Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Picha ya juu ikionesha mtaa wa mabanda wa Mathare mjini Nairobi Kenya

Maji ni muhimu ili makazi duni Kenya yadhibiti COVID-19

UN-Habitat/Julius Mwelu
Picha ya juu ikionesha mtaa wa mabanda wa Mathare mjini Nairobi Kenya

Maji ni muhimu ili makazi duni Kenya yadhibiti COVID-19

Afya

Lengo namba 6 la malengo ya maendeleo endelevu, SDG, linalenga kufanikisha upatikanaji wa maji kwa wote na kwa usawa ifikapo mwaka 2030. Lakini bado ulimwenguni kote, kama ripoti ya maendeleo ya maji ya Umoja wa Mataifa, ilivyoonesha, mabilioni ya watu bado wanakosa maji safi na salama na huduma za kujisafi na watu wanaachwa nyuma kwa sababu mbalimbali ikiwemo  ubaguzi kwa misingi ya jinsia, kabila, tamaduni na hali ya kijamii.

 

Haki ya raia wote wa Kenya kupata maji safi na yenye ubora kwa idadi ya kutoshesheleza,  imewekwa katika Katiba ya nchi. Hata hivyo, utafiti huo umebaini kuwa wakati makundi ya mijini yanapata maji bora kuliko maeneo ya vijijini, bado kuna ukosefu wa  usawa katika upatikanaji na uwezo wa kununua kwa watu wanaoishi kwenye makazi yasiyo rasmi.

Kunawa mikono bado ni changamoto

Kenya ina idadi ya watu milioni 47.5 na takriban asilimia 60 ya wakazi wake wa mijini wanaishi katika makazi yasiyokuwa rasmi, wengi wao ni katika miji ya Nairobi, Mombasa na Kisumu.

Kufuatia kuthibitishwa kwa mgonjwa wa kwanza wa virusi vya Corona au COVID-19 katikati ya mwezi Machi mwaka 2020, kwa kufuata nyayo za mataifa mengine ulimwenguni zinazokabiliwa na janga hilo na mapendekezo ya shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, serikali iliwasihi wananchi kufuata kanuni za WHO za kunawa mikono,  usafi na kutochangamana   Lakini bado ni vigumu  kutekeleza hatua hizi katika makazi duni ambako upatikanaji wa maji si wa uhakika na kutochangamana hakuwezekani

Ni wakazi wachache tu wanaokaa  katika makazi duni ambao wanapata huduma ya maji, ya umma ambayo ni ya gharama kidogo. Katika makazi yasiyokuwa rasmi, usambazaji wa maji umebinafsishwa na vikundi na wakazi wengi wanategemea wachuuzi wa maji binafsi, haswa wakati wa kiangazi.

 

Idadi kubwa ya waliohojiwa hutumia zaidi ya asilimia tatu ya kipato cha mwezi cha kaya kununua maji, kiwango ambacho ni cha kimataifa cha bei nafuu. Kwa kuzingatia kuwa wakazi wa makazi yasiyo rasmi hulipa hadi mara 50 ya bei ya maji kwa lita kuliko kaya za tabaka la kati, na kupata maji mengi ya kunawa mikono mara kwa mara ni changamoto ya kiuchumi.

Zaidi ya hayo, asilimia 35 ya waliohojiwa kwenye uchunguzi walionesha kuwa inawachukua zaidi ya dakika 30 kupata maji kwa sababu kuna maeneo machache ya maji wanakoishi na wanalazimika kusafiri umbali mrefu kuchota maji. Waliohojiwa pia walionesha tukio kubwa la magonjwa yanayotokana na maji kama vile kipindupindu katika jamii zao, kama matokeo ya uchafu kwa sababu mifereji ya maji taka iko katika hali mbaya.

Masuala mengi yanayohusiana na usalama yaliongezwa wakati wa uchunguzi, mara nyingi na wanawake ambao wakati mwingine hulipa watu kuwalinda wakati wanateka maji baada ya giza. "Wakati wa mchana, ni vigumu sana kwa sababu watu wengi wanataka maji, kwa hivyo napenda kuteka maji usiku. Lakini sio salama kwa sababu watu wanaporwa, "mhojiwa mmoja alisema. Wengine walionesha kuongezeka kwa uhalifu wakati wanalazimika kuacha nyumba zao bila kutarajia kusafiri umbali mrefu ili kuteka maji usiku.

Mtaa wa mabanda wa Mathare, jijini Nairobi, Kenya.
© Julius Mwelu/ UN-Habitat
Mtaa wa mabanda wa Mathare, jijini Nairobi, Kenya.


Haki ya maji, "suala la uzima na kifo" wasema watetezi wa haki mashinani.

"Serikali inapaswa kutambua kwamba kuwa na maji safi ni haki yetu. Wanaweza kupatia Ikulu maji safi kwa hiyo inapaswa kuwapatia maji safi wakazi wa Mathare. Sisi sio watu tusio na thamani,” alisema Njeri Mwangi wa Kituo cha Haki ya Jamii cha Mathare. 

Ili kutekeleza mradi wa uchunguzi, ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilishirikiana na mtandao wa vituo 24 vya haki za kijamii, SJCs, katika maeneo ya Nairobi, Kisumu na Pwani. Vituo hivyo vya kijamii, ni muhimu katika kupazia sauti wasio na sauti na vikundi vya pembezoni ili kuonesha ukosefu wa usawa wanaokabiliwa nao katika kupata maji safi, na hivyo kuelezea vipaumbele vyao na kufanikisha lengo namba 6 la SDGs mashinani.

Tangu mwaka 2017, ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeshirikiana na SJCs nchini Kenya na kuibua kazi za vituo hivyo na masuala ya haki za binadamu yanayokabili makazi duni. Mradi huu ulikuwa ni fursa nyingine ya kusaidia vituo hivyo na kujenga uwezo wa watetezi vijana wa haki za binadamu mashinani.