Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA yawezesha wanawake na wasichana Zambia kujikwamua dhidi ya ukatili wa kijinsia

Mwaka*, mwanamke aliyenusurika ukatili wa kijinsia, alikaa kwenye makazi ya Laweni baada ya kutoroka unyanyasaji wa mumewe.
© UNFPA Zambia/Jadwiga Figula
Mwaka*, mwanamke aliyenusurika ukatili wa kijinsia, alikaa kwenye makazi ya Laweni baada ya kutoroka unyanyasaji wa mumewe.

UNFPA yawezesha wanawake na wasichana Zambia kujikwamua dhidi ya ukatili wa kijinsia

Wanawake

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani na afya ua uzazi UNFPA linavisidia vituo ambavyo vinawawezesha wanawake na wasichana nchini Zambia kuondokana na mzunguko wa ukatili wa kijinsia.

"Tulianza maisha yetu pamoja tangu mwanzo. Nilifurahia maisha, nilijawa na shauku na upendo wa kipofu,” anasema mama wa watoto watatu aitwaye Mwaka ambalo si jina lake halisi. "Kisha, baadaye, unagundua mtu huyu ni nani na wa aina gani."

Akiwa na miaka 22, Mwaka aliolewa na mwanaume ambaye alikutana naye kupitia kwa mama yake. Alikuwa ameajiriwa kufanya kazi kama mwalimu wa sayansi na Kiingereza katika shule ya binafsi ya mama yake.

Akiwa mdogo na mwenye mvuto wa mapenzi, Mwaka hakuona jinsi mwenzi wake alivyokuwa akimdanganya na kumnyanyasa. 

"Alinibana, alinifanya nijihisi si salama na sina akili," ameliambia shirika la UNFPA. "Mwishowe, nikawa mtu wa kuomba msamaha kwa makosa yote ambayo sikufanya."

Ukatili wa kijinsia umeshamiri Zambia 

Kwa mujibu wa UNFPA kote nchini Zambia, zaidi ya theluthi moja ya wanawake waliripoti mwaka 2018 kwamba walifanyiwa ukatili wa kimwili tangu wakiwa na umri wa miaka 15. 

Wakati huo huo, karibu nusu ya wanawake wote waliowahi kuolewa wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamesema wamenusurika unyanyasaji wa kihisia, kimwili au kingono kwa mume au mpenzi.

Wakati wa ndoa ya Mwaka kwa miaka 11, mume wake alizidi kuwa jeuri alikataa kumwacha aondoke nyumbani peke yake na kumshambulia na kumwachia majeraha usoni na mwilini mwake. Alitishia kumuua yeye na watoto wake, wakati mmoja hata kuweka kisu kwenye shingo ya Mwaka.

Mwaka anasema "Kama ninavyoona sasa, muwe wangu alitaka kuwa na udhibiti kamili juu yangu".

Kwa bahati nzuri, Mwaka aliweza kujitenga. Kwa msaada kutoka kwa jamaa, yeye na watoto wake walimtoroka mumewe na kusindikizwa na polisi hadi kwenye kimbilio la karibu ambalo ni makazi ya kituo cha Laweni.

Mahali salama na tulivu

Katika lugha ya Chewa, Laweni inaweza kumaanisha “mapumziko au mahali pa usalama”. Na hivyo ndivyo wengi wa wanawake na wasichana wanaokuja kukaa kwenye makazi haya hutafuta.

Makazi ya kituo hicho yanaendeshwa na Jumuiya ya Vijana Wanawake wa Kikristo (YWCA) ya Zambia, na makao hayo yanayoungwa mkono na UNFPA yanahudumia zaidi waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia, wa biashara haramu ya binadamu, pamoja na wale wanaokabiliwa na mimba za utotoni. 

YWCA inawapa wanawake na wasichana hao fursa ya kupata chakula, mavazi, matibabu, matunzo ya ujauzito, msaada wa kisheria na ushauri wa kisaikolojia na kijamii.

"Wanapokuja kwenye makazi, wanawake hubeba mzigo mzito," Grace, ambaye ni mshauri, ameliambia shirika la UNFPA. 

"Lakini hapa, tunajenga fursa salama kwao kufunguka na kuzungumzia juu ya hisia zao za kweli na changamoto zinazowakabili."

Mwaka alipofika kwa mara ya kwanza katika makazi ya Laweni, alijihisi faraja kwamba uzoefu wake wa unyanyasaji ulikuwa umeisha. 

Lakini hisia zingine pia ziliingia za hofu. Hisia ya kina ya kupoteza kila kitu, uuvunjika moyo na kujiamini kwake.

Alitilia shaka uamuzi wake wa kumwacha mumewe na kuwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wa watoto wake. Lakini alipotathimini kiwewe alichokipata, alianza kupata nafuu kihisia.

"Akili yangu ilifunguka kuona mitazamo mipya," Mwaka alisema. "Nilianza kuwa na matumaini, na niliweza kushughulikia hisia na maumivu yangu na kupata tena nguvu na uvumilivu."

Mwaka hayuko peke yake

Mwaka hayuko peke yake katika suala hili ni mabadiliko ambayo Neema ambaye pia si jina lake halisi ameshuhudia hapo awali kwa wanawake wengine. "Wanajikomboa kutoka kwenye woga, aibu, hatia, hasira, chuki na kujichukia," anasema. "Muhimu zaidi, wanajua kuwa hawako peke yao."

Washauri wanapatikana kwa wanawake na wasichana kwenye makazi mchana na usiku. 

Huduma za kisheria pia zinapatikana, Mwaka alikuwa na wakili aliyepangiwa kesi yake na hati ya ulinzi iliyotolewa dhidi ya mumewe.

"Ninajihisi furaha sana kuwa hapa na kuwa sehemu ya safari ya wanawake hawa," anasema Grace

Na kuongeza kuwa “Nimeona jinsi wanawake wanavyoteseka. Ninataka tu kuwasaidia kuzungumza na kujua wanachoweza kufanya licha ya yale waliyopitia hapo awali. Ninawaona kama dada na mabinti. Ninawaamini."

Mwaka* akionyesha moja ya ubunifu wake wa kisanii.
© UNFPA Zambia/Jadwiga Figula
Mwaka* akionyesha moja ya ubunifu wake wa kisanii.

Maisha mapya

Baada ya kukaa kwa miezi michache katika makao ya YWCA, Mwaka aliweza kuhama na watoto wake hadi nyumbani kwa mama yake.

Makao ya wanawake katika makazi ya Laweni yanatofautiana sana, na wengine wanaishi huko kwa wiki mbili huku wengine hadi mwaka mmoja au zaidi.

Kwa mwanzo wake mpya, Mwaka aliwaandikisha watoto wake katika shule mpya na akaanza kufanya kazi ya muda kama karani wa ofisi. 

Akiwa ameketi jikoni kwake mwezi Julai 2023, mchoraji huyo mahiri alitafakari juu ya uzoefu wake na jinsi walivyombadilisha kifikra akiwa amezungukwa na ubunifu wake wa kupendeza.

"Nilijifunza mambo muhimu kutokana na kile kilichotokea," anasema Mwaka na kuongeza kuwa "Unapojitenga na mnyanyasaji, unaweza kuona thamani ya wewe ni nani. Na mara tu unapotambua thamani ya wewe ni nani, utastawi.”