Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miezi sita ya vita Gaza: UN inapanga ujenzi mpya na kujikwamua

Ghorofa ambayo ni makazi ya watu imesambaratishwa katika kitongoji Al-Shaboura mjini Rafahcha
UN News/Ziad Taleb
Ghorofa ambayo ni makazi ya watu imesambaratishwa katika kitongoji Al-Shaboura mjini Rafahcha

Miezi sita ya vita Gaza: UN inapanga ujenzi mpya na kujikwamua

Amani na Usalama

Katika miezi sita ya vita huko Gaza, vita iliyoanza baada ya shambulio baya la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba mwaka jana, zaidi ya watu 33,000 wamekufa, karibu asilimia 90 ya vituo vya afya vimeharibiwa au kusambaratishwa kabisa, na zaidi ya Wapalestina milioni moja wameachwa bila makazi, kulingana na Benki ya Dunia.

Mustakbali wa eneo hilo

Bado haijulikani ni kiasi gani cha uharibifu na vifo zaidi vinawangoja wakazi wa Gaza kabla ya amani kurejea katika eneo hilo. 

Hata hivyo, katika mazingira haya yasiyo na uhakika, mashirika ya Umoja wa Mataifa tayari yanapanga mikakati ya siku zijazo.

Vita hiyo imeharibu kabisa karibu shughuli zote za kiuchumi, amesema Aya Jaafar, mwanauchumi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani ILOILO inakadiria kuwa zaidi ya ajira 200,000 zimepotea huko Gaza, ikiwa ni sawa na asilimia 90 ya soko zima la ajira kabla ya mgogoro.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa pia lilikadiria kuwa upotevu wa mapato Gaza umefikia dola milioni 4.1 kwa siku, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa asilimia 80 ya Pato la Taifa la eneo hilo linalokaliwa.

Ujenzi ulikuwa moja ya sekta muhimu zaidi huko Gaza, lakini shughuli katika sekta hiyo zimepungua kwa takriban asilimia 96, limesema shirika la ILO. 

nyingine muhimu za uzalishaji, ikiwa ni pamoja na kilimo, viwanda na huduma, pia zimesambaratika.

Baadhi ya maduka ya mikate yanaendelea kufanya kazi Gaza
© WFP
Baadhi ya maduka ya mikate yanaendelea kufanya kazi Gaza

ILO inakadiria kuwa takriban asilimia 25 ya waliouawa huko Gaza walikuwa wanaume wenye umri wa kufanya kazi, na wanawake huko kwa ujumla hawafanyi kazi. 

Jaafar amesisitiza kuwa kupotea kwa wafadhili kutamaanisha kwamba familia zitakabiliwa na matatizo baada ya kumalizika kwa vita. 

Pia inazua wasiwasi kuhusu uwezekano wa unyonyaji wa ajira ya watoto.

Mipango ya ajira itakuwa muhimu baada ya vita, Jaafar anasema. 

Inatarajiwa kuwa biashara zitahitaji ruzuku na ruzuku ya mishahara kama sehemu ya mchakato wa kufufua upya uchumi wa ndani.

Uwekezaji wa ILO pia utakuwa muhimu katika kutoa fursa za ajira huku ikijenga upya miundombinu iliyoharibika.

Kuanzisha upya uzalishaji wa ndani

Upatikanaji wa chakula bado ni suala muhimu la kibinadamu, hasa kaskazini mwa Gaza.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, Abdel Hakim Elwaer, kabla ya mzozo huo, kilimo na uvuvi vilishamiri huko Gaza, na watu wengi pia waliweza kujipatia matunda na mboga kwa kiasi.

Sasa, karibu nusu ya ardhi yote ya kilimo imeharibiwa na ugavi wa uagizaji bidhaa wa sekta binafsi umetatizwa anasema Elvaer.

Hakuna chakula cha kutosha kwa mifugo iliyosalia, ambayo baadhi ya Wagaza wanaripotiwa kuila wenyewe kutokana na ukosefu wa chakula kingine. 

FAO imebainbisha kuwa ilichukua miezi mitatu kupata idhini kutoka kwa mamlaka ya Israeli kwa usambazaji wa tani 500 za chakula cha mifugo.

Watu Gaza wanatarajiwa kuhitaji msaada kwa miaka mingi ijayo
© UNRWA
Watu Gaza wanatarajiwa kuhitaji msaada kwa miaka mingi ijayo

"Wakazi wa Gaza wako tayari kuanza tena uzalishaji wa ndani," amesema Elvaer akiongeza kuwa, "lakini wanahitaji mbegu, mbolea na dawa."

Kufufua sekta ya kilimo cha biashara hadi viwango vya kabla ya Oktoba 7 itakuwa changamoto. 

Msemaji huyo wa FAO anaamini kwamba msaada wa kibinadamu utahitajika kwa angalau miaka miwili hadi "kiwango fulani cha utulivu, uaminifu na imani kitakapopatikana tena ambacho kitaruhusu watu kurejea kwenye biashara zao.”

Gharama na muda wa ujenzi upya

Ni mapema mno kusema ni kiasi gani ujenzi wa Gaza utagharimu kadri uharibifu unavyoendelea.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Rami Alazze wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Biashara na Maendeleo UNCTAD, itachukua miongo kadhaa, pamoja na nia ya jumuiya ya kimataifa na uwekezaji wa makumi ya mabilioni ya dola, kuifufua Gaza.

Benki ya Dunia inakadiria gharama ya uharibifu wa mali hadi mwisho wa Januari 2024 pekee kuwa ni dola bilioni 18.5. 

Idadi hii haijumuishi gharama ya msaada wa kibinadamu kwa watu. Kwa kuongezea, mabomu ambayo hayajalipuka itabidi kusafishwa katika eneo lote la Gaza kazi ambayo itachukua miaka, kulingana na ofisi ya Umoja Huduma ya uteguzi wa mabomu UNMAS.

Kutokuwa na uhakika 

Haijulikani ikiwa pesa zitatengwa kwa ajili ya ujenzi mpya, na kuna mambo mengine mengi tu. 

Je, ukarabati utaanza mara tu baada ya kumalizika kwa uhasama, ikiwa kizuizi cha Israeli, ambacho kimekuwa kikifanya kazi kwa miaka 18, kitakomeshwa, kama Gaza inaweza kuendeleza ukuaji wa asilimia 10 wa uchumi katika miaka ijayo, kiwango cha maendeleo ambacho kitahitajika hadi mwaka 2035 ili "kurejea katika hali iliyokuwa kabla ya vikwazo vya 2006." Leo wataalam wanahoji maswali haya yote leo.

Mkazi wa Gaza akiangalia uharibifu uliofanywa kwenye mtaa wake
© UNRWA
Mkazi wa Gaza akiangalia uharibifu uliofanywa kwenye mtaa wake

Hata hivyo, katika hali mbaya zaidi, ikiwa uchumi unakua kwa asilimia 0.4 kila mwaka kama ilivyokuwa katika miaka ya hivi karibuni, itachukua Gaza miongo saba kurejea katika viwango vya kiuchumi vya mwaka 2022, anasema Alazze.

"Tunapaswa kuwapa watu matumaini ya siku zijazo tena, na nadhani hilo linaweza tu kufanywa kupitia mpango wa kina wa kisiasa unaojumuisha suluhisho la serikali mbili," amesema.