Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 5.7 walazimika kuwa wakimbizi wa ndani Mashariki mwa DRC-UNHCR

Baba wa watoto sita anatafuta usalama kwa familia yake katika eneo la makazi ya muda karibu na Goma baada ya mkewe kuuawa na bomu huko Sake, jimbo la Kivu Kaskazini.
© UNHCR/Blaise Sanyila
Baba wa watoto sita anatafuta usalama kwa familia yake katika eneo la makazi ya muda karibu na Goma baada ya mkewe kuuawa na bomu huko Sake, jimbo la Kivu Kaskazini.

Watu milioni 5.7 walazimika kuwa wakimbizi wa ndani Mashariki mwa DRC-UNHCR

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi (UNHCR) limetoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kutokana na ongezeko la hatari kwa watu waliokimbia makazi yao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. 

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa shirika hilo Matthew Saltmarsh mjini Geneva Uswisi hii leo “Miaka miwili ya mizozo katika maeneo ya Kivu Kaskazini huko Rutshuru na Masisi imewalazimu zaidi ya watu milioni 1.3 kukimbia makazi yao ndani ya DRC, na kusababisha jumla ya watu milioni 5.7 kuwa wakimbizi wa ndani katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri.”

Ameongeza kuwa tangu mapigano makali yashike kasi katika mji wa Sake, tarehe 7 Februari, karibu watu 300,000 wamewasili katika jiji la Goma, ambako hali ilikuwa mbaya. 

Watu zaidi ya 85,000 walikuwa wamekimbia ghasia hizo hizo na kutafuta makazi katika eneo la Minova la Kivu Kusini, ambalo tayari lilikuwa limepokea watu 156,000 waliokimbia makazi yao tangu Januari.

Mauaji na ubakaji

Kwa mujibu wa UNHCR shambulio la makombora katika kituo cha biashara tarehe 20 Machi lilimuua mwanamke mkimbizi wa ndani na kuwajeruhi wengine watatu, wakiwemo watoto wawili.

Ripoti za milipuko ya mabomu ya kiholela huko Sake na Goma katika wiki za hivi karibuni, ambayo iliua zaidi ya watu 30 na kujeruhi takriban 80, pia zilitia wasiwasi mkubwa. 

Mwaka jana 2023, shule 25 zilichukuliwa na vikundi vyenye silaha visivyo vya serikali katika maeneo ya Masisi na Rutshuru pekee, na shule zingine 17 zilishambuliwa. 

Mwaka huu 2024, shule saba zimeharibiwa na milipuko ya mabomu.

Pia mwaka 2023, katika eneo la Kivu Kaskazini pekee, kulikuwa na kesi 50,159 zilizoripotiwa za unyanyasaji wa kijinsia, zaidi ya nusu ya kesi hizo zikiwa ni ubakaji, asilimia 90 ya waathirika hao walikuwa wanawake na wasichana, wakati asilimia 37 walikuwa ni watoto.

Machafuko lazima yakome kuokoa maisha

UNHCR imekuwa ikitoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa ghasia hizo na kuzitaka pande zote katika mzozo huo kuheshimu na kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu, na kuwalinda raia.

Hatua za kibinadamu zilioongezeka katika majimbo ya Mashariki kati ya Juni na Desemba 2023 msaada wa kuokoa Maisha ulifikia zaidi ya watu milioni 3.1.

UNHCR imetoa hifadhi ya dharura kwa zaidi ya watu 40,000 walio katika mazingira magumu zaidi waliofika Goma, lakini hii imesaidia sehemu ndogo tu ya hitaji hilo.

UNHCR imepokea asilimia 14 tu ya dola milioni 250 zinazohitajika kwa ajili ya kukabiliana na hali ya wakimbizi na mahitaji yao nchini DRC kwa mwaka 2024.

Ukosefu wa fedha unatishia utoaji wa misaada, na hivyo kuzidisha janga baya la kibinadamu katika eneo hilo.