Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi 15 zimechaguliwa kwenye Baraza la Haki za Kibanadamu, Urusi haimo

Baraza Kuu limechagua wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu HRC
UN Photo/Cia Pak
Baraza Kuu limechagua wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu HRC

Nchi 15 zimechaguliwa kwenye Baraza la Haki za Kibanadamu, Urusi haimo

Haki za binadamu

Leo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limefanya uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa HRC, ambapo nchi 17 ziliingia kwenye kinyang’anyiro kugombea nafasi 15 kutoka kwa makundi tofauti ya kikanda. 

Nchi zilizochaguliwa, zitahudumu katika HRC kwa miaka mitatu, kuanzia Januari 1, 2024. 

Kutokana na kura hiyo, Baraza hilo lilijumuisha Burundi, Cote d’Ivoire, Ghana, Malawi, China, Indonesia, Japan, Kuwait, Albania, Bulgaria, Brazil, Jamhuri ya Dominika, Cuba, Ufaransa na Uholanzi. 

Nchi tatu ambazo ni Albania, Bulgaria na Shirikisho la Urusi, zilikuwa zikigombea viti viwili ambavyo vitajumuishwa upya  kutoka kwenye kundi la nchi za Ulaya ya Kati na Mashariki. 

Nchi 160 zilipiga kura ya kukikubali Bulgaria kwa Baraza la Haki za Binadamu, nchi 123 zilikwenda kwa Albania, na nchi 83  kura zao zilikwenda kwa Urusi. 

Nchi zote, isipokuwa Jamhuri ya Dominika, zilizochaguliwa kwa HRC leo zilikua wanachama wa zamani wa Baraza hilo. 

Nani anaweza kugombea ujumbe wa Baraza hilo

Nchi yoyote ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa inaweza kugombea kiti katika Baraza la Haki za Kibanadamu isipokuwa ikiwa tayari imetumikia mihula miwili mfululizo kama mjumbe wa Baraza. 

Uchaguzi wa HRC hufanyika katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo nchi zote 193 ambazo ni wanachama hushiriki.