Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko Kenya,  manusura wapaza sauti, UN yataka mnepo upatiwe kipaumbele

Watoto wanaoishi Kiambiu ambao waliathiriwa na mafuriko wakifunga foleni kwenye shule ya Dr Livingstone kupokea mlo wa mchana.
UN News/Thelma Mwadzaya
Watoto wanaoishi Kiambiu ambao waliathiriwa na mafuriko wakifunga foleni kwenye shule ya Dr Livingstone kupokea mlo wa mchana.

Mafuriko Kenya,  manusura wapaza sauti, UN yataka mnepo upatiwe kipaumbele

Msaada wa Kibinadamu

Nchini Kenya manusura wa mafuriko yanayoendelea kukumba taifa hilo la Afrika Mashariki wameendelea kupatiwa misaada kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa huku baadhi yao akiwemo mama aliyejifungua mtoto wake wiki moja iliyopita akisimulia hali ilivyokuwa na hivi sasa nini amesaidiwa.

Nancy Muranditsi anasema mambo ni magumu kwani hana chakula, ajira na amelazimika kuhamia kwenye nyumba aliyoko sasa kwasababu ya mafuriko. Wahisani walimpatia vitanda na bidhaa za matumizi mengine na anasimulia kwamba,“hii nyumba ninayoishi inavuja.Tumelazimika kuondoa godoro kwani lililowa maji.Pale ukutani pana shimo na linaingiza maji ya mvua.Nilipojifungua sikuwa na kitu.Hawa wahisani wa shirika la Tushinde ndio walionisaidia na chakula na pia kunilipia baada ya kujifungua hospitalini.”

Nancy Muranditsi, Mzazi akiwa na mwanawe mchanga anayeishi Kiambiu.
UN News/Thelma Mwadzaya
Nancy Muranditsi, Mzazi akiwa na mwanawe mchanga anayeishi Kiambiu.

Mitaa ya mabanda imetwama kwenye maji

Maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni ya mitaa ya mabanda kwenye mji mkuu, Nairobi.Daraja la mto Nairobi, ndilo linalounganisha mtaa wa Yerusalem na ule wa mabanda wa Kiambiu nalo limeharibiwa na maji ya mvua.Mafundi wanajitahidi kufanya ukarabati ili wakaazi waweze kuvuka kwa urahisi na kusalia salama.

Anne Ochieng ni mkazi wa Kiambiu na mhudumu wa jamii wa kujitolea na anabainisha kuwa usalama wa wanawake na watoto uko hatarini kwani,“lile daraja linalounganisha Kiambiu na kituo cha Stage 23 huko Yerusalem,lilisombwa na maji. Mimi mwenyewe nafanya kazi upande ule mwengine.Wakati nahitaji kwenda kazini lazima nizunguke sana na kuchelewa.Ukitoka kazini kuchelewa pia inakuwa tatizo kwani utachelewa nyumbani na sehemu hiyo sio salama.”

Mvua ya msimu wa masika ilianza mwezi wa Machi na maji yamejaa kwenye mto Nairobi. Kingo za mto zimemomonyoka na wakaazi wako hatarini kama anavyoelezea Elizabeth Atieno Aluoch, kiongozi wa wanawake eneo la Eastleigh Kusini kuwa,“Hili daraja limeleta shida tangu liharibike.Kina mama hawawezi kwenda sokoni nao watoto pia hawawezi kwenda shule kwani wanahofia usalama wao.”

Nyumba za udongo na maboksi zinazovuja

Mtaa huu wa Kiambiu uko upande wa pili wa daraja na nyumba zimejengwa kwa udongo, maboksi, magunia na hata mabati.Kimsingi zinavuja na wakaazi wanalala kwenye mazingira yaliyotota. Nancy Muranditsi ni mkaazi wa Kiambiu na mama wa watoto 5. Watoto wake wakubwa wanne wanashinda kwenye shule ya Dkt. Livingstone iliyoko upande wa pili wa darajani mtaani Jerusalem ambako pia ni kituo cha kugawa chakula.Chakula anachopakua ni kwa hisani ya wasamaria wema wanaopatia wanawake na watoto kwenye kituo cha Dkt.  Livingstone.

