Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika yaendelea kubeba mzigo wa Malaria duniani, hatua madhubuti zachukuliwa: WHO

Mhudumu wa afya akijiandaa kutoa chanjo ya malaria wakati wa huduma ya afya ya jamii nchini Cameroon.
WHO
Mhudumu wa afya akijiandaa kutoa chanjo ya malaria wakati wa huduma ya afya ya jamii nchini Cameroon.

Afrika yaendelea kubeba mzigo wa Malaria duniani, hatua madhubuti zachukuliwa: WHO

Afya

Leo ni siku ya Malaria duniani ambapo mwaka huu inahamasisha kuongeza mapambano dhidi ya ugonjwa huu ili kuwa na ulimwengu wenye usawa zaidi kwani imebainika kuwa watu wanaoishi katika mazingira magumu ndio wanaoathirika zaidi. 

Bara la Afrika limeendelea kuongoza kwa kubeba mzigo mkubwa wa wagonjwa wa Malaria na vifo ambapo kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO kanda ya Afrika takwimu za mwaka 2022 zinaonesha bara hilo linabeba asilimia 94 ya wagonjwa huku vifo vikiwa ni asilimia 95. 

Hata hivyo shirika hilo limesema nchi za Afrika zienaendelea kuchukua hatua Madhubuti kukabilina na ugonjwa huo hasakatika kuzuia ili kuepusha vifo na mzigo wa kiuchumi wa kukabiliana na athari zake.

Matumizi ya chanjo dhidi ya malaria

Mathalani WHO imesema katika kuadhimisha siku hii nchi tatu za Afrika Magharibi ambazoo ni Benin, Liberia na Sierra Leon leo zimezindua kampeni kubwa ya utoaji chanjo ya kuokoa maisha dhidi ya Malaria ikiwalenga mamilioni ya watoto katika nchi hizo.

Pia kampeni hiyo inatoa wito wa kuongeza kiwango cha chanjo dhidi ya malaria kwa mataifa mengine ya kanda ya Afrika ya WHO.

WHO inasema uzinduzi huo wa leo wa chanjo kwa nchi tatu unafanya idadi ya nchi za Afrika zinazotoa chanjo dhidi ya malaria kama sehemu ya programu za kitaifa za chanjo kufikia 8.

Shirika hilo limesema zaidi ya nchi 30 za Afrika zimeonyesha dhamira ya kutaka kupata chanjo hiyo na WHO inasema zimepangwa kupokea na kuanza kutoa chanjo hiyo mwakani kwa msaada wa muungano wa chanjo duniani GAVI wakati juhudi zingine zikiendelea ili kupanua wigo wa vita dhidi ya malaria katika kanda ya Afrika kwa kujumuisha na mbinu zingine za muda mrefu kama matumizi ya vyandarua vyenye dawa na dawa za kujikinga.

Idadi ya dozi za chanjo zilizopatikana

Kwa Bebib WHO inasema imepokea dozi 215,900. Dozi ya malariwa inapaswa kutolewa mara nne kwa kila mtoto kuanzia umri wa miezi 5.

Profesa Benjamin Hounkpatin, waziri wa afya wa Benin amesema “Kuanzishwa kwa chanjo ya malaria katika mpango uliopanuliwa wa chanjo kwa watoto wetu ni hatua kubwa ya kupiga vita janga hili. Ningependa kuwahakikishia kuwa chanjo za malaria ni salama na zinafaa na zinachangia ulinzi wa watoto wetu dhidi ya ugonjwa huu hatari na mbayá.”

Nchini Liberia, chanjo hiyo imezinduliwa katika Kaunti ya Rivercess kusini mwa nchi hiyo na itatolewa baadaye katika kaunti nyingine tano ambazo zina mzigo mkubwa wa malaria. 

Takriban watoto 45,000 wanatarajiwa kunufaika na dozi 112,000 za chanjo iliyopo.

"Kwa muda mrefu sana, malaria imeiba kicheko na ndoto za watoto wetu. Lakini leo, kwa chanjo hii na dhamira isiyoyumba ya jjamii zetu, wahudumu wa afya na washirika wetu, ikiwa ni pamoja na GAVI, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na WHO, tunavunja mnyororo na kuwa na nyenzo yenye nguvu itakayowalinda kutokana na ugonjwa huu mbaya na vifo vinavyohusiana na janga hilo, kuhakikisha haki yao ya afya na mustakabali mwema. Hebu tukomeshe malaria nchini Libeŕia na tufungue njia kwa ajili ya jamii yenye afya na haki zaidi,” amesema Dkt. Louise Kpoto, waziri wa afya wa Liberia.

