Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia El Fasher, Sudan zikiongezeka mashirika ya Umoja wa Mataifa yaonya

Watoto wakitembea kuelekea kituo cha wakimbizi wa ndani huko El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan (Maktaba)
© UNICEF/Shehzad Noorani
Watoto wakitembea kuelekea kituo cha wakimbizi wa ndani huko El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan (Maktaba)

Ghasia El Fasher, Sudan zikiongezeka mashirika ya Umoja wa Mataifa yaonya

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la Mpango wa Chakula Ulimwenguni (WFP), la kuhudumia watoto (UNICEF) na la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) yameonya kuhusu mstakabali wa maisha ya watu wa Sudan hasa kutokana na kuongezeka kwa ghasia katika eneo la El Fasher huko Darfur Kaskazini nchini Sudan.

WFP

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linaonya kwamba muda unayoyoma dhidi ya kuzuia baada la njaa huko Darfur, Sudan huku mapigano yanayozidi katika mji mkuu wa Darfur Kaskazini wa El Fasher yakizuia juhudi za kuwasilisha msaada muhimu wa chakula katika eneo hilo.

Katika taarifa yake iliyotolewa Mei 3 leo WFP imesem raia katika El Fasher na eneo pana la Darfur tayari wanakabiliwa na kiwango kikubwa cha njaa, lakini uwasilishaji wa msaada wa chakula umekuwa wa hapa kutokana na mapigano na vikwazo visivyoisha vya ukiritimba. Kuongezeka kwa ghasia za hivi karibuni karibu na El Fasher kumesitisha misafara ya misaada kutoka kwenye kivuko cha mpaka cha Tine, Chad  ukanda wa kibinadamu uliofunguliwa hivi majuzi ambao unapitia mji mkuu wa Darfur Kaskazini.

Wakati huo huo, vikwazo kutoka kwa mamlaka katika Bandari ya Sudan vinazuia WFP kusafirisha msaada kupitia Adre, ukanda mwingine pekee unaoweza kuvuka mpaka kutoka Chad. Njia hii inaweza kutumika Darfur Magharibi na maeneo mengine katika Darfur ya Kati, Kusini na Mashariki. Vikwazo hivi vya ufikiaji vinahatarisha mipango ya WFP ya kutoa msaada muhimu kwa zaidi ya watu 700,000 kabla ya msimu wa mvua wakati barabara nyingi katika Darfur hazipitiki.

UNICEF

Ongezeko la mapigano katika jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan limesababisha vifo vya watoto katika wiki za hivi karibuni. Lakini tishio la shambulio la kijeshi dhidi ya El Fasher, jiji linalohifadhi takriban watu 500,000 waliohamishwa na ghasia mahali pengine nchini, linahatarisha kuongezeka kwa janga, kuhatarisha maisha na ustawi wa watoto 750,000 huko El Fasher, na pengine uwezekano wa mamilioni ya watu wengine zaidi.

 “Tunatoa wito kwa wahusika katika mzozo huo kujiondoa haraka kutoka kwa makabiliano hayo hatari.” Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEFCatherine Russel ameeleza kupitia taarifa yake iliyotolewa jana Mei 2 jini New York, Marekani.  

Takriban watu 43, wakiwemo watoto na wanawake, wameuawa tangu kuongezeka kwa mapigano ndani na karibu na El Fasher zaidi ya wiki mbili zilizopita. Mashambulizi yanayoendelea, ikiwa ni pamoja na matumizi ya silaha za milipuko katika vitongoji vya makazi, ni hatari sana kwa watoto, na yatasababisha tu watoto wengi kuhama, kujeruhiwa na kuuawa. Takwimu za UNICEF zimebainisha.

UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) inaendelea kutoa wito kwa usalama wa raia, upatikanaji salama kwa mashirika ya misaada ili msaada na vifaa viweze kutolewa na zaidi ya yote, kukomesha uhasama. Washirika wa kibinadamu pia wanahitaji usaidizi zaidi ili kuongeza uwezo wao wa kuchukua hatua.

UNHCR pamoja na wadau wa Umoja wa Mataifa, inasalia nchini Sudan kusaidia watu wake na inaendelea kufanya kazi popote inapopata ufikiaji salama. “Katika Khartoum, Darfur na Jimbo la Kordofan, tunashirikiana na wadau wa ndani, viongozi wa wakimbizi na mitandao ya ulinzi ya kijamii ili kufuatilia mahitaji na kusaidia pale tunapoweza. Pia tupo katika majimbo ya Bahari ya Shamu, Kaskazini, White Nile, Blue Nile, Gedaref na Kassala, ambayo huhifadhi mamia ya maelfu ya wakimbizi ambao tayari wako nchini kabla ya vita.”

Huku hali ya kibinadamu ikiendelea kuwa mbaya zaidi, rasilimali za kifedha zinazohitajika kukidhi mahitaji kote Sudan na katika nchi jirani hazitoshelezi. Hadi sasa, ni asilimia 10 tu ya dola bilioni 2.6 zinazohitajika kufikia zaidi ya watu milioni 18 kwa msaada wa kuokoa maisha ndani ya Sudan zimepokelewa, na ni asilimia 8 tu zimefikiwa za mahitaji ya kifedha ya  dola bilioni 1.4 yaliyoainishwa katika Mpango wa Kukabiliana na Wakimbizi wa Kikanda wa 2024 kwa Sudan.