Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Namibia na mwelekeo wa kutokomeza maambukizi ya VVU na homa ya ini kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto

Namibia imepatiwa na WHO hati ya ngazi ya fedha na shaba kwa kuwa kwenye mwelekeo wa kutokomeza maambukizi ya VVU na Homa ya ini aina B mtawalia kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
WHO Africa
Namibia imepatiwa na WHO hati ya ngazi ya fedha na shaba kwa kuwa kwenye mwelekeo wa kutokomeza maambukizi ya VVU na Homa ya ini aina B mtawalia kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Namibia na mwelekeo wa kutokomeza maambukizi ya VVU na homa ya ini kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto

Afya

Namibia imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa katika mwelekeo wa kihistoria wa kutokomeza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi au VVU na Homa ya Ini aina ya B kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Taarifa iliyotolewa na na shirika la  Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika huko Windhoek, mji mkuu wa Namibia inasema taifa hilo linakuwa la kwanza pia kufikia hatua hiyo miongoni mwa nchi zilizokuwa na idadi kubwa ya maambukizi hayo.

Eneo la nchi za kusini na mashariki mwa Afrika linabeba zaidi ya nusu ya watu wanaoishi na VVU na bara la Afrika kwa ujumla lina theluthi mbili ya maambukizi mapya ya Homa ya Ini aina ya B, duniani kote.

WHO inasema Namibia ina zaidi ya watu 200,000 wanaoishi na VVU na idadi kubwa ya maambukizi hayo yanapata wanawake.

Maendeleo yamepatikana kwani tangu mwaka 2010, duniani kote watoto milioni 2.5 wameepuka maambukizi ya VVU kutoka kwa mama zao wakiwa tumboni na kati yao hao 28,000 wako Namibia.

Hatua ilizochukua Namibia zimefanikishwa na utashi wa kisiasa

“Huduma za upimaji wa VVU miongoni mwa wajawazito sasa zinapatikana karibu nchini kote Namibia na upatikanaji wa dawa umepunguza maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto kwa asilimia 70, katika kipindi cha miaka 20,” imesema taarifa hiyo.

Mwaka 2022, ni asilimia 4 tu ya watoto waliozaliwa na mama waliokuwa wanaishi na VVU ndio walioambukizwa virusi hivyo 

Takribani asilimia 80 ya watoto wachanga wanapata kwa wakati muafaka dozi ya chanjo ya Homa ya Ini aina ya B pale wanapozaliwa , moja ya sababu kuu ya mafanikio kuelekea kutokomeza maambukizi hayo.

Huduma za mama na mtoto na matibabu ni bure

Namibia imejumuisha pia huduma za wajawazito, afya ya uzazi na afya ya mtoto kwenye huduma ya msingi ya afya. Serikali imetenga fedha kwenye bajeti kwa ajili ya mipango ya kiafya kitaifa, ambapo huduma za afya zinapatikana, wananchi wanazimudu na ni bora na zaidi ya yote ni bure.

Kwa kuzingatia kigezo mahsusi cha WHO, Namibia imepatiwa hati ya ngazi ya FEDHA kwa maendeleo ya kupunguza maambukizi ya homa ya ini aina ya B na  hati ya ngazi ya SHABA kwa maendeleo yake katika kutokomeza maambukizi ya VVU.

Kauli ya Mkuu wa WHO Afrika

Akizungumzia hatua hii, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema hii ni hatua ya mafanikio makubwa kwa Namibia kwani imeonesha uwezekano wa kuokoa maisha kutokana na utashi wa kisiasa na utekelezaji wa dhati wa vipaumbele vya afya ya umma.

Amesema kwa juhudi za pamoja tunaweza kuchagiza maendeleo ya kufikia lengo la kutokomeza maambukizi ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa VVU, Homa ya Ini aina ya B na kaswende.

Mchakato wa kutoa hadhi kwenye kutokomeza magonjwa huongozwa na WHO kwa ushirikiano na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuhudumia watoto, UNICEF, la kutokomeza UKIMWI, UNAIDS na lile la afya ya uzazi, UNFPA.

Soma taarifa nzima hapa.