Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lapitisha azimio linalodai kusitishwa mapigano mara moja Gaza wakati wa Ramadhan

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield akipiga kura ya kujizuia kwenye Baraza la Usalama wakati wa upigaji kura uliopitisha azimio la kudai usitishaji mapigano mara moja Gaza
UN Photo
Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield akipiga kura ya kujizuia kwenye Baraza la Usalama wakati wa upigaji kura uliopitisha azimio la kudai usitishaji mapigano mara moja Gaza

Baraza la Usalama lapitisha azimio linalodai kusitishwa mapigano mara moja Gaza wakati wa Ramadhan

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo Jumatatu limepitisha azimio la kutaka kusitishwa kwa mapigano mara moja kwa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote waliosalia na haja ya dharura ya kupanua wigo wa uingizaji wa misaada katika Ukanda wa Gaza. 

Azimio hilo limepitishwa kwa kura 14 za kuunga mkono huku Marekani ikijizuia kupiga kura.

Azimio hilo lazima litekelezwe

Akizungumza mara tu baada ya kura hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X zamani Twitter amesema kwamba “azimio lililokuwa likisubiriwa kwa muda mrefu lazima litekelezwe. Na kushindwa kwa Baraza kufanya hivyo hakutaweza kusamehewa."

Algeria inasema rasimu ya azimio itakomesha umwagaji damu Gaza

Balozi wa Algeria kwenye Umoja wa Mataifa , Amar Benjama amesema rasimu hiyo ya azimio itakomesha mauaji ambayo yamekuwa yakiendelea kwa miezi mitano sasa Gaza.

Tweet URL

Amesema "Umwagaji damu umekwenda kwa muda mrefu sana. Hatimaye, Baraza la Usalama limeitikia wito wa jumuiya ya kimataifa na Katibu Mkuu."

Rasimu hiyo ya azimio inatoa ujumbe wa wazi kwa watu wa Palestina, amesema.

Na kuongeza kuwa "Jumuiya ya kimataifa, kwa ujumla, hahawatupa watu wa Palestina. Kupitishwa kwa azimio la leo ni mwanzo wa kufikia matarajio ya watu wa Palestina, kukomesha umwagaji damu bila masharti yoyote."

Azimio la pita, Marekani yajizuia kupiga kura

Marekebisho ya maneno ya mdomo yaliyopendekezwa na Urusi hayakupita kwa sababu ya ukosefu wa kura za kutosha.

Lakini katika kura hiyo kubwa, kulikuwa na wajumbe 14 waliounga mkono, huku Marekani ilijizuia kupiga kura. Kwa hivyo azimio limepitishwa.

Jambo la kushikilia katika kura hiyo ni kuondolewa kwa neno "kudumu" kutoka kwa toleo la awali la rasimu. Sasa llimewekwa neno "kusitishwa kwa mapigano mara moja".

Urusi yapendekeza marekebisho

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia amesema ukweli kwamba neno "kudumu" katika aya ya kwanza ya ya azimio hilo lilibadilishwa na lugha dhaifu "haikubaliki".

Ameendelea kusema kwamba sote tulipokea maagizo ya kupiga kura kwenye maandishi ambayo yalikuwa na neno 'kudumu' na kitu kingine chochote kinaweza kuonekana kama ruhusa kwa Israeli kuendelea na mashambulizi yake.

Kwa hivyo, ujumbe wake umependekeza marekebisho ya mdomo ili kurejesha neno "kudumu" kwenye rasimu ya azimio hilo.

Balozi wa kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa Gilad Erdan, akizungumza kwenye Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati likiwemo suala la Palestina
UN Photo
Balozi wa kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa Gilad Erdan, akizungumza kwenye Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati likiwemo suala la Palestina

Ukosefu wa lawama dhidi ya Hamas ni fedheha: Israel

Baada ya kupitishwa kwa azimio hilo Gilad Erdan, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa , amehoji ni kwa nini Baraza la Usalama "linabagua" miongoni mwa waathiriwa?, akikumbusha kwamba lililaani shambulio baya kwenye ukumbi wa tamasha huko Moscow siku ya  Ijumaa, lakini lilishindwa kulaani mauaji ya tamasha la muziki la Nova la tarehe 7 Oktoba mwaka jana.

