Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sera ya Uganda ya kufungua milango kwa wakimbizi yatatizwa

Wanawake wakichota maji katika makazi ya wakimbizi ya Nakivale nchini Uganda.
© UNHCR/Esther Ruth Mbabazi
Wanawake wakichota maji katika makazi ya wakimbizi ya Nakivale nchini Uganda.

Sera ya Uganda ya kufungua milango kwa wakimbizi yatatizwa

Wahamiaji na Wakimbizi

Idadi ya wakimbizi wanaokaribishwa nchini Uganda kutoka Sudan inazidi  kuongezeka, baadhi yao wakifika mji mkuu wa Uganda, Kampala tangu mwanzo wa mwaka wa 2024  wakitafuta usalama kutokana na vita ambayo imedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja, inaeleza taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi (UNHCR).

Taarifa hiyo iliyotolewa leo leo Mei 17 huko Geneva, Uswisi inafafanua kuwa pamoja na wakimbizi wa Sudan, wastani wa watu 2,500 wanaingia Uganda kila wiki, hasa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan Kusini, wakisukumwa na migogoro inayoendelea na changamoto zinazohusiana na hali ya hewa.  

Upungufu wa fedha umeathiri sana sekta ya afya inayo wahudumia wakimbizi na jamii zinazowazunguka. Hali ambayo imepelekea kupunguzwa kwa Idadi ya wafanyakazi wa vituo vya afya na upungufu wa vifaa vya kukidhi mahitaji muhimu ya afya. 

Mlipuko wa ugonjwa wa macho mekundu (conjunctivitis) kote nchini pia umeathiri makazi kadhaa ya wakimbizi  ikiwemo makazi ya Nakivale na kuna wasiwasi kuwa ugonjwa huu unaweza kuwa mbaya zaidi kutokana na upungufu wa maji na sabuni. Pia kuna wasiwasi wa afya ya akili ambapo wakimbizi wanne wameripotiwa kujaribu  kujiua miongoni mwao wakiwa ni vijana.

Msongamano shuleni 

Shule zimejaa kupita kiasi na hakuna walimu wa kutosha wala vifaa vya elimu hali inyofanya iwe vigumu kwa watoto ambao wanawakilisha zaidi ya nusu ya jumla ya wakimbizi kupata elimu. Huduma muhimu kama vile usajili wa wakimbizi unakumbwa na ucheleweshaji mrefu kwa sababu ya ukosefu wa vifaa na zana muhimu zinazofanya mchakato uwe mwepesi. 

Uwekezaji katika kusaidia wakimbizi kwa shughuli za kuzalisha kipato umelazimika kupunguzwa, na kuwa na athari mbaya kwenye juhudi za kuwafanya wakimbizi wasitegemee misaada. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,  UNHCR pamoja na maafisa wakuu wa Uganda wametembelea wadau muhimu ikiwa ni pamoja na Serikali za Denmark, Uholanzi, na Ubelgiji pamoja na taasisi za Muungano wa Ulaya (EU), ili kuonesha athari kubwa za upungufu wa fedha, na kutetea kuongeza kwa rasilimali. UNHCR ilisisitiza umuhimu wa msaada wa wafadhili katika kupunguza shida za wakimbizi na jamii zinazowahifadhi.  

Uganda ina idadi kubwa zaidi ya wakimbizi na waomba hifadhi barani Afrika, ikiwa na karibu watu milioni 1.7 hasa kutoka Sudan Kusini na DRC, lakini ilikuwa kati ya mipango 13  ya  UNHCR iliyopungukiwa zaidi kifedha duniani mwaka 2023. 

Ukarimu wa Uganda

Kwa miongo kadhaa, Uganda imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia wakimbizi na imekuwa ishara ya utulivu katika eneo hili, kwa kukumbatia sera za maendeleo ambazo ni mfano wa  Mkataba wa Wakimbizi Duniani, unayoruhusu wakimbizi kuwa na ardhi na uhuru wa kusafiri na kuishi mijini mradi waweze kujitegemea. 

Ikiwa sera hizo zitapoteza mwelekeo kutokana na upungufu wa fedha, "tunaweza kuona watu wakihama kutoka Uganda wakitafuta namna ya kuishi."

Mwezi Mei, wakimbizi walianza kuondoka kwenda nchi jirani wakidai ukosefu wa msaada na kupunguzwa kwa mgao wa chakula. Ikiwa hakuna hatua itakayochukuliwa, mafanikio ya maendeleo na uwezo wa taasisi utadhoofika na kuishi kwa amani na jamii zinazowahifadhi kutatatizwa. Msaada zaidi wa kimataifa unahitajika ili kusaidia ahadi ya Uganda ya kulinda wakimbizi.