Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Tangu vita ianze makombora ya Israel yamepiga moja kwa moja shule 212

Mtoto akipita kwenye mitaa ya jimbo la Khan Younis huku majengo yakiwa yamesambaratishwa kwa makombora. Jimbo hili liko kusini mwa Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba
Mtoto akipita kwenye mitaa ya jimbo la Khan Younis huku majengo yakiwa yamesambaratishwa kwa makombora. Jimbo hili liko kusini mwa Ukanda wa Gaza.

GAZA: Tangu vita ianze makombora ya Israel yamepiga moja kwa moja shule 212

Amani na Usalama

Mashambulizi makubwa yanayofanywa na Israeli dhidi ya Gaza kufuatia mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas dhidi ya taifa hilo yamejumuisha makombora yaliyorushwa moja kwa moja dhidi ya shule 212  kwenye eneo hilo lililozingirwa, umeonesha uchambuzi mpya uliofanywa kwa pamoja kati ya Umoja wa Mataifa na wadau wake.

Picha za setilaiti zinaonesha angalau shule 53 zimeharibiwa kabisa tangu kuanza kwa vita Oktoba 7, 2023 na takribani ongezeko la asilimia 9 la mashambulizi dhidi ya shule kuanzia katikati ya mwezi uliopita wa Februari, imesema ripoti hiyo ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, shirika la kiraia la Education Cluster na Save the Children.

Mashambulizi dhidi ya maeneo ya shule yamezidi kusababisha hali ya kiutu ambayo tayari ni mbaya kuwa mbaya zaidi, imesema ripoti hiyo wakati huu ambapo Israeli inaimarisha mashambulizi yake kutokea angani, ardhini na baharini kwenye karibu eneo lote la Ukanda wa Gaza.

Mkazi wa Khan  Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza akiburuza mali zake kwenye mitaa ya jimbo hilo ambako mashambulizi makali yanaendelea kufanywa na jeshi la Israeli
© UNICEF/Eyad El Baba
Mkazi wa Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza akiburuza mali zake kwenye mitaa ya jimbo hilo ambako mashambulizi makali yanaendelea kufanywa na jeshi la Israeli

Uharibifu umesambaa

Kati ya majengo 563 ya shule Gaza, 165 kati ya 212 yaliyoshambuliwa moja kwa moja, yako kwenye maeneo yaliyotengwa na jeshi la Israeli kuwa eneo la kimbilio. Hii inajumuisha shule 62 zilizoku jimbo la kusini la Khan Younis, na 76 kati ya shule 94 kwenye jimbo la Gaza upande wa kaskazini.

Zaidi ya maeneo ya shule moja kati ya mbili zinazoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA zimeshambuliwa, imesema ripoti hiyo, sambamba na majento ya serikali yakilengwa na makombora ya Israeli wakati wa operesheni yake ya ardhini.

Ikimulika kiwango cha madhara ya vita hiyo, ripoti hiyo inadokeza kuwa zaidi ya wanafunzi 625,00 na walimu 22,000 awali walikuwa wanakwenda kwenye shule 813.