Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchumi wa dunia umeboreka kidogo ingawa tahadhari yahitajika: UN Ripoti

Uchumi wa dunia unatarajia kukua kwa nguvu zaidi, wachumi wa Umoja wa Mataifa wanatabiri.
© Unsplash/Omid Armin
Uchumi wa dunia unatarajia kukua kwa nguvu zaidi, wachumi wa Umoja wa Mataifa wanatabiri.

Uchumi wa dunia umeboreka kidogo ingawa tahadhari yahitajika: UN Ripoti

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya katikati ya mwaka ya hali na mtazamo wa uchumi wa Dunia kwa mwaka 2024 iliyotolewa leo inaonyesha matarajio ya kiuchumi duniani yameboreka tangu utabiri uliotolewa Januari 2024, lakini mtazamo ni wa matumaini yanayohitaji tahadhari.

Ripoti hiyo iliyotolewa na Idara ya masuala ya kiuchumi na kijamii ya Umoja wa Mataifa DESA imesema” Kuendelea kwa viwango vya juu vya riba, matatizo ya madeni, na hatari za kijiografia na kisiasa vihatarisha ukuaji thabiti na endelevu wa uchumi.”

Imeongeza kuwa “Pia mishtuko ya mabadiliko ya tabianchi inayozidi kuwa mibaya inaleta changamoto zaidi kwa mtazamo wa uchumi wa dunia, na kutishia miongo kadhaa ya mafanikio ya maendeleo, hasa kwa nchi zinazoendelea na za visiwa vidogo vinavyoendelea.”

Ripoti hiyo pia inajadili jinsi mahitaji ya madini muhimu yalivyokua kwa kasi, wakati upelekaji wa teknolojia zinazotoa hewa ukaa kidogo nazo zikiongezeka kwa kasi.

Ripoti imesisitiza kuwa sekta muhimu ya madini inatoa fursa mpya kwa nchi nyingi zinazoendelea, lakini usimamizi madhubuti wa rasilimali za madini unasalia kuwa muhimu ili kufikia matokeo chanya kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu na kuepuka yale mabaya.

Sekta ya kilimo Pakistan inahaha kutokan na ukulima mdogo
Courtesy: Lok Sujag Pakistan
Sekta ya kilimo Pakistan inahaha kutokan na ukulima mdogo

Ukuaji wa uchumi wa dunia ni asilimia 2.7

Wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Mkurugenzi wa Uchambuzi wa Uchumi na Kitengo cha Sera katika Idara ya Uchumi na Masuala ya Kijamii cha Umoja wa Mayaifa DESA, Shantanu Mukherjee, amesema, "utabiri wetu ni wa matumaini yaliyolindwa, lakini kwa tahadhari muhimu."

Mukherjee ameeleza kuwa kwa mwaka 2024, "utabiri wa ukuaji wa dunia sasa unakadiriwa kuwa asilimia 2.7, ambayo ni juu kutoka asilimia 2.4 tuliyokuwa tukiitarajia Januari, na kwa 2025 tunatarajia asilimia 2.8, pia juu kidogo kutoka kwa kile tulichokuwa tukifikiria awali,” na pia amebainisha kwamba mabadiliko haya “kwa kweli yanatokana na utendaji bora kuliko uliotarajiwa katika baadhi ya mataifa makubwa yaliyoendelea na yanayoibukia kiuchumi.”

Wafanyakazi wanatekeleza jukumu lao katika kiwanda cha uzalishaji nchini Ethiopia.
ILO Photo/Marcel Crozet
Wafanyakazi wanatekeleza jukumu lao katika kiwanda cha uzalishaji nchini Ethiopia.

Taswira katika nchi zinazoendelea

Kwa upande mwingine, amesema, "mtazamo wa nchi nyingi zinazoendelea sio mzuri, na matarajio ya ukuaji uchumi katika 2024 na 2025 yanabaki kuwa chini ya wastani wa kabla ya janga la coronavirus">COVID-19."

Muhimu zaidi, Mukherjee ameongeza kuwa kwa Afŕika na nchi zenye maendeleo duni LDCs, "matarajio yanarekebishwa kushuka chini hadi kufikia takriban asilimia 3.3 ya ukuaji kwa mwaka huu 2024."

Afisa huyo wa DESA amewaambia waandishi wa habari mjini New York kwamba ripoti hiyo mpya inajumuisha nyongeza ya madini.

Amesema, "Tunachunguza, masuala mawili yanayohusiana ambayo tunafikiri ni muhimu. La kwanza ni jinsi ya kuhimiza uzalishaji na upatikanaji wa madini muhimu, kwa kiwango na kasi inayohitajika kwa mabadiliko ya nishati. Na la pili ni je, nchi hizo ambazo ni tajiri wa rasilimali hizi zinawezaje kutumia rasilimali hizi ili kugeuka kuwa mafanikio ya muda mrefu ya SDG? Swali la pili tunalofikiria, linahusiana na kikao cha ngazi ya juu HLPF mwaka huu, lakini pia ni muhimu sana kwa sababu wakati ukuaji kwa ujumla ni wa chini, hili ni eneo ambalo kuna uwezekano wa kuleta faida kubwa zaidi.”

Katika karakana ya Gibson Kawago ambako wanarejelea betri chakavu za kompyuta mpakato ili kuzalisha makasha ya betri yanayotumika kupatia nishati ya umeme.
Gibson Kawago
Katika karakana ya Gibson Kawago ambako wanarejelea betri chakavu za kompyuta mpakato ili kuzalisha makasha ya betri yanayotumika kupatia nishati ya umeme.

Uzalishaji wa madini ya lithium

Naye Mkuu wa DESA wa idara ya  Ufuatiliaji wa Kiuchumi Ulimwenguni katika Kitengo cha Uchambuzi wa Uchumi na Sera, Hamid Rashid, ameeleza kuwa uzalishaji wa lithiamu "umejikita katika nchi mbili, Australia na Chile, wakati usindikaji umejikita zaidi nchini China."

Ripoti hiyo imesisitiza kwamba nchi zilizojaliwa kuwa na rasilimali muhimu za madini zitahitaji sera mahiri, pamoja na uwezo madhubuti wa utekelezaji ili kupata manufaa na kuepuka laana mpya ya rasilimali, kupambana na mtiririko haramu wa fedha na kuhakikisha usambazaji wa madini muhimu yanayohitajika kwa mabadiliko yanayojali mazingira.