Mpango wa majaribio wa chanjo

Chanjo mbili salama na zinazofaa za RTS, S na R21 zinazopendekezwa na WHO, ni mafanikio kwa afya ya mtoto na udhibiti wa malaria. Mpango wa majaribio wa chanjo ya malaria nchini Ghana, Kenya na Malawi ulifikia zaidi ya watoto milioni 2 kuanzia mwaka 2019 hadi 2023, na kuonyesha kupungua kwa ugonjwa huo wa malaria kwa asilimia 13 katika jumla ya vifo vya watoto na kupungua kwa idadi ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini.

Nchini Sierra Leone dozi ya kwanza imetolewa kwa watoto katika kituo cha afya cha Western Area Rural ambako mamlaka imeanza kampeni hiyo ya chanjo kwa kutoa chanjo 550,000 na kisha chanjo hiyo itazambazwa katika vituo vya afya nchini kote.

"Pamoja na chanjo mpya, salama na yenye ufanisi, sasa tuna zana ya ziada ya kupambana na ugonjwa huu. Pamoja na vyandarua vilivyotiwa dawa, utambuzi na matibabu ya kutosha, na kunyunyizia dawa ndani ya nyumba, hakuna mtoto anayepaswa kufa kutokana na maambukizi ya malaria,” amesema Dkt. Austin Demby, Waziri wa Afya wa Sierra Leone.

Malaria bado ni mtihani Kanda ya Afrika

Kwa mujibu wa WHO malaria inasalia kuwa changamoto kubwa ya kiafya katika kanda ya Afrika, ambayo ni nyumbani kwa nchi 11 ambazo hubeba takriban asilimia 70 ya mzigo wa kimataifa wa malaria. Kanda hiyo ilichangia asilimia 94 ya visa vya malaria duniani na asilimia 95 ya vifo vyote vya malaria mwaka 2022, kulingana na Ripoti ya Dunia ya Malaria ya mwaka 2023.

Dkt. Matshidiso Moeti, ambaye ni Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrikaamesema "Kanda ya Afrika inasonga mbele katika utoaji wa chanjo ya malaria jambo ambalo linabadilisha mwelekeo katika mapambano yetu dhidi ya ugonjwa huu hatari. Kwa kufanya kazi na nchi wanachama na washirika wetu, tunaunga mkono juhudi zinazoendelea za kuokoa maisha ya watoto wadogo na kupunguza mzigo wa malaria katika eneo hilo."

Naye mkuu wa program za GAVi Aurelia Nguyen amesema “Leo tunasherehekea watoto zaidi kupata fursa ya nyenzo mpya ya kuokoa Maisha kupambana na moja ya magonjwa hatari zaidi Afrika yanayokatili watu wengi. Kuanzishwa kwa program hii ya janjo na kujumuishwa katika programu za kitaifa za chanjo za kawaida nchini Liberia, Sierra Leone na Benin  sanjari na mbinu zingine za kupambana na malaria kutaokoa maisha na kutoa afueni kwa familia, jamii na mifumo ya afya ambayo tayari imelemewa.”

Changamoto za vita dhidi ya malaria

WHO inasema za kupambana na malaria Afrika zimedumaa tangu mwaka 2017 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kibinadamu, fursa ndogo na huduma zisizo bora za afya, vikwazo vya kijinsia, vitisho vya kibaolojia kama dawa za kuulia wadudu na usugu wa dawa na pia mgogoro wa kimataifa wa kiuchumi.

Pia limesema mifumo duni ya afya na mapengo katika takwimu za ugonjwa huo pia vimeongeza changamoto.

Ili kurejesha mchakato wa kupambana na malaria katika msitari WHO imependekeza jitihada madhubuti katika hatua za kudhibiti malaria katika ngazi zote  hususani katika nchi zinazobeba mzigo mkubwa wa ugonjwa huo, ufadhili wa ndani na wa kimataifa, hatua zinaoongozwa na sayansi na takwimu, hatua za haraka kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi katika afya , kukumbatia utafiti na ubunifu na kuwa na ushirikiano imara katika kuratibu hatua dhidi ya malaria.

Pia WHO inatoa wito wa kushughulikia ucheleweshaji wa kutekeleza mipango ya vita dhidi ya malaria.