Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi maskini zashindwa kupatia wananchi fedha za kuchechemua uchumi wakati wa COVID-19 - Ripoti

Mifumo ya chakula barani Afrika imevurugwa kwa kiasi kikubwa kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi na hivi karibuni zaidi janga la Corona.
© FAO/Petterik Wiggers
Mifumo ya chakula barani Afrika imevurugwa kwa kiasi kikubwa kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi na hivi karibuni zaidi janga la Corona.

Nchi maskini zashindwa kupatia wananchi fedha za kuchechemua uchumi wakati wa COVID-19 - Ripoti

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, limerudisha nyuma maendeleo yaliyopatikana kwa mamilioni ya watu katika nchi maskin ina kuongeza pengo kubwa zaidi la ukosefu wa usawa, imesema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa hii leo jijini New York, Marekani.

 

Ripoti hiyo ya ufadhili kwa maendeleo endelevu ya mwaka 2021 iliyotolewa na kikosi kazi cha ufadhili kwa maendeleo imeonesha kuwa uchumi wa dunia umekumbwa na mdororo ambao haujawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 90.

Jamii zilizo hatarini zaidi ndio zimeathirika zaidi ambapo ajira milioni 114 zimepotea, watu milioni 120 wametumbukia katika uhohehahe.

Tofauti kubwa zaidi katika hatua za kukabiliana na janga la COVID-19 zimeongeza pengo au nyufa zilizokuwepo kati ya nchi na nchi na wat una watu, imesema ripoti hiyo iliyoandaliwa na mashirika 60 ya kimataifa.

Ripoti inasema “wakati fungu la kihistoria la dola trilioni 16 limetolewa na serikali mbalimbali duniani ili kuchechemua uchumi na kupunguza madhara ya janga la Corona, ni chini ya asilimia 20 ya fedha hizo zimetumika katika nchi zinazoendelea.”

Kwa upande wa chanjo dhidi ya Corona ambazo tayari zimeanza kutolewa katika maeneo mbalimbali duniani kama njia ya kukabiliana na ugonjwa huo, ni nchi 9 tu kati ya nchi 38 ambazo zinatoa chanjo hizo ndio nchi zinazoendelea. Nchi nyingi ni zile tajiri.

Chanjo ya AstraZeneca dhidi ya COVID-19 ikiwasili kwenye kituo cha kuhifadhia chanjo mjini Kinshasa DRC
© UNICEF/Sibylle Desjardins
Chanjo ya AstraZeneca dhidi ya COVID-19 ikiwasili kwenye kituo cha kuhifadhia chanjo mjini Kinshasa DRC

Kabla ya janga la Corona, takribani nusu ya zinazoendelea na zile za kipato cha chini zilikuwa katika tishio au tayari zilikuwa zinakumbwa na mzigo wa madeni. 

Ripoti inaonya kuwa huku nchi hizo zikiwa pia na tatizo la kupungua kwa mapato yatokanayo na kodi, mzigo wa madeni umezidi kuwa mkubwa na kuweka mashakani ufanikishaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ifikapo mwaka 2030.

Ripoti inasema kuwa hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kushughulikia kitendo cha kuongezeka kwa pengo la ukosefu wa usawa, na hatimaye kujenga upya na kwa ubora zaidi jamii na kuzuia kurejea nyuma kwa hatua za kimaendeleo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amesema, “ripoti ya leo ina mapendekezo muhimu; inatoa wito kwa serikali kuwekeza katika ulinzi wa watu wake, miundombinu endelevu na ajira zisizoharibu mazingira. Halikadhalika inatoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia nchi maskini zaidi na zilizo hatarini kwa kusamehe madeni na hatua nyingine za kuziwezesha kuwa na uwezo wa kifeha ikiwemo kuwapatia haki za ziada za kukopa.”

Ripoti pia inapendekeza nchi hizo kupatiwa kipindi kirefu cha kurejesha mikopo bila riba na kuoanisha masoko ya mitaji na maendeleo endelevu kwa kuondoa motisha ya muda mfupi kwenye mnyororo wa uwekezaji.

Bi. Mohammed amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake umejizatiti kuendelea kuhakikisha kuwa nchi zote zinaibuka sawa kutoka janga la Corona na zinakuwa na fursa sawa wa kujijenga upya salama, haraka na kwa mustakabali sawia na endelevu.
TAGS: Ufadhili kwa Maendeleo, SDGs, Amina J. Mohammed