Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji kutoka nchi za kipato cha chini na kati waongoza kwa kutuma fedha makwao- IOM

Familia moja yawasili Brazil baada ya kuvuka mpaka wa Venezuela kwa miguu.
© IOM/Gema Cortes
Familia moja yawasili Brazil baada ya kuvuka mpaka wa Venezuela kwa miguu.

Wahamiaji kutoka nchi za kipato cha chini na kati waongoza kwa kutuma fedha makwao- IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM leo limezindua Ripoti ya Dunia ya Uhamiaji 2024, ambayo inaonesha mabadiliko makubwa katika mifumo ya uhamiaji duniani, ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao na pia ongezeko la fedha zinazotumwa na wahamiaji kwenda nchi zao.

Mkurugenzi Mkuu wa IOM Amy Pope amezindua rasmi ripoti hiyo nchini Bangladesh, nchi ambayo iko mstari wa mbele katika changamoto za uhamiaji na kusema "Ripoti ya Uhamiaji Duniani ya 2024 inasaidia kuondoa utata wa uhamaji wa binadamu kupitia takwimu na uchambuzi unaozingatia ushahidi." 

Na zaidi ya yote ripoti hiyo inaweka bayana kuwa uhamiaji wa kimataifa unasalia kuwa kichocheo cha maendeleo ya binadamu, ukuaji wa kiuchumi ikidhihirishwa na ongezeko la zaidi ya asilimia 650 la utumaji wa fedha kimataifa unaofanywa na wahamiaji kuanzia mwaka 2000 hadi 2022 ikiwa ni ongezeko kutoka dola bilioni 128 hadi dola bilioni 831.

Ongezeko hilo limekuweko licha ya makadirio ya wachambuzi ya kwamba utumaji wa fedha utapungua kutokana na coronavirus">COVID-19.

Kati ya dola hizo bilioni 831, dola bilioni 647 zilitumwa na wahamiaji kuelekea nchi za kipato cha chini na cha kati. “Fedha hizi zinachangia kwa kiwango kikubwa katika pato la ndani la taifa na duniani kote, fedha hizo zimevuka kiwango cha uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni kwa nchi hizo,” imesema ripoti hiyo.

Ikimulika mambo makuu yaliyobainika, ripoti inaonesha kuwa wakati uhamiaji wa kimataifa unaendelea kuchochea maendeleo ya binadamu, bado kuna changamoto. 

Mathalani wahamiaji duniani wakikadiriwa kuwa milioni 281, idadi ya watu wanaofurushwa makwao kutokana na vita, ghasia, majanga ya asili na sababu nyinginezo inaendelea kuongezeka kwa kiwango cha juu na kufikia milioni 117, na hivyo kupatia umuhimu hoja ya kutatua janga la  ukimbizi.

Unaweza kupakua ripoti nzima hapa