"Wananchi, bila kujali wanaishi wapi, wanastahili kufurahia muziki kwa usalama na amani na Baraza la Usalama linapaswa kuwa na uwazi wa kimaadili kukemea vitendo hivyo vya ugaidi kwa usawa, bila ubaguzi," amesema.

Na kuongeza kuwa "Cha kusikitisha, leo vilevile Baraza hili lilikataa kulaani mauaji ya Oktoba 7 hii ni aibu".

Bwana. Erdan amebainisha zaidi kwamba kwa muda wa miaka 18 iliyopita, Hamas ilianzisha mashambulizi yasiyoisha dhidi ya raia wa Israel. 

Amesisitiza kuwa ni "Maelfu kwa maelfu ya makombora na mabomu ya kiholela dhidi ya raia," 

Ameongezea kwamba ingawa azimio hilo lilishindwa kulaani Hamas, "limeeleza jambo ambalo lilipaswa kuwa nguvu ya kimaadili. Azimio hili linalaani uchukuaji wa mateka, na kukumbuka kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa," amesema, akisisitiza kuwachukua mateka raia wasio na hatia, ni uhalifu wa kivita.

"Linapokuja suala la kuwarejesha mateka nyumbani, Baraza la Usalama halipaswi kukubaliana na maneno pekee bali kuchukua hatua, hatua za kweli," aliongeza.

Mwangalizi wa kudumu wa eneo linalokaliwa la Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Riyad Mansour,akizungumza baada ya upigaji kura kwenye Baraza la Usalama kuhusu azimio linalodai usitishaji mapigano mara moja Gaza
UN Photo
Mwangalizi wa kudumu wa eneo linalokaliwa la Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Riyad Mansour,akizungumza baada ya upigaji kura kwenye Baraza la Usalama kuhusu azimio linalodai usitishaji mapigano mara moja Gaza

Mateso ya Gaza lazima yakome sasa: Palestina

Riyad Mansour, Mwangalizi wa Kudumu wa eneo la Palestina kwenye Umoja wa Mataifa amesema imechukua muda wa miezi sita, huku zaidi ya Wapalestina 100,000 wakiuawa na kujeruhiwa, hatimaye kudai kusitishwa kwa mapigano mara moja.

Wapalestina huko Gaza wamepiga kelele, kulia, kulaani na kuomba, na kukaidi tabia mbaya mara kwa mara. Sasa wanaishi na njaa huku wengi wakifukiwa chini ya vifusi vya nyumba zao.

"Tatizo lao lazima lifikie ukomo na lazima lifikie ukomo mara moja," amewaambia mabalozi.

 Amesema utawala wa sheria za kimataifa unaharibiwa na jinai za Israel. Badala ya kutekeleza agizo la lazima kutoka kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC, Israel imeongeza maradufu operesheni zake.

Amesema Wapalestina wameuawa ikiwa wangebaki, au kuondoka, na sasa Israel inatishia uvamizi wa Rafah.

Pia wameendelea na uchochezi wao kwa Umoja wa Mataifa, wakimshambulia mkuu wa Umoja wa Mataifa na shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA. Umoja wa Mataifa lazima ulindwe, amesema.

"Uchochezi huu wa kutisha una madhara halisi ya maisha kwa Umoja wa Mataifa na wahudumu wa kibinadamu ambao wanalengwa na mashambulizi, wanaouawa, kukamatwa na kuteswa", amesema.

Pia una matokeo mabaya kwa maisha kwa kuzuia misaada ya UNRWA. "Ni wakati wa hatua hizi zote za Israeli kudhibitiwa kwa hatua kubwa za kimataifa", ameongeza alikaribisha kupitishwa kwa azimio hilo na akatoa salamu za umoja wa Waarabu katika kudai usitishaji vita.

"Hii lazima iwe hatua ya mabadiliko, hii lazima iongoze kuokoa mashinani. Hii lazima iashirie mwisho wa shambulio hili la ukatili dhidi ya watu wetu", amesema, akitangaza kwamba taifa lake lote lilikuwa linauawa.