Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO na NASA Harvest wapeleka tabasamu kwa wakulima

Wakulima wa Malawi. Mbali na matumizi yake kwa ajili ya kukabiliana na majanga yahusianayo na mabadiliko ya tabianchi, takwimu za makadirio ya mavuno iliyokusanywa katika GIEWS ni muhimu sana kwa wakulima, ikiruhusu mipango bora katika msururu wa ugavi w…
©NASA Harvest/Christina Justice
Wakulima wa Malawi. Mbali na matumizi yake kwa ajili ya kukabiliana na majanga yahusianayo na mabadiliko ya tabianchi, takwimu za makadirio ya mavuno iliyokusanywa katika GIEWS ni muhimu sana kwa wakulima, ikiruhusu mipango bora katika msururu wa ugavi wa chakula cha kilimo.

FAO na NASA Harvest wapeleka tabasamu kwa wakulima

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katika nyakati za zamani, wakulima walikuwa wakiangalia anga la usiku ili kujua wakati sahihi wa kupanda au kuvuna, katika zama za sasa taarifa hizo hazipatikani tena kutoka kwenye kuangalia nyota, bali kutoka kwenye unajimu unaotengenezwa na wanadamu kwa kutumia programu za simu.

Matumizi ya zana hizi za ubunifu yanawasaidia wakulima kulima chakula vizuri, pia inasaidia serikali kufanya maamuzi bora ya sera na inaweza kuchukua jukumu lisiloweza kupimika katika kusaidia juhudi za misaada kufikia haraka wale wenye uhitaji wakati wa maafa.

Kupitia Mfumo wake wa Taarifa za Ulimwenguni na Tahadhari za Mapema kuhusu chakula na kilimo (GIEWS), Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) limeungana na Muungano wa Usalama wa Chakula na Kilimo Duniani wa Utawala wa Kitaifa wa Anga (NASA), inayojulikana kama NASA Harvest, ili kuboresha makadirio ya mavuno ya mazao, kutoa masuluhisho yaliyotengenezwa maalum ili kutathmini mazao na kusaidia kupanga majibu ya haraka kwa maafa.

Kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID), mradi huu, uliozinduliwa mwaka 2021, unachanganya takwimu za utafiti ziliyokusanywa moja kwa moja kutoka shambani kwa kutumia programu ya simu pamoja na picha za satelaiti za shamba zilizopigwa kutoka angani, vifurushi viwili vya takwimu kisha vinawekwa kwenye mifano ya ujifunzaji wa mashine ili kutoa ramani zinazoeleza ardhi ya kilimo kwa usahihi zaidi na kutoa ufahamu juu ya hali ya mazao.

Ndoa hii ya vyanzo vya takwimu vya shamba na satelaiti ni muhimu hasa katika nchi kama Malawi na Namibia, ambako shamba ya wakulima wadogo ni sehemu kubwa ya maeneo fulani zaidi, na satelaiti pekee haziwezi kutambua mipaka ya mashamba ya kilimo kwa urahisi.

Wanaume wanafanya kazi ya kutengeneza barabara iliyoharibika katika Wilaya ya Mulanje nchini Malawi baada ya Kimbunga Freddy. (Maktaba)
© UNOCHA/Jane Kiiru
Wanaume wanafanya kazi ya kutengeneza barabara iliyoharibika katika Wilaya ya Mulanje nchini Malawi baada ya Kimbunga Freddy. (Maktaba)

Athari za Kimbunga Freddy

Nchini Malawi, FAO na NASA Harvest, linalo ongozwa na Chuo Kikuu cha Maryland, walitumia zana za kidijiti na za upelelezi wa mbali zilizozalishwa kama sehemu ya mradi huo kutoa tathmini ya haraka ya mafuriko yaliyosababishwa na Kimbunga cha Tropiki Freddy mwezi Machi na Aprili mwaka 2023.

Freddy ilileta mvua za miezi sita ndani ya siku sita tu, ikisababisha vifo vya zaidi ya watu 500 na kuwakosesha makazi takriban watu 565,000, kuongeza huzuni, jambo baya zaidi ni kwamba mfumo wa hali ya hewa uliikumba Malawi mwishoni mwa msimu wa mvua, wakati viwango vya mito vilikuwa tayari juu.

Tathmini hiyo, iliyotekelezwa na Wizara ya Kilimo ya Malawi kwa msaada wa kiufundi kutoka kwa maafisa wa FAO na NASA Harvest walio kwenye ardhi nchini Malawi, ilikusanya takwimu kutoka mashamba 2,095 katika wilaya 11 kusini mwa nchi hiyo.

Kati ya wakulima waliohojiwa, asilimia 86 waliripoti mafuriko kwenye mashamba yao, zaidi ya robo ya wakulima walipoteza akiba ya chakula kutokana na mafuriko, na karibu asilimia 40 ya wakulima waliripoti vifo vya mifugo, karibu wakulima wote waliohojiwa waliripoti kwamba mavuno ya sasa hayatoshi kukidhi mahitaji yao ya kaya hadi mavuno ya Aprili 2024.

