Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchango wa EU waiwezesha WFP kutoa msaada wa kuokoa maisha Sudan

Malori 16 ya kubeba mizigo ya msaada wa kibinadamu yanavuka mpaka kutoka Tine (Chad) hadi Darfur Kaskazini. (Maktaba)
© WFP
Malori 16 ya kubeba mizigo ya msaada wa kibinadamu yanavuka mpaka kutoka Tine (Chad) hadi Darfur Kaskazini. (Maktaba)

Mchango wa EU waiwezesha WFP kutoa msaada wa kuokoa maisha Sudan

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa msaada wa Muungano wa Ulaya (EU), limeweza kutoa msaada wa dharura wa chakula kwa karibu watu milioni 6.4 nchini Sudan tangu mzozo huo kuzuka nchini Sudan zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Aidha takribani  watu 550,000 wamepokea pesa taslimu. 

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo Mei 08 mjini Port Sudan nchini Sudan na Nairobi, Kenya imefafanua kuwa hili limewezekana kwa kiasi kutokana na mchango wa Euro milioni 28 kutoka Operesheni za Misaada ya Kibinadamu ya Muungano wa Ulaya (ECHO) mwaka wa 2023. WFP pia ilitumia ufadhili huu kusaidia kutibu na kuzuia utapiamlo kwa watoto 260,000 na wanawake wajawazito au wanaonyonyesha.

"Katikati ya kuongezeka kwa migogoro na njaa inayoongezeka, ufadhili wa kutosha ni muhimu ili kukidhi mahitaji ya kibinadamu yanayoongezeka. Tunashukuru sana Muungano wa Ulaya kwa mchango wao, ambao ulitusaidia kuokoa maisha wakati wa mzozo huu,” amesema Eddie Rowe, Mkurugenzi na Mwakilishi wa WFP nchini Sudan.

Uwezekano wa janga

WFP imekuwa ikionya kuwa Sudan inaweza kuwa janga kubwa zaidi la njaa duniani wakati wa msimu ujao wa muwambo, unaoanza Mei na kudumu hadi Oktoba. Hivi sasa, wakati wa msimu wa mavuno, idadi ya watu milioni 17.7 tayari wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, wakati karibu watu milioni 5 wako hatua moja tu kutoka katika baa la njaa (IPC 4). Hali ya uhakika wa chakula inatarajiwa kuwa mbaya zaidi katika miezi ijayo kama hatua za haraka hazitachukuliwa kusaidia wale wanaokabiliwa na viwango vya juu vya njaa.

Mwaka huu 2024, EU imekusanya kiasi cha awali cha EUR milioni 117 kwa ajili ya msaada wa kibinadamu nchini Sudan, pamoja na EUR milioni 185 za ziada ili kukabiliana na athari za mgogoro katika nchi jirani. Kiasi hiki kipya cha fedha kinakuja baada ya ufadhili wa kibinadamu wa Kamisheni ya Ulaya kwa Sudan mnamo mwaka jana 2023, ambayo ilifikia EUR milioni 128. “Wakati WFP ikifanya kazi ya kupanua shughuli zake ili kuepusha hatari ya janga la kibinadamu, uungwaji mkono wa wadau kama vile EU - mmoja wa wadau wetu wakarimu nchini Sudan - bado ni muhimu kwa juhudi za WFP.” Amesema Eddie Rowe.