Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Syria: Kueleka miaka 13 ya mzozo, Guterres ataka suluhu ya kudumu ya mzozo

Mtoto akiwa amebeba dawa aliyopatiwa na wahudumu wa afya kwenye kliniki tembezi huko Aleppo nchini Syria.
© UNICEF/Khudr Al-Issa
Mtoto akiwa amebeba dawa aliyopatiwa na wahudumu wa afya kwenye kliniki tembezi huko Aleppo nchini Syria.

Syria: Kueleka miaka 13 ya mzozo, Guterres ataka suluhu ya kudumu ya mzozo

Amani na Usalama

Miaka 13 inaelekea kutimu tangu kuanza kwa mapigano nchini Syria wakati huu ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anazungumzia udharura wa kupatikana kwa suluhu ya kisiasa nchini humo huku akisisitiza ulinzi wa raia na hali mbaya ya kiutu inayokabili wananchi.

Taarifa iliyotolewa leo na msemaji wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani inamnukuu Katibu Mkuu akisema mwezi Machi ni kumbukizi ya miaka 13 ya mzozo nchini Syria, ulioanza tarehe 15 mwezi Machi mwaka 2011, mzozo unaombatana na mfumo wa ukatili na machungu yasiyojulikana dhidi ya raia.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa watu milioni 16.7, sawa na asilimia 70 ya wananchi wote wa Syria, watahitaji msaada wa kiutu mwaka huu wa 2024. Takribani nusu ya idadi ya wananchi wa Syria kabla ya kuanza kwa vita bado wanasalia kuwa wakimbizi wa ndani au nje ya Syria.

Majanga mfululizo, yakiambatana na matetemeko ya ardhi yaliyokumba taifa hilo mwezi Februari mwaka jana, yamesababisha vifo vya watu wapatao 5,900, miundombinu imeharibika na kuzidi kutwamisha mamilioni ya watu ambao tayari walikuwa wanahaha kupata misaada ya kuwawezesha kuishi.

Jamii zinahaha kuishi, wakati huu ambapo ufadhili wa misaada ya kiutu umepungua na kufikia kiwango cha chini zaidi. Mwaka 2023, ni dola bilioni 2.02 tu sawa na asilimia 37.4 zilipatikana kati ya dola bilioni 5.41 zilizohitajika ili kufanikisha operesheni za usaidizi zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa.

Vifaa vya kujisafi vikisambazwa kwa familia kaskazini-magharibi mwa Syria, familia ambazo ziliathiriwa na tetemeko la ardih. (maktaba)
© UNICEF/Joe English
Vifaa vya kujisafi vikisambazwa kwa familia kaskazini-magharibi mwa Syria, familia ambazo ziliathiriwa na tetemeko la ardih. (maktaba)

‘Fanyeni liwezekanalo’

Ni kwa kuzingatia hilo, Katibu Mkuu kupitia taarifa yake ametaka wadau kufanya kila liwezekanalo kufikia suluhu ya kisiasa ambayo ni ya dhati na halali.

Amesema “jawabu ambalo ameesma litakidhi matamanio halali ya wananchi wa Syria, lirejeshe uhuru wa nchi na umoja kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2254 la mwaka 2015  na pia liweke mazingira yanayotakiwa kuwezesha wakimbizi warejee nyumbani kwa hiari kwa njia salama, na utu.”

Ulinzi wa raia

“Tunahitaji kulinda pia raia pamoja na miundombinu ya kiraia,” amesisitiza Katibu Mkuu.

Halikadhalika ametoa wito wa hatua za kimkakati za kukabili ugaidi, kwa mujibu wa sheria za kimataifa; ufikishaji misaada ya kiutu bila vikwazo vyovyote kote Syria na ufadhili wa dharura ili kuendeleza operesheni za kiutu ambazo ni muhimu.

“Muda mrefu umepita mno kwa pande muhimu kuongeza juhudi zao na kukidhi mahitaji haya. Kizazi kizima cha Syria tayari kimelipa gharama kubwa,” ameonya Katibu Mkuu.

Tokomeza ukwepaji sheria

Bwana Guterres pia amemulika suala la watu kukamatwa kiholela nchini Syria, watu kutoweshwa, mauaji ya kiholela na ukatili wa kijinsia akisema vinaendelea kukwamisha amani endelevu nchini humo.

“Tuna wajibu wa kumaliza ukwepaji sheria,” amesema.

“Mamia ya maelfu, kama sio mamilioni ya manusura na waathirika pamoja na familia zao wanategemea hatua hizo,” amesema Katibu kwao.