Takwimu hiyo yenye ilitolewa ndani ya siku badala ya wiki, Katika hali ya dharura, kasi na usahihi kama huo unaweza kuleta mabadiliko ulimwenguni kwa juhudi za usaidizi na majibu.

"Matokeo ya tathmini ya shamba yalitoa ufahamu muhimu juu ya athari za Freddy, na kuipa serikali taarifa muhimu za misaada kwa wakati kwenye maeneo na watu wanaohitaji zaidi," alisema Jonathan Pound, Mchumi wa FAO anayefanya kazi na GIEWS.

Ramani hizi za ardhi ya kilimo za Malawi zilitengenezwa kwa kutumia modeli za mashine ya kujifunza ya NASA Harvest na takwimu za ardhini. Bluu nyepesi inaonyesha maeneo ya mashamba yaliyofurika na Kimbunga Freddy.
©FAO/NASA Harvest/Malawi Ministry of Agriculture/UNOSAT
Ramani hizi za ardhi ya kilimo za Malawi zilitengenezwa kwa kutumia modeli za mashine ya kujifunza ya NASA Harvest na takwimu za ardhini. Bluu nyepesi inaonyesha maeneo ya mashamba yaliyofurika na Kimbunga Freddy.

Jinsi Inavyofanyika nchini Malawi

Ili kukusanya takwimu za msingi ambazo tathmini za haraka kama hizi zinategemea, maafisa kutoka Wizara ya Kilimo, waliopatiwa mafunzo na FAO na NASA Harvest kwa njia ya mtandao, walikusanya takwimu kwenye ardhi kwa kutumia programu ya simu, iliyounganishwa na GPS ili kuashiria mahali sahihi pa shamba.

Programu hiyo ni rahisi kutumia na hukusanya taarifa wakati maafisa wa eneo hilo wanatembea kati ya mistari ya mazao, Kwa kuwa pia inafanya kazi nje ya mtandao, programu hiyo inapunguza gharama na huwapa watumiaji uhuru wa kupakia takwimu baadaye.

Kila shamba linatambulishwa kwa kuratibu  GPS na kuweka  jina la aina ya mazao yanayopandwa, pamoja na taarifa nyingine nyingi kuhusu shamba, takwimu hizi kisha hutumika kufundisha mifumo ya ujifunzaji ya mashine inayotambua ardhi ya kilimo na aina za mazao kutoka kwa picha za satelaiti, na kutoa ramani zenye msongo wa juu.

Jinsi inavyofanya kazi nchini Namibia

Nchini Namibia, ambayo ilikumbwa na ukame mwaka 2023, programu ya simu iliruhusu maafisa wa eneo na maafisa ugani kukamilisha jumla ya tathmini 4,500, badala ya 600 ambazo zingefanywa kwa kutumia karatasi na kalamu, njia hii si tu ni nafuu na sahihi lakini pia inapunguza muda kwa kuwa taarifa zote ni sanifu

Zaidi ya kuongeza kasi ya shughuli na kupunguza gharama, "faida kubwa ni kuboresha kwa kiasi kikubwa ubora wa takwimu inayokusanywa," alisema Samuel Kirichu, Afisa wa FAO anayefanya kazi katika ofisi ya nchi ya Malawi.

Hii ni kweli hasa kwa wakulima wadogo ambao mara nyingine hawana maarifa sahihi kuhusu ukubwa wa mashamba yao, kuwa na takwimu sahihi zaidi ya ardhi yao kunaweza kusaidia kutoa taarifa bora kuhusu matumizi yao ya pembejeo kama vile mbegu na mbolea, kuepuka hatari ya kurutubisha Zaidi na kupunguza gharama zao.

Kulingana na Christina Justice, kiongozi wa Usalama wa Chakula na tahadhari ya mapema kwa NASA Harvest, takwimu zinazokusanywa kwa njia hii pia husaidia kutambua maeneo ambayo kuna tishio la maendeleo kwa mazao, kama vile ukame na magonjwa, aidha, kuwa na "makadirio ya mavuno yanavyoonekana miezi kadhaa kabla ya mavuno ni muhimu sana," kwani inaruhusu mipango bora kwenye mlolongo wa usambazaji wa kilimo-chakula.

Maarifa haya ni muhimu sana msimu huu wa kilimo, kwani athari za El Nino zinatarajiwa kuhatarisha mavuno nchini Malawi.

"Pamoja na utabiri wa El Nino kuleta hali ya ukame msimu huu, ufuatiliaji wa karibu wa mazao na upatikanaji wa haraka wa takwimu ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote," alisema Pound.

Zaidi ya hayo, FAO na NASA Harvest wanapanga kutoa makadirio ya mapema ya mavuno kwa msimu wa 2023/2024 kwa Wizara za Kilimo huko Malawi, Namibia, na Kazakhstan, kazi pia inaendelea ili kuboresha tathmini za mazao kwa kutumia simu na kupanua mradi huo kwa nchi nyingine.