Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanahabari wana jukumu muhimu la kuelimisha juu ya mabadiliko ya tabianchi: UN

Baadhi yao wamepumzika baada ya siku yenye shughuli nyingi kwenye Mkutano wa Viongozi wa Dunia.
UN News/Laura Quinones
Baadhi yao wamepumzika baada ya siku yenye shughuli nyingi kwenye Mkutano wa Viongozi wa Dunia.

Wanahabari wana jukumu muhimu la kuelimisha juu ya mabadiliko ya tabianchi: UN

Tabianchi na mazingira

Leo ni siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani mwaka huu ikibeba maudhui “Vyombo vya Habari kwa ajili ya Sayari: Uandishi wa habari katika kukabiliana na mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi”  kwani Umoja wa Mataifa unasema mchango wa wanahabari na vyombo vya habari ni kiini katika kuhabarisha na kuelimisha umma kuhusu changamoto hiyo ya tabianchi. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akisistiza kuhusu maudhui ya maadhimisho ya mwaka huu katika ujumbe wake amesema dunia hivi sasa inapitia dhadhura ya mazingira ambayo haijawahi kushuhudiwa na inatishia kizazi hiki na vijavyo hivyo watu wanahitaji kujua kuhusu janga hili akiongeza kuwa “Waandishi wa habari na wafanyakzi wa vyombo vya habari wana jukumu muhimu la kuwahabarisha na kuwaelimisha. Vyombo vya habari vya kijamii, kitaifa na kimataifa vinaweza kutangaza habari kuhusu janga la mabadiliko ya tabianchi, kupotza kwa bayoanuwai na haki ya mazingira.”

Zaidi ya hapo amesema wanatoa ushahidi kuhusu uharibifu wa mazingira ambao unaweza kusaidia kuwawajibisha wahusika na ndio maana haishangazi kwamba baadhi ya watu wenye nguvu, makampuni na taasisi wanafanya kila wawezalo kuwazuia waandishi wa habari za mazingira kufanya kazi yao.

Bila ukweli, hatuwezi kupigana na habari potofu na za uongo, bila uwajibikaji, hatutakuwa na sera madhubuti na bila uhuru wa vyombo vya habari, hatutakuwa na uhuru wowote.

Guterres ameonya kwamba hivi sasa Uhuru wa vyombo vya habari umebinywa. Na uandishi wa habari za mazingira ni taaluma inayozidi kuwa hatari. Makumi ya waandishi wa habari wanaoripoti uchimbaji haramu wa madini, ukataji miti, ujangili na masuala mengine ya mazingira wameuawa katika miongo ya hivi karibuni nakatika idadi kubwa ya kesi zao, hakuna mtu ambaye amewajibishwa.

Akiunga mkono kauli hiyo mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO Audrey Azoulay amesema, "wakati ubinadamu unakabiliana na hatari hii iliyopo, lazima tukumbuke, katika Siku hii ya Dunia, kwamba changamoto ya mabadiliko ya tabianchi pia ni changamoto ya uandishi wa habari na wanahabari. Hakuna hatua madhubuti ya hali ya hewa inayowezekana kufikiwa bila fursa huru ya kupata habari za kisayansi na za kuaminika. Ndiyo maana maudhui ya mwaka huu yanaangazia uhusiano muhimu kati ya kulinda uhuru wa kujieleza ambayo ni manufaa ya umma duniani na kulinda sayari yetu.”

Kwa mujibu wa ripoti ya UNESCO ya hivi karibuni kabisa katika miaka 15 iliyopita kumekuwa na mashambulizi 750 dhidi ya wanahabari na vyombo vya habari vinavyoripoti masuala ya mazingira na mashambulizi hayo yanaongezeka.

Na zaidi ya hayo “Asilimia 70 ya waandishi wa habari za mazingira wamekuwa waathiriwa wa mashambulizi, vitisho au shinikizo kwa sababu ya kazi yao, na waandishi wa habari za mazingira 44 wameuawa katika miaka hiyo 15 iliyopita. Hivyo Bi. Azoulay amesisitiza kuwa upatikanaji wa habari za kuaminika ni muhimu zaidi katika mwaka huu wa chaguzi kuu ambapo wananchi wapatao bilioni 2.6 kutoka mataifa mbalimbali wanatarajiwa kushiriki haki yao ya msingi ya kupiga kura.

Hivyo Umoja wa Mataifa unasisitiza kwamba, "Bila ukweli, hatuwezi kupigana na habari potofu na za uongo, bila uwajibikaji, hatutakuwa na sera madhubuti na bila uhuru wa vyombo vya habari, hatutakuwa na uhuru wowote," hivyo uhuru wa vyombo vya habari sio chaguo, bali ni lazima.

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametoa wito kwa serikali, sekta binafsi na mashirika ya kiraia kuungana na Umoja wa Mataifa katika kuthibitisha dhamira ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari na haki za wanahabari na wanataaluma wa vyombo vya habari duniani kote.