Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za kijasiri zinahitajika ili kutokomeza mateso na ukatili Haiti – UN

Katikati ya mji wa Port-au-Prince Haiti machafuko yamesababisha kundi kubwa la watu kutawanywa
© UNICEF/Herold Joseph
Katikati ya mji wa Port-au-Prince Haiti machafuko yamesababisha kundi kubwa la watu kutawanywa

Hatua za kijasiri zinahitajika ili kutokomeza mateso na ukatili Haiti – UN

Haki za binadamu

Ufisadi, ukwepaji sheria na ukosefu wa utawala bora uliogubikwa na viwango vya juu vya uhalifu unaofanywa na magenge, vimemomonyoa utawala wa kisheria nchini Haiti na kudhoofisha taasisi za serikali ambazo zinakaribia kusambaratika, imesema ripoti mpya ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu iliyochapishwa hii leo huku ikitaka hatua za haraka na za kijasiri zichukuliwe ili kukabiliana na hali ya janga inayokumba taifa hilo la Karibea.

Tweet URL

Ripoti hiyo inayojikita kwenye kipindi cha kuanza tarehe 25 Septemba 2023 hadi tarehe 29 Februari 2024, inaweka bayana vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu usababishwao na ukosefu wa usalama huku wananchi wakishindwa kufurahia haki zao za msingi.

Vifo vyaongezeka, magenge ya uhalifu yaua waume mbele ya wake zao

Inajumuisha taarifa kutoka kitengo cha Haki za Binadamu cha Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Haiti, BINUH, na taarifa zilizokusanywa na William O’Neill ambaye ni Mtaalam Maalum wa Haki za Binadamu Haiti aliyeteuliwa na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu.

Idadi ya watu waliouawa na waliojeruhiwa kutokana na uhalifu wa magenge imeongezeka kwa kiasi kikubwa kwani mwaka 2023, waliouawa walikuwa 4,451 ilihali katika miezi mitatu ya mwanzo ya 2024 idadi ni 1,554.

Magenge ya uhalifu yameendelea kutumia ukatili wa kingono kutesa, kuadhibu na kudhibiti wananchi. Wanawake wamekuwa wanabakwa pindi magenge ya uhalifu yanapovamia makazi yao,  na katika matukio mengi, wanawake hao wameshuhudia waume zao wakiuawa mbele ya macho yao.

Les Cayes, mji mdogo ulio kusini mwa Haiti.

Kwa mujibu wa ripoti,  baadhi ya wanawake wanalazimishwa kuingia kwenye uhusiano wa kingono na wafuasi wa magenge ya uhalifu, uhusiano ambao unagubikwa na manyanyaso.

Halikadhalika, ubakaji wa mateka unaendelea kutumika kama njia ya kulazimisha wanafamilia kulipa kikombozi. Vitendo vya ukatili wa kingono, vinaripotiwa kwa kiwango kidogo, na hata vikiripotiwa hakuna hatua inayochukuliwa dhidi ya wahalifu.

Usalama ni kipaumbele Haiti- Türk

Akizungumza baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo, Kamishna Mkuu wa Umoja wa MAtaifa wa  Haki za Binadamu Volker Türk amesema kutatua suala la ukosefu wa usalama linasalia kuwa kipaumbele ili kulinda wananchi na kuzuia machungu zaidi kwa raia.

“Ni muhimu pia kulinda taasisi zinazotakiwa kusimamia utawala wa sheria, taasisi ambazo zimeshambuliwa hadi hazina uwezo wa kufanya chochote,” amesema Türk akiongeza kuwa watoto wa kike na wa kiume nao wanaendelea kutumikishwa na kunyanyaswa na magenge hayo ya uhalifu, ambapo watoto hao wanashindwa kuondoka kwa hofu ya kulipiziwa visasi, ambavyo katika baadhi ya matukio, wale waliofanya hivyo waliuawa.

Amesisitiza kuwa vitendo vyote hivyo lazima vikome.

Ripoti inasisitiza umuhimu wa kupeleka haraka kikosi cha kimataifa cha usaidizi wa usalama Haiti, ili kusaidia Polisi wa Taifa kukomesha ghasia, kulinda raia kwa ufanisi na kurejesha utawala wa sheria.

Soma ripoti nzima hapa.