Kituo cha kucheza na kupokea mlo mmoja

Watoto hawa ni wakaazi wa mtaa wa Kiambiu na wanakutana kwenye kituo hiki ambacho ni shule ya msingi kwa ajili ya kupata mlo wa siku na kucheza. Mlo unatolewa na shirika la kiraia la Tushinde ambalo Mercy Mugo ni mratibu wake na wakiwa mtaani wanaona kuwa,“Wengi tunaokutana nao hawana pa kuishi.Wengi walikuwa wanaishi pembezoni ya mto na ikalazimika kuwaondoa na kuwahamishia maeneo ya juu kwani maji ya mvua yalijaa pomoni.Tumegawa pia vitanda kwa familia 44.Vyengine vinaendelea kuundwa.Kwa sasa idadi ya wanaopokea msaada imeongezeka kwani hatutaki kuacha mtoto yoyote nje pale anapoandamana na mwenzake aliye kwenye programu zetu.Tunawahudumia wote.” 

Daraja linalounganisha mtaa wa Jerusalem na mtaa wa mabanda wa  Kiambiu.
UN News/Thelma Mwadzaya
Daraja linalounganisha mtaa wa Jerusalem na mtaa wa mabanda wa Kiambiu.

Tujikite  kwenye kuhimili madhara ya tabianchi – UN Kenya

Ni mashirika kama haya yanayofanya Kazi na wadau wengine kupambana na athari za mafuriko. Kwa upande wake Umoja wa Mataifa umechangia vifaa na msaada wa dharura kwa wahanga wa mafuriko. Dkt. Stephen Jackson ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya na anaelezea kuwa mchango wao umeleta tija na ,”baadhi ya misaada ambayo tumekuwa tukigawa ni hema kwa waliopoteza makaazi yao, chakula, hela , dawa, vyandarua vya mbu… ni bidhaa za aina tofauti ambazo Umoja wa mataifa na washirika tumefanikisha…. Kiasi ya watu laki moja ishirini na tano wamefikiwa. Tunajua kuwa Mvua bado iko njiani kwahiyo mambo yatakuwa magumu Kabla ya afueni kupatikana.”

Umoja wa mataifa kwa ushirikiano na wadau kama shirika la msalaba mwekundu wanaofanya kazi kwa karibu na serikali ya Kenya uko mstari wa mbele kuokoa maisha ya wakenya.Kitisho kipya kimezuka nacho ni mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza yanayosambazwa na maji kama vile kipindupindu na malaria.

Dkt. Stephen Jackson, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya akizungumza na Thelma Mwadzaya kuhusu mchango wa UN wa msaada wa walioathiriwa na mafuriko.
UN News
Dkt. Stephen Jackson, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya akizungumza na Thelma Mwadzaya kuhusu mchango wa UN wa msaada wa walioathiriwa na mafuriko.

Dkt. Jackson anakiri kuwa kujihami ni muhimu ili kupunguza makali ya dhoruba za mabadiliko ya tabia nchi na ni kwa , “kujenga makinga maji na matenki ambayo yatahifadhi maji kwa ajili ya msimu wa kiangazi. Inahusu kukumbatia kilimo cha kumwagilia maji badala ya kutegemea mvua…. Kupanda mimea inayoweza kuhimili Mvua chache….kwa mazao na mimea ya mifugo. Kadhalika ni kuimarisha mifumo ya mabomba ya maji taka yanapotokea mafuriko na pia kuwawezesha wakaazi kuhimili makali. Tunahitaji kusukuma hoja ya kuhimili dhoruba.  

Imeandaliwa na Thelma Mwadzaya Idhaa ya Kiswahili ya UN, Kenya