Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rafah ikilengwa itakuwa ni mauaji - OCHA

Watoto wadogo wamesimama nje ya makazi yao ya muda huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza. (Maktaba)
© WHO
Watoto wadogo wamesimama nje ya makazi yao ya muda huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza. (Maktaba)

Rafah ikilengwa itakuwa ni mauaji - OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Operesheni za jeshi la Israel huko Rafah, “zinaweza kusababisha mauaji na kudumaza kazi ya kuokoa maisha zinazofanyika Gaza, imesema hii lwo ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA.

Jens Laerke ambaye ni msemaji wa OCHA amewaambia waandishi wa habari kuwa operesheni zozote za kijeshi ardhini zitamaanisha machungu zaidi na vifo kwa wapalestina milioni 1.2 ambao kwa sasa wamefurushwa makwao kwenye mji wa Rafah na viunga vyake huko Kusini mwa Gaza.

Akipigia ‘chepuo’ hofu hiyo ya OCHA, Daktari Rik Peeperkorn, Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya, WHO, kwenye eneo linalokaliwa la wapalestina, oPt, amesema mipango ya kutatua jambo kwa muda mfupi imeandaliwa iwapo uvamizi kamilifu wa kijeshi utafanyika, lakini haitatosha kuzuia janga la kibinadamu Gaza kuzidi kuwa baya.

Mipango ya dharura

“Mipango ya kuendana na wakati ni mipando ya dharura. Haitazuia kinachotarajiwa kuwa janga kubwa, ongezeko la vifo vya watu na watoto vitokanavyo na operesheni za kijeshi,” amesisitiza Daktari PeeperKorn.

“Mfumo wa afya hautaweza kuhimili kiwango cha majeruhi kitakachosababishwa na uvamizi huo.”

Kuzidi kuzorota kwa usalama kutakwamisha pia harakati za kusafirisha vyakula, maji na vifaa vya matibabu ndani ya Gaza kupitia maeneo yaliyowekwa ya kuvuka mipakani, amesema afisa huyo wa WHO.

Baada ya takribani miezi saba ya mashambulizi makubwa ya kijeshi yanayofanywa na Israel kufuatia mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ni hospitali 12 tu kati ya 36 huko Gaza na na vituo vya afya ya msingi 22 kati ya 88 kwenye eneo hilo linalozingirwa, ndio vinafanya kazi, kwa mujibu wa WHO.

Huduma ya kusafisha figo mashakani

Huduma ya wagonjwa kusafishwa figo kwenye hospitali ya Najjar huko Rafah ambayo ndio pekee kwa mamia ya wagonjwa nayo iko mashakani, amesema Daktari Ahmed Dahir, kiongozi wa WHO huko Gaza.

“Tutazidi kuona madhara zaidi katika miaka ijayo, amesema Daktari Pepperkorn akisema kuwa watoto 30 wameripotiwa kufa kwa sababu ya magonjwa yanayohusiana na utapiamlo.

WHO na wadau wake sasa wamechukua hatua za dharura za kuweka hospitali ya muda huko Al Mawasi mkoani Rafah.

Bohari kubwa nayo imewekwa kwenye mji wa kati wa Deir Al Balah.

Vifaa vingine vya misaada vimewekwa hospitali ya Al-Aqsa huko Deir Al Balah na hospitali ya European Gaza karibu na mji wa Khan Younis huko kusini mwa Gaza.

Kituo cha tiba cha Khan Younis nacho kinakarabatiwa ili kiweze kutoa huduma za msingi za afya, wakati huu ambapo usafishaji na ukaguzi wa vifaa muhimu umekamilika.

Vyumba 9 kati ya 10 vya upasuaji vinafanya kazi na timu za huduma za dharura za afya zinajiandaa kufanya kazi sambamba na wafanyakazi wa kitaifa, imesema WHO.

Kujipanga kuweka maeneo muhimu

WHO na wadau wake wanatenga pia vituo vya afya ya msingi na tiba huko Khan Youni na maeneo ya kati, pamoja na kuweka vifaa vya matibabu ili kuwezesha vituo hivyo kubaini na kutibu magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, halikadhalika kutibu majeraha.

Huko Kaskazini, WHO inasaidia kuimarisha huduma kwenye hospitali za Al-Ahli, Kamal Adwan na Al-Awda ambako vifaa vya matibabu na wahudumu wameandaliwa.

“Mipango inaandaliwa pia kusaidia kurejesha hospitali rafiki kwa wagonjwa, kwa kujikita zaidi kwenye huduma kwa watoto, na kupanua vituo vya afya ya msingi na matibabu,” imeripoti WHO.