Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR inapambana kuwasaidia wakimbizi dhidi ya mafuriko Afrika Mashariki

Mafuriko ya hivi majuzi yaliyotokea kote nchini Kenya yamesababisha familia nyingi za wakimbizi kuhama makazi yao katika kambi za wakimbizi za Dadaab.
© UNHCR/Mohamed Maalim
Mafuriko ya hivi majuzi yaliyotokea kote nchini Kenya yamesababisha familia nyingi za wakimbizi kuhama makazi yao katika kambi za wakimbizi za Dadaab.

UNHCR inapambana kuwasaidia wakimbizi dhidi ya mafuriko Afrika Mashariki

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi, UNHCR, linapambana kuhakikisha linawasaidia wakimbizi katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa Afrika Mashariki dhidi ya madhila yanayosababishwa na mafuriko makubwa kutoka na mvua za El Niño zinazoendelea. 

Makala hii ambayo video zake zimekusanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR inaanzia Bujumbura Burundi kisha inakupeleka Kenya katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab.

Nyumba zilizoko Kajaga katika mji mkuu wa Burundi Bujumbura, ambako wakimbizi wa mijini pia wanaishi, zimefurika huku mto wa Rusizi ukivunja kingo zake kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.
© UNHCR/Bernard Ntwari
Nyumba zilizoko Kajaga katika mji mkuu wa Burundi Bujumbura, ambako wakimbizi wa mijini pia wanaishi, zimefurika huku mto wa Rusizi ukivunja kingo zake kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

Ni mitumbwi ikikatiza katika baadhi ya mitaa ya Bujumbura, katika ambazo kwa kawaida ni barabara za mitaa lakini sasa zimegeuka kuwa mikondo ya maji.

"Nilipohamia hapa mnamo 2020 hakukuwa na maji, magari yangeweza kufika nyumbani kwangu anaeleza Nyembo, mkimbizi wa vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, “lakini maji yalipoanza kuongezeka yalijaza nyumba, tulitoka kwanza, kisha tukarudi. Tuliporudi maji yalikuwa yamepungua, lakini yalianza kupanda tena. Kadiri miaka ilivyosonga, viwango vya maji viliendelea kuongezeka kila msimu. Mwaka huu viwango vya maji ni vya juu sana, ni janga. Sijui la kufanya, sina uwezo wa kukodisha nyumba nyingine ya kukaa."

Neziya Nsananikiye, mkimbizi wa ndani wa Burundi, kwa lugha ya Kirundi anasema kwamba hajawahi kuona mafuriko namna hii, maji hayajawahi kuwa juu hivi. Huu umekuwa mwaka mbaya.

Sasa video hii ya UNHCR inaonesha mtumbwi uliosheheni vifaa vya ndani kama magodoro, viti na mabegi. Kjaga Justin Ngoma naye mkimbizi wa ndani nchini Burundi, anahama mtaa, "mafuriko yamenilazimisha kuhama. Maji yamekuwa yakiongezeka hapa. Sisi ni familia ya watu kumi, na kuna watoto pia ambao wako shuleni. Mimi pia ni mwanafunzi. Mara nyingi tunachelewa darasani. Tulipohamia hapa, hatukuwahi kufikiria kwamba maji yanaweza kufikia kiwango hiki. Lakini yameendelea kuongezeka, hivyo tukaamua kuhama.”

Wafanyikazi wa UNHCR wakihamisha vifaa muhimu vya msaada vitavyogawiwa kwa familia za wakimbizi waliokimbia makazi yao kutokana na mafuriko katika kambi za Dadaab.
© UNHCR/Mohamed Maalim
Wafanyikazi wa UNHCR wakihamisha vifaa muhimu vya msaada vitavyogawiwa kwa familia za wakimbizi waliokimbia makazi yao kutokana na mafuriko katika kambi za Dadaab.

Na sasa tuelekee katika kambi ya wakimbizi Dadaab nchini Kenya. Huko nako hali ni tete, mvua zimesababisha mafuriko kambini. UNHCR inasema takribani watu 20,000 katika kambi hiyo ya Dadaab wamepoteza makazi yao kutokana na kuongezeka kwa viwango vya maji -wengi wao wakiwa wale waliokimbia Somalia kutokana na ukame.

Korad Abdiwanhab, Mkimbizi kutoka Somalia anasema, "Maji yaliingia ndani ya nyumba kutoka pande zote mbili. Wimbi la kwanza lilikuwa hadi kiwango hiki." Hapo anaonesha kuwa maji kwa vyovyote yangefukika zaidi ya sentimita thelatini za sakafu ndani ya nyumba, “maji ya mafuriko yalipoingia nyumbani, nilimwamsha binti yangu mwenye ulemavu na watoto wengine. Nilijaribu kuwaokoa watoto kabla ya nyumba kuporomoka. Baada ya nyumba kuporomoka, tulikimbia kuelekea kwenye shule. Tuliingia ndani ya shule ambapo tulikaa kwa usiku kadhaa. Maji yamepungua lakini, hatuna pa kurudi. Hakuna makazi. Hakuna vyoo. Hakuna nyumbani."

Kote Afrika Mashariki ambako mafuriko yametokea na kuwaathiri wakimbizi kama Tanzania, Burundi, Kenya na Somalia, UNHCR inajitahidi kuwasaidia lakini rasilimali zaidi za wafadhili zitakuwa muhimu ili kuwapa watu usaidizi wa haraka wa kuokoa maisha pamoja na msaada wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Muhumed Shafat mwenye umri wa miaka 70 na familia yake wanatafuta hifadhi katika moja ya shule katika kambi za wakimbizi za Dadaab, baada ya makazi yao kuharibiwa na mafuriko.
© UNHCR/Mohamed Maalim
Muhumed Shafat mwenye umri wa miaka 70 na familia yake wanatafuta hifadhi katika moja ya shule katika kambi za wakimbizi za Dadaab, baada ya makazi yao kuharibiwa na mafuriko.

Mwezi Aprili mwaka huu 2024, UNHCR ilizindua Mfuko wake wa kwanza kabisa wa Kuhimili Tabianchi, ambao unalenga kuchangisha dola milioni 100 kusaidia wakimbizi, jamii zinazowahifadhi na nchi zao za asili zilizoathiriwa zaidi na dharura ya tabianchi, na kukuza ushiriki wa wakimbizi katika hatua za kitaifa na za mitaa.