Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Itakuwa ni janga kubwa Rafah, muafaka wa kusitisha mapigano usipofikiwa: Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

Itakuwa ni janga kubwa Rafah, muafaka wa kusitisha mapigano usipofikiwa: Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amerejea kusisitiza wito wake wa kusitishwa mapigano, kuachiliwa kwa mateka wote na kuepusha zahma kubwa ya kibinadamu kwa watu wa Gaza.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York Marekani amesema “Tuko katika wakati maamuzi kwa ajili ya watu wa Palestina na Israeli na kwa hatima ya Ukanda mzima. Makubaliano kati ya Serikali ya Israel na uongozi wa Hamas ni muhimu kukomesha mateso yasiyovumilika ya Wapalestina huko Gaza na ya mateka na familia zao. Itakuwa jambo la kusikitisha ikiwa wiki nzima ya harakati za kidiplomasia kwa ajili ya amani huko Gaza, hazitazaa matunda ya usitishaji wa mapigano, kuachiliwa kwa mateka na mashambulizi makubwa huko Rafah.”

Tweet URL

Onyesheni ujasiri wa kisiasa

Guterres amerejea ombi lake kwa pande zote mbili kuonyesha ujasiri wa kisiasa na kujitahidi kufikia makubaliano sasa ili kukomesha umwagaji damu, kuwakomboa mateka na kusaidia kuleta utulivu eneo ambalo bado liko katika hatari yajanga kubwa la kibinadamu.

Amesisitiza kuwa “Hii ni fursa muhimu kwa Ukanda mzima na Dunia kwa ujumla ambayo dunia haiwezi kuipoteza,”  hata hivyo ameonya kwamba mambo bado yanakwenda kombo. 

Amesema “Ninasikitishwa na kutiwa hofu na kurejea kwa mashambulizi ya vikosi vya jeshi la Israel Rafah. Kufungwa kwa vivuko vya Rafah na Karem Shalom kunaongeza zahma kwahali ya kibinadamu ambayo tayari ni mbayá. Ni lazima vifunguliwe mara moja.”

Ameitaka serikali ya Israel kukomesha mara moja mashambulizi zaidi na kujihusisha kikamilifu katika majadiliano ya kiplomasia yanayoendelea.

Mauaji tuliyoshuhudia yanatosha

Mkuu huyo wa Umoja wa mataifa amehoji baada yaWaisrael zaidi ya 1000 kuuawa  katika shambulio la kigaidi la Hamas la Oktoba 7 mwaka jana na zaidi ya Wapalestina 34,000 kuuawa Gaza, “Je tulichokishuhudia hakitoshi? Je Wapalestina hawajakumbwa na vifo vya kutosha na uharibifu? Tusifanye makosa kwani mashambulizi kamili Rafah yatakuwa zahma ya kibinadamu. Raia zaidi watauawa na kujeruhiwa, familia zaidi zitalazimika kukimbia kwa mara nyingine na kutokuwa na mahala popote salama pa kwenda kwa sababu hakuna mahala salama Gaza.”

Ameongeza kuwa wakati huohuo athari zake zitakwenda mbali , kwenye Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na kwenye Ukanda mzima.

Rafah ni kitovu cha operesheni za kibinadamu Gaza hivyo “ Kuishambulia Rafah kutaathiri zaidi juhudi zetu za msaada wa kibinadamu kwa hali mbayá iliyopo huku baa la njaa likinyemelea.”

Sheria za kimataifa lazima ziheshimiwe

Guterres amesisitiza kwamba sheria za kibinadamu za kimataifa ni lazima ziheshimiwe  nahazina mjadala, “raia wanapaswa kulindwa endapo wataamu kuondoka ama kusalia katika mji huo. Na sheria hizo za kibinadamu ni lazima ziheshimiwe hna pande zote.”

Katibu Mkuu ameikumbusha Israel juu ya wajibu wake wa wa kuwezesha ufikishaji wa misaada ya kibinadamu na wahudumu wa kibinadamu kuingia kote Gaza.

Ameendelea kusema kwamba hata marafiki wa karibu wa Israel wameonya kwamba uvamizi wa Rafah utakuwa ni makosa makubwa, janga la kisiasa na jinamizi la kibinadamu.

Amewataka wale wote wenye ushawishi kwa Israel kuingia kati kusitisha jinamizi linaloendelea huku akiikumbusha jumuiya ya kimataifa kwamba ina wajibu wa kutimiza katika kuchagiza usitishaji mapigano, kuachiliwa kwa mateka bila masharti, na kuingizwa kwa misaada ya kibinadamu.

Amezisistiza pande zote kuwa “Ni wakati wa kukumbatia fursa hii na kufikia muafaka .”