Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 10,000 wamezikwa katika vifusi Gaza: UN

Mazingira chafu na yasiyo salama katika makazi na maeneo mengine inachangia moja kwa moja janga la kibinadamu huko Gaza.
UNICEF and UNDP PAPP/Abed Zagout
Mazingira chafu na yasiyo salama katika makazi na maeneo mengine inachangia moja kwa moja janga la kibinadamu huko Gaza.

Watu 10,000 wamezikwa katika vifusi Gaza: UN

Msaada wa Kibinadamu

Katika hatua inayotia wasiwasi Gaza , Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharira  OCHA imesema zaidi ya watu 10,000 wanaaminika kuzikwa chini ya vifusi.

Ofisi hiyo imeongeza kuwa vitongoji vyote vilisawazishwa, na kusababisha uharibifu wa maelfu ya majengo, huku kukiwa na mashambulizi makali na ya mara kwa mara ya Israel "katika sehemu nyingi za Ukanda wa Gaza kutokea angani, nchi kavu na baharini.”

Ofisi ya OCHA imeonyesha kuwa kufukua miili ya waliofunikwa chini ya kifunsi ni changamoto kubwa kutokana na ukosefu wa tingatinga, wachimbaji na wafanyakazi. 

Shirika hilo limesema "inaweza kuchukua hadi miaka mitatu kufukua miili yote kwa kutumia zana za zamani zinazopatikana" kwa ulinzi wa Raia wa Palestina, likielezea hofu yake kwamba kuongezeka kwa joto kutaongeza kasi ya kuharibika kwa miili hiyo, ambayo inaweza kuongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa.

Jinamizi lazima liishe

Katika wito wa kukomesha uhasama, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Catherine Russell, amesema "jinamizi kwa familia za Gaza lazima likomeshwe.”

Ameyasem hayo katika ujumbe mfupi wa video kwenye kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa X akieleza kwamba watoto wote walionaswa katika mji wa kusini wa Rafah ambao ni takriban 600,000 "wamejeruhiwa, ni wagonjwa, wanaugua utapiamlo, wameumizwa, au wanaishi na ulemavu."

Ameonya kwamba operesheni yoyote ya kijeshi inayoongezeka katika jiji hilo italeta maafa makubwa zaidi.

Kwa kuwa zaidi ya siku mia mbili zimepita tangu vita vikali vizuke Gaza, Mkurugenzi Mtendaji huyo amerejea wito wake wa kulinda wanawake na watoto, vifaa, huduma na misaada ya kibinadamu ambayo wanaitegemea.

Mabomu na makombora mazito

Kufuatia kuondoka kwa vikosi vya Israel mwezi uliopita kutoka mji wa kusini wa Khan Yunis, ujumbe wa timu ya Umoja wa Mataifa ya tathmini uliripoti Aprili 10 kwamba mitaa na maeneo ya umma yamejaa silaha ambazo hazikulipuka. 

Aidha, mabomu ya pauni elfu moja yalipatikana "yakitupwa kwenye makutano makubwa ya barabara na ndani ya shule."

Juhudi zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa zinaendelea kufanya maeneo hayo kuwa salama kwa wakazi wa Gaza kurejea Khan Yunis, ikiwa ni pamoja na kutathmini ya uharibifu wa vituo vya shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA na kuchora ramani ya maeneo hatarishi yenye makombora na risasi zisizolipuka.

UNMAS inaendesha kampeni za uhamasishaji kupitia mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa simu za rununu SMS, pamoja na vipeperushi, kwa takriban watu milioni 1.2 huko Gaza kama sehemu ya vifurushi vya misaada vinavyosambazwa na washirika wengine wa kibinadamu.

UNRWA inaripotiwa kuwa kuna wastani wa tani milioni 37 za uchafu katika eneo hilo, ambalo lina uwezekano wa kuwa na tani 800,000 za asbestosi na uchafuzi mwingine.

Idadi kubwa ya vifo

OCHA imeripoti kuwa Wapalestina 80 wameuawa na wengine 118 wamejeruhiwa na mlipuko wa  mabomu ya Israel kati ya Aprili 29 na Mei 1, ikinukuu mamlaka ya afya huko Gaza, na kufanya idadi ya vifo huko Gaza tangu Oktoba 7 mwaka jana kufikia si chini ya watu 34,560 raia wa Wapalestina, huku wengine 77,765 wakijeruhiwa.

Hii ni pamoja na uvamizi ambao ulifanyika Jumatatu wiki hii karibu saa sita na dakika ishiri ni na tano mchana ambapo wanawake wawili na wasichana wawili waliuawa na wengine kujeruhiwa wakati nyumba waliyokuwemo ilipogongwa.