Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi wa Gaza wako katika jakamoyo wakisubiri taarifa kuhusu wito wa kusitisha mapigano: UN

Kaskazini mwa Gaza iko kwenye magofu baada ya miezi kadhaa ya mashambulizi ya mabomu.
© WFP/Ali Jadallah
Kaskazini mwa Gaza iko kwenye magofu baada ya miezi kadhaa ya mashambulizi ya mabomu.

Wananchi wa Gaza wako katika jakamoyo wakisubiri taarifa kuhusu wito wa kusitisha mapigano: UN

Amani na Usalama

Wakati kukiwa na ongezeko la wito wa kimataifa kwa Israel kujizuia na mashambulizi zaidi Gaza na ripoti za leo za mashambulizi mengine mabaya zaidi ya usiku kucha, wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza kuhusu athari mbaya zinazoendelea za vita hiyo na haja ya kuhakikisha njia za kuaminika za usambazaji wa misaada kwa watu wanaohitaji kwa udi na uvumba zinapatikana. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula Duniani WFP kupitia mkurugenzi wake wa eneo linalokaliwa la Palestina Matthew Hollingworth, limesema "Theluthi moja ya familia zote zinazoishi hapa zina watoto wa umri wa chini ya miaka mitano, hao ni watoto wengi sana.” 

Akizungumza kutoka shule ya Deir Al Balah, inayoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA amesema watoto hawa wana mahitaji mengi “Wanachohitaji ni shule, maji safi na salama, utulivu zaidi,  na pia wanahitaji kurejea kwa maisha ya kawaida, "

Likiunga mkono wasiwasi huo shirika la UNRWA limegusia mashambulizi yanayoendelea likisema “kumekuwa na zaidi ya mashambulizi 360 kwenye vituo vyake tangu kuanza kwa vita. Mbali na makumi ya maelfu ya waathiriwa, miundombinu muhimu imeathiriwa pia, pamoja na kisima cha maji cha shirika hilo kilichoko katika jiji la Khan Younis.”

Na ili kukarabati chanzo hicho cha maji UNRWA inasema kunahitajika kuondoa tani za uchafu ikiwemo vilipuzi na vifaa vingie vya mabaki ya virta kama vilivyobainiwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya msaada wa kutegua mabomu UNMAS nav yote vinahitaji kuondolewa kwa usalama kipande kwa kipande,."

Kupata hifadhi shuleni

Shule ya UNRWA  ya Al Qastal iliyoko katikati mwa Ukanda wa Gaza sasa ni nyumbani kwa karibu familia 2,400 ambazo zimefurushwa na vita vya karibu miezi saba huko Gaza.

Bwana. Hollingworth  ameongeza kuwa "Watu wanatoka kote Ukanda wa Gaza, kuanzia mji wa Gaza wenyewe,mji jirani wa Khan Younis na kutoka katika vitongoji vyote tofauti ambako watu wameathiriwa kwa sababu ya vita,” 

Kauli yake inakuja huku kukiwa na ripoti ambazo hazijathibitishwa kwamba watoto wawili wamekufa katika mashambulizi ya Isarel ya usiku wa kuamkia leo kwenye nyumba moja huko Rafah, na wengine kuuawa wakati ghorofa wanamoishi lilipopigwa na kombora katika mji wa Gaza.

Wakati wasiwasi mkubwa ukiendelea kuhusu uwezekano wa uvamizi wa Israel katika mji wa Rafah ambao Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alionya Jumanne kwamba "Yatakuwa ni mashambulizi yasiyoweza kuvumilika" - afisa huyo wa WFP amebainisha kuwa mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa pamoja na washirika wengine wa kimataifa na wa ndani wamefanya kazi pamoja kwa mafanikio ili kutoa msaada wa kuokoa maisha hususani katika eneo la kaskazini.

Bomoabomoa Ukingo wa Magharibi

Katika hali inayohusiana na hiyo na ishara ya hali mbaya inayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu a masualam ya dharura, OCHA, imechapishatakwimu mpya kutoka Ukingo wa Magharibi zikionyesha kwamba ubomoaji wa mali ya Wapalestina na kuwalazimisha kuyahama makazi yao unaendelea bila kusitishwa.

Takwimu za hivi karibuni kutoka OCHA zimeonyesha kuwa hadi tarehe 22 Aprili, zaidi ya majengo 380 yamebomolewa katika majimbo ya Ukingo wa Magharibi, na kuwang'oa watu 650.

Ikiwa uharibifu utaendelea kwa kiwango hiki, kufikia mwisho wa mwaka, rekodi ya mali 1,500 zitaharibiwa, ikiwa ni idadi kubwa zaidi tangu OCHA ianze kukusanyatakwimu mwaka 2009.

Jimbo la Jerusalem limeshuhudia uharibifu mkubwa zaidi, huku majengo 80 yakibomolewa na watu 115 kuyahama makazi yao.

Kwa upande wa shule ya Al Qastal, wapokeaji msaada wanapata vifaa mbalimbali muhimu ambavyo ni pamoja na chakula na virutubisho maalum vya lishe kwa watoto na watoto wachanga ili kuhakikisha ukuaji wa afya, zao amesema Bwana. Hollingworth.

Idadi ya vifo na majeruhi inaongezeka

Habari za hivi karibuni kutoka kwa mamlaka ya afya ya Gaza zinaonyesha kuwa Wapalestina wasiopungua 34,568 wameuawa na 77,765 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza tangu Oktoba 7.

Takriban watu 1,250 waliuawa katika mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas kusini mwa Israel ambayo yalizua vita, huku zaidi ya watu 250 wakichukuliwa mateka. 

Makumi ya watu bado wanaaminika kushikiliwa katika eneo hilo na wizara ya afya ya Gaza imeonya kwamba endapo hakutopatikana usitishwaji mapigano basi Maisha ya watu yataendelea kukatiliwa zaidi.

Maandamano ya New York yameondolewa

Haya yanajiri huku mamia ya maafisa wa polisi wakiripotiwa kufuta maandamano ya wafuasi wa Palestina yaliyohusisha mamia ya watu katika Chuo Kikuu cha Columbia jijini New York Jumanne jioni.

Kwa amri ya mamlaka, polisi waliwaondoa waandamanaji ambao walikuwa wamejifungia ndani ya jengo kwenye chuo kikuu hicho huku kukiwa na ripoti za mapigano makubwa kati ya waandamanaji wapinzani usiku kucha kwenye Chuo Kikuu cha California, Los Angeles.

Saa chache kabla, mkuu wa haki za Umoja wa Mataifa Volker Türk alionya dhidi ya "hatua nzito zinazochukuliwa dhidiya baadhi ya vyuo vikuu nchini Marekani wakati wa kukabiliana na maandamano ya kupinga vita Gaza.”

Rais wa chuo kikuu cha Columbia alikuwa ametangaza kuwa mazungumzo na waandamanaji yameshindwa kufikia muafaka na taasisi hiyo haitakubali madai ya kuitaka kujitenga na Israel.