Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi yataka iondolewe kwenye ajenda ya Baraza la Usalama

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Burundi Ezechiel Nibigira akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA74.
UN Photo/Cia Pak
Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Burundi Ezechiel Nibigira akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA74.

Burundi yataka iondolewe kwenye ajenda ya Baraza la Usalama

Amani na Usalama

Mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA74 ukitamatishwa hii leo  jiijni New York, Marekani, Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Burundi Ezechiel Nibigira amehutubia jukwaa hilo akitaka ajenda ya Burundi kwenye Baraza la Usalama iondolewe kwa kuwa hali ya usalama nchini humo ni tulivu.

Waziri Nibigira amesema hali ya usalama ni nzuri na tulivu kuanzia kaskazini hadi kusini, mashariki hadi magharibi na kwamba wananchi wanatekeleza haki zao za kiraia na kisiasa bila kikwazo chochote.

Katu hatujaacha kusema ya kwamba Burundi inawekwa kwenye ajenda ya Baraza la Usalama kwa sabau za kisiasa na maslahi ya wageni ambao hawana jema na wananchi wa Burundi. Hali ya kisiasa na usalama ndani ya nchi yangu haina tishio lolote la usalama wa kimataifa kiasi cha kuhalalisha kuwekwa katiak ajenda ya Baraza la Usalama,” amesema Waziri Nibigira.

Uchaguzi Mkuu 2020

Akizungumzia uchaguzi mkuu wa 2020, Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Burundi amesema, “maandalizi yanaendelea vyema na kwamba tayari mifumo ya kitaifa ya maandalizi iko sawa kuhakikisha kuwa uchaguzi huo mkuu unakuwa wa wazi, huru na wa haki. Kamisheni ya taifa ya uchaguzi, CENI tayari inafanya kazi.”

Waziri Nibigira amesema kwa mujibu wa kalenda yao, uchaguzi huo wa rais, wabunge na madiwani utafanyika tarehe 20 mwezi Mei mwaka 2020 na kwamba, “kampeni za uchaguzi zitaanza tarehe 27 mwezi Aprili hadi 17 mwezi Mei. Uchaguzi wa maseneta utafanyika tarehe 20 mwezi Julai mwaka 2020 ilhali  ule wa madiwani wavitongoji utafanyika tarehe 24 Agosti mwaka 2020.”

Hali ya kibinadamu Burundi

Waziri Nibigira amesema kuhusu hali ya kibinadamu, tunapongeza kitendo cha kurejea kwa kiwango kikubwa wakimbizi wa Burundi ambao walikimbia nchi yao mwaka 2015. Halikadhalika maelfu ya wakimbizi wa Burundi wanarejea wenyewe kwa hiari bila msaada wa shirika la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR. Kati ya tarehe 1 Agosti mwaka 2017 hadi tarehe 23 mwezi huu wa Septemba, wakimbizi 77,080 kutoka kaya 25,666 walirejea kwa hiari kutoka Tanzania, Kenya na DR Congo.”

Amesisitiza kuwa, kasi hii ya kurejea nyumbani ni ishara tosha ya kuwepo kwa amani, utulivu na imani na taifa lao la Burundi bila kujali kauli za wachochezi wa kigeni wanaoendelea kuzitoa ili kuhakikisha kuwa wakimbizi wanasalia uhamishoni.

Marekebisho ya mundo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Akizungumzia hoja hii ya marekebisho ya mundo wa Baraza la Usalama ambalo tangu kuanzishwa kwake wajumbe wa kudumu wenye kura turufu ni watano; Uingereza, Marekani, Ufaransa, Urusi na China, Waziri Nibigira amesema, “Burundi inashikilia msimamo wa bara la Afrika kupitia makubaliano ya Ezulwini na azimio la Sirte yanayotaka kuona marekebisho dhidi ya ukosefu wa haki kwa Bara la AFrika kutokuwa na kiti cha kudumu kwenye Baraza hilo. Tangu miaka kadhaa sasa, Afrika haijaacha kulaumu ukosefu huu wa haki wa kihistoria unaonyima takribani watu bilioni 1.2  haki yao ya kuwakilishwa.”

Wakimbizi wa Burundi wanaorejea nchini mwao kutoka Tanzania wakiwa kwenye kituo cha mpito cha Mabanda katika jimbo la Makamba nchini Burundi. (24 Aprili 2018)
OCHA/Christian Cricboom
Wakimbizi wa Burundi wanaorejea nchini mwao kutoka Tanzania wakiwa kwenye kituo cha mpito cha Mabanda katika jimbo la Makamba nchini Burundi. (24 Aprili 2018)

Mpango wa amani Afrika

Mpango huu wa amani barani Afrika nao ulikuwa sehemu ya hotuba ya Waziri huyo wa Burundi ambaye amesema, “Burundi inaunga mkono kwa dhati mpanog wa Muungano wa Afrika wa kukomesha milioni ya mitutu bunduki barani humo kati ya sasa hadi mwaka 2020, mpango ambao Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeunga mkono kupitia azimio namba 2457. Kwa mantiki hiyo tunatiwa moyo na maendeleo mapya huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Sudan na Sudan Kusini.”