inagharimu dola kidogo tu Marekani lakini kwa Haiti huuzwa kati ya dola 5,000 hadi 6,000.

Uchunguzi huo pia umebaini uwepo wa “bunduki zisizoweza kufuatiliwa” bunduki ambazo zinatengenezwa kisiri na mauzo yake ni rahisi mtandaoni, hivyo kuepuka mchakato wa ufuatilaji ambao hukumba zile zinazotengenezwa viwandani. Silaha hizi hazina namba ya ufuatiliaji na hivyo basi huwezi kujua ziko wapi na zinapatikana wapi.

Silaha za moto zilizopokonywa wakati wa ukaguzi wa mpaka.
UNODC
Silaha za moto zilizopokonywa wakati wa ukaguzi wa mpaka.

Usambazaji: Vyanzo na njia za usafirishaji kutoka Marekani

Idadi ndogo ya majenge ya uhalifu nchini Haiti, yamejikita katika kupata, kuhifadhi na kusambaza silaha na risasi, kwa mujibu wa ripoti ya UNODC.

Idadi kubwa ya silaha na bunduki zinazosafirishwa kiharamu nchini Haiti, iwe moja kwa moja au kupitia nchi nyingine, zinatokea Marekani, amesema Bi. Betrand wa UNODC, akiongeza kuwa silaha na bunduki zinanunuliwa kutoka maduka yenye leseni, maduka ya maonesho ya bunduki au husafirishwa kwa njia ya bahari.

Ameongeza kuwa shaka na shuku zimeibuka juu ya uwepo wa operesheni kinyume cha sheria zinazohusisha ndege zisizosajiliwa na viwanja vya ndege kupitia pwani ya kusini mwa Flora na uwepo wa viwanja vidogo vya ndege vya kisira nchini Haiti.

Msako wa usafirishaji haramu wa silaha

UNODC imebaini njia nne zinazotumiwa kusafirisha kiharamu kupitia mipaka isiyo na ulinzi ya Haiti, mbili kutokea Florida kwa kutumia meli za mizigo hadi Port-au-Prince hadi pwani za kaskazini na magharibi kupitia Turks na Caicos na Bahamas na nyingine kupitia kontena za mizigo, meli za uvuvi, boti za kusindikizia meli au ndege ndogo zinazowasili kwenye mji wa kaskazini wa Cap Haitien na kwa njia ya ardhini kutokea Jamhuri ya Dominica.

Kwa kiwango kubwa silaha zinakamatwa na Marekani  kwenye msako huko Miami na ingawa mamlaka za udhibiti zimeongeza maradufu silaha zilizokamatwa mwaka 2023, mamlaka bado zinashindwa kukamata silaha na risasi ambazo mara nyingi hufichwa kwenye vifurushi vilivyofungashwa katika maumbo na ukubwa mbali mbali, imesema UNDOC.

Ili kudhibiti uingiaji wa silaa nchini humo, ofisi hiyo ya  Umoja wa Mataifa inapatia mafunzo vitengo vya udhibiti bandari na viwanja vya ndege, vikijumuisha polisi na maafisa wa forodha, na walinzi wa pwani ili kubaini na kukagua konteni zilizo hatarini zaidi kubeba silaha. Halikadhalika wanashirikiana kuwezesha matumizi ya rad ana mbinu nyingine za kisasa.

Watu waliokimbia makwao kutokana na machafuko wakipata hifadhi sasa shuleni Port-au-Prince
© IOM/Antoine Lemonnier
Watu waliokimbia makwao kutokana na machafuko wakipata hifadhi sasa shuleni Port-au-Prince

Jamii ya kimataifa iongeze juhudi

Lakini, kwa Haiti kuweza kufuatilia na kudhibiti mipaka yake yote, utulivu unapaswa kuimarishwa, amesema Afisa huyo, akiongeza kuwa maafisa polisi wamejikita kujaribu kudhibiti ghasia kwenye mitaa ya Port-au-Prince.

Kuhusu ujumbe wa kimataifa wa usaidizi wa usalama Haiti unaosubiriwa na ambao umepatiwa mamlaka na Baraza la  Usalama la Umoja wa Mataifa, Bi. Bertrand amesema itakuwa vema kusaidia kazi ya kijasiri ambayo tayari imefanywa na polisi.

Bwana Muggah anakubali, akisema kuwa kuimarisha Polisi wa Kitaifa Haiti ni kipaumbele kisicho na upinzani.

“Katika mazingira ya kisiasa na kijiografia ambako watu wengi wakati mwingine hawachukui hatua haraka,” ameonya kuwa jamii ya kimataifa ina wajibu muhimu wa kusaidia Haiti katika zama hizi za uhitaji, kwa sababu hali mbaya inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo hatutachukua hatua.”