Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yapitisha azimio kutangaza Mei 25 kila mwaka siku ya kimataifa ya mpira wa miguu

Mipira inayotumika kuchezea mpira wa miguu au kandanda
OSCE
Mipira inayotumika kuchezea mpira wa miguu au kandanda

UN yapitisha azimio kutangaza Mei 25 kila mwaka siku ya kimataifa ya mpira wa miguu

Utamaduni na Elimu

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo Jumanne limepitisha azimio la kutangaza tarehe 25 mwezi Mei kila mwaka kuwa siku ya kimataifa ya mpira wa miguu au kandanda.

Msemaji wa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Monica Grayley akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani amesema rasimu ya azimio hilo ilizingatiwa chini ya Ajenda namba 11 “Michezo kwa Maendeleo na Amani: kujenga dunia yenye amani na bora kupitia maadili ya Olimpiki.” 

Nchi zaidi ya 70 kati ya 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa walifadhili azimio hilo, kwa kutambua jinsi mpira wa miguu umeenea duniani na athari zake Chanya kwenye nyanja mbali mbali za maisha ikiwemo biashara, amani na diplomasia, na nguvu ya michezo katika suala la ushirikiano.

Kutoka Afrika Mashariki nchi zilizofadhili azimio hilo ni Burundi, Kenya, Tanzania na Uganda.

Mali (13) na Dieumerci Mbokani  wa timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kwenye mafunzo ya haki za mtoto kupitia soka.
© UNICEF/UN0658457/Josue Mulala
Mali (13) na Dieumerci Mbokani wa timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kwenye mafunzo ya haki za mtoto kupitia soka.

Azimio hilo namba 78/L.56,pia linakabirisha Mpango wa Mpira wa Miguu katika kusongesha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, mpango ambao ni jukwaa la kushirikisha na kuchechemua SDGs au Ajenda 2030.

Halikadhalika linapongeza nchi ambazo zimeandaa au zitaandaa mashindano ya kimataifa ya mchezo wa mpira wa miguu na linazihamasisha kuhakikisha mashindano hayo yanakuwa na mchango kwenye kusongesha amani duniani na haki. 

Vile vile linazingatia nafasi ya michezo ikiwemo ya watu wenye ulemavu katika kusongesha amani na maendeleo, kuheshimu haki za binadamu na kutokomeza ubaguzi wa rangi, kuimarisha usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana.

Mwaka 2013, Baraza Kuu lilitangaza tarehe 6 ya mwezi Aprili kila mwaka kuwa siku ya kimataifa ya Michezo na